Mtume (saaw) Alikuwa Nabii na Mtawala

Wakati tukiwa bado ndani ya mwezi wa Rabi ul awwal, mwezi aliozaliwa kipenzi chetu na kiongozi wetu Mtume SAAW, ni vyema kukumbushana juu ya haiba ya Mtume SAAW kwa usahihi wake kwamba alikuwa Nabii na mtawala.

Kwa kuangalia sira ya Mtume SAAW na nusus mbali mbali za kisharia tutaona wazi bila ya tembe ya shaka kuwa Mtume (SAAW) mbali ya U-Nabii wake pia alikuwa Mtawala aliyetawala, kuendesha na kusimamia dola.

Mtume (SAAW) alikuwa ni kiongozi wa wazi tokea kupewa kiapo yaani Baia’h ya pili ya Aqaba. Katika Sira ya Ibn Hisham tunaona kuwa Mtume (SAAW) alipokutana na watu wa makabila ya Aus na Khazraj walipokuja Makkah aliwaambia:

Nitaingia katika makubaliano ya kiapo pamoja nanyi muda wa kwamba mutanihifadhi kama mnavyowahifadhi wanawake wenu na watoto wenu”. Baraa (ra) akanyoosha mkono wake ili ambayiishe kwa hayo, akasema: “Tumekubayiisha ewe Mtume wa Allah, wallahi sisi ni watu wa vita na watu wa silaha na tumezirithi kutoka kwa mababu na mababu”. Na kabla Baraa (ra) hajamaliza maneno yake Abu Haitham bin Tayhan akamkatiza kwa kusema: Ewe Mtume wa Allah kati yetu na watu (yaani Mayahudi ) kuna mkataba na sisi tutauvunja , na iwapo tutafanya hilo na kisha Allah akakupa ushindi utarudi kwa watu wako na kutuacha?

Mtume (saw) akatabasamu na akasema Bali damu yenu ni damu yangu na kitukufu chenu ni kitukufu kwangu, mimi ni katika nyinyi na nyinyi ni katika mimi, tutapigana na yeyote mutakaepigana nae na nitaweka amani  na Yule mlioweka nae amani.”

Baadae  wakatoa baia’h  kwa Mtume (SAAW) na kutamka “Tumembayiisha Mtume (saw) juu ya kusikiza na kutii katika mazito yetu  na mepesi yetu, na yanayotuchangamsha na yanayotuchukiza na tusiwe wenye kujipendelea na wala tusizozane kuhusu utawala na wanaohusika”.

Kisha Mtume(SAAW) akasema: Nitoleeni watu kumi na mbili kati yenu ili wawe ni wasimamizi juu ya watu wao”.

Jamii ya Madina haikuwa ni mkusanyiko holela wa Waislamu, bali ilikuwa na muundo na fungamano maalum. Mtume (SAAW) tangu alipoingia Madina aliweza  kuunda mfumo wa kisiasa na kuweka taratibu, kanuni, udhibiti na utii katika jamii. Huku akifanya kazi zilizo chini yake akiwa ni mtawala. Mtume (SAAW) alisaini mikataba pamoja na Mayahudi, Banu Dhamrah na Banu Madlaj. Baadae mikataba ilifungwa pamoja na Makureshi na watu wa Ayla, Al-Jarba na Uzra.

Baadhi ya nukta muhimu katika moja ya mikataba zinasomeka hivi:

  1. Marafiki wa Mayahudi ni kama wao. Asitoke yeyote nje ya Madina isipokuwa kwa idhini ya Muhammad
  2. Yathrib ni tukufu kwa watu wa mkataba.
  3. Iwapo mvutano au ugomvi utatokea na ikahofiwa uharibifu basi marudio yake ni kwa Allah Azzah wa Jallah na kwa Mtume wake SAAW.
  4. Makureshi na wasaidizi wao wasipewe hifadhi.

