Kampeni ya ‘Elimu ni Faraja na sio Fadhaa”

بسم الله الرحمن الرحيم

Utangulizi:
Wakati huu ambapo shule zimefungwa ndani ya kipindi cha mapumziko ya mwisho wa mwaka kwa wanafunzi, pia ni kipindi hiki ndio muda wa harakati na pirikapirika kwa wazazi na walezi wa wanafunzi kujiandaa kwa muhula mpya wa masomo ya mwaka mpya ambao utaanza sio muda mrefu.
Kwa masikitiko makubwa  mfumo wa elimu wa kibepari unaoongozwa kwa misingi ya usekula,  badala ya kuleta utulivu, faraja na sakina ya nafsi kwa wanafunzi, wazazi, walezi na jamii nzima umekuwa chanzo cha fadhaa, khofu na kuchanganyikiwa kwa wadau wote, iwe wanafunzi, wazazi, wazee na jamii kwa jumla. Baadhi ya fadhaa   na kuchanganyikiwa kunakotokana na mfumo huu wa kielimu  ni kama  yafuatayo:
1. Kugeuzwa elimu kuwa  biashara na uwepo mfumo mbaya wa kiuchumi kumepelekea :
• Kuchanganyikiwa jamii katika utafutaji wa malipo ya ada kwa ajili ya watoto wao.
• Kuchanganyikiwa   katika utafutaji wa gharama za vifaa, kama sare mpya, madaftari, vitabu nk.
2. Kushindwa shule za Umma / serikali kutoa elimu stahiki ya kiwango kumewafanya wazazi :
• Kuchanganyikiwa  kwa kuhangaika na kutapatapa ili kuwapatia watoto wao shule za kibinafsi ambazo ni bora kuliko shule za Umma.
3. Kwa Waislamu kutojua au kwa wenye mashule hususan yaliyobeba lakabu za Kiislamu kwa kuwaoneshwa wazazi, walezi , wanafunzi na  jamii kwa jumla  kimakosa  juu hukmu ya kisharia ya elimu za kisekula kwamba  ni jambo la faradhi kumepelekea:
• Kuchanganyikiwa kwa wazazi, walezi na wanafunzi kwa kuekeza juhudi kubwa kwa ufahamu kwamba elimu hizo ni faradhi, hivyo wao wamo katika ibada tukufu ya faradhi.
4. Kunasibishwa elimu na ufanisi wa kimaisha, upeo wa kiuchumi na kuongezeka rizki  kumepelekea haya:
• Wazazi kuwekeza jitihada kubwa kiasi cha kuchanganyikiwa na kutumia rasilmali nyingi kuwasomesha watoto, na pale watoto hao  wanapopata matokeo kinyume na  matarajio yao, hilo huwapa hali ya kuchanganyikiwa kupita mipaka kwa  wanafunzi, wazazi na walezi kwa kudhani kwamba wameshakosa fursa ya ukombozi wao wa rizki
• Aidha, dhana ya elimu na rizki huzua tafrani kiasi kikubwa kwa  kuharibu muamala mwema na mahusiano mahala pa kazi baina ya mwajiri na mwajiriwa (industrial relations)   kwa kuwa mwajiri hutaraji uaminifu katika kazi yake ilhali  mwajiriwa  ana dhana kwamba  ajira ndio chanzo cha rizki yake, iwe kwa kusaidia ndugu, kujenga, kuowa na kuhudumia familia, hata kama anacholipwa ni kiasi kidogo,  mwajiriwa hulazimisha  kuweza kupata hata kwa njia zisozo halali, ilimradi apate kazini hapo. Kwa kuwa huona kazi hiyo ni matunda ya elimu yake.
5. Maadaili sio kipimo cha kumpa kazi mwalimu
• Hili huvuruga jamii  kwa kuambukiza  wanafunzi maadili mabaya, na wazazi kukosa utulivu kwa kipindi chote watoto wao wanapokuwa shule, hususan watoto wa kike.
6. Kipimo cha ufaulu kilipofungwa katika shahada tu/ kipande cha karatasi
• Hili limezuwa tafrani katika kuongeza rushwa katika taasisi za elimu, udanganyifu katika mitihani na kuondosha ghera ya kujituma kwa baadhi , kwa kuwa mwanafunzi akiweza kuwa na uwezo wa kuinuna ile karatasi anafanya hivyo, bila ya kujituma. Hilo pia lina athari katika matumizi ya elimu husika baada ya ajira , mwajiriwa huwa ana maarifa machache kwa kuwa alipata cheti kwa udanganyifu badala ya kuisoma fani  husika kwa kina.
7. Kuchanganyikiwa kwa mzigo wa nadharia.
• Wanafunzi hubebeshwa mzigo mkubwa wa kukariri nadharia ambazo hazina umuhimu hususan za kihadhara, badala ya kumpa elimu ya madania ambayo inashikamana moja kwa moja na utatuzi wa matatizo katika mazingira yoyote, na kwa imani yoyote aliyonayo. Hivyo wanafunzi huchanganyikiwa kwa kukariri mzigo mkubwa wa nadharia  ambazo  hazikuwa na umuhimu wowote.
Hayo ni baadhi ya madhaifu yanayozua fadhaa na hali ya kuchanganyikiwa inayotokomana na mfumo mbovu wa kielimu wa kibepari.
Badala ya elimu kuwa  faraja, kuwaleta watu karibu, kuwaleta watu na uchamungu na kuthaminiana  imeleta natija kinyume  na hayo.

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!