Mtume (saw) akiwa ni kiongozi na mtawala wa dola, aliunda muundo maalum wa dola (structure of the state) unaojumuisha kuwa na wasaidizi katika utawala na masuala ya kiutendaji. Walikuwepo viongozi kama Amir wa jihadi, Ma-wali (Ma-Gavana), Ma-kadhi, Majlis Ummah (Shura) nk.

Imepokewa na Tirmidhi na Hakim kutoka kwa Abi Said Al Khudhri amesema: Amesema Mtume (SAAW):

“Mawaziri (wasaidizi) wangu wawili kutoka mbinguni ni Jibril na Mikail, na katika ardhi ni Abubakar na Umar”.

Mtume (SAAW alisimamia jeshi na kuteua viongozi/maamiri wa Jihad. Alimteua Abu Salama Ibn Abdil Asad (ra) kuwa ni kamanda wa kikosi cha watu 150 na alimkabidhi bendera. Katika vita vya Mu’tah alimchagua Zaid bin Harithah kuwa kiongozi, na akawateuwa viongozi baada yake iwapo atauawa.

Aidha, Mtume SAAW aliwahi kumteuwa Usama bin Zaid katika uongozi kama huo awali. Imepokewa na Muslim kutoka kwa Suleiman bin Buraid kutoka kwa baba yake:

Mtume (SAAW alipokuwa akimteuwa mtu kuwa Amiri wa jeshi au misafara alimuusia uchamungu kwanza yeye mwenyewe, kisha Waislamu wote kwa ujumla kufanya mambo ya kheri”

Dola ya Kiislamu ilipotanuka, Mtume (SAAW) akiwa ni mtawala mweledi (stateman) alichagua ma-wali na ma-a’mil katika kila wilaya na miji ili wasimamie uendeshaji wa mambo ya watu na kutatua matatizo yao. Alimchagua Utba bin Usayd (ra) kuwa wali wa Makkah, Muadh bin Jabal kuwa wali wa al-Janad nk.

Mtume (SAAW kutokana na mamlaka yake ya utawala alichaguwa ma-kadhi kwa lengo la kutoa hukumu kwa njia ya kulazimisha ili itatuke mizozo baina ya watu. Mfano, alimteuwa Ali (ra) kuwa kadhi wa Yemen na kumuelekeza, akasema SAW:

Wakikujia watu wawili ili uwahukumu basi usimhukumu wa mwanzo mpaka umsikilize wa pili ndipo utakapojua vipi utatoa hukumu” (Tirmidhi na Ahmad)

Ili upatikane ufanisi mzuri katika uendeshaji na kuhudumiwa raia vizuri zaidi, Mtume (SAAW) aliunda baraza la ushauri (Shura). Alikuwa akitaka ushauri kwa watu weledi wakiwemo Muhajirun na Ansar wanaowakilisha watu wao. Na katika watu maalum katika Masahaba wake kuwafanya makhsusi kwa ushauri kama Abubakar, Umar, Hamza, Ali, Salman Alfarisy, Hudhaifa nk.                                                   

Kwa kuzingatia haya ambayo ni baadhi ya aliyoyatekeleza Mtume (SAAW) ikiwemo kufunga mikataba baina ya tawala, kuweka katiba na kanuni za kuendesha mambo ya serikali, kuunda jeshi, kutuma mabalozi, kuweka magavana (wali) katika kila wilaya za dola nk. ni wazi kuwa Mtume SAAW alikuwa ni mtawala. Lakini kuwa kwake mtawala hakukumuondoshea cheo cha Utume wake.

Ni wajibu wetu katika mwezi huu wa Rabi ul awwal khasswa na wakati wote kuwakumbusha Waislamu na wasiokuwa Waislamu juu ya usahihi huu wa haiba hii ya Mtume SAAW ambae ni kigezo chema kwetu Waislamu katika kila kipengee cha maisha yetu.

#MuhammadNiNuruKwaUlimwengu

Risala ya Wiki No. 21              

16 Rabi ul awwal 1440 Hijri    | 24 -11- 2018 Miladi

Afisi ya Habari –   Hizb ut- Tahrir Tanzania

http://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!