Ardhi Iliyoporwa

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Tunajua kwamba kupora katika hali zote ni haramu. Jee! Serikali itakaponyang’anya ardhi ya watu na kuiuza au ikajenga nyumba na kuziuza itajuzu kununua ardhi hiyo? Jee! atakaponunua mtu mwengine ardhi hiyo kutoka Serikalini na kuiuza au kama atalinunua jengo hilo na kuliuza itasihi kununua ardhi hiyo au jengo hilo kutoka kwa mtu huyo?.

Jawabu:

Hapana shaka aina zote za uporaji ni haramu. Na mwenye kupora ardhi, huyo ametenda jambo kubwa la haramu na amefanya dhambi nzito. Kwa kauli ya Mtume (SAW) ‘Atakaedhulumu kiasi cha shubiri moja ya ardhi, atazongeshwa katika ardhi saba siku ya Kiama’. Hadithi hii imepokewa na Muslim kutokana na Hadithi ya bibi ‘Aysha (RA).

Hii inamaanisha kwamba, mwenye kupora sehemu ya ardhi iwe kubwa au ndogo huyo amefanya madhambi makubwa ambayo yatamfanya aadhibiwe siku ya Qiyama na katika dunia atastahiki adhabu ya taazir na atalazimika kukirejesha alichokipora katika hali ile ile alivyokichukua. Kwa kauli ya Mtume (SAW) ‘Kama kilivyo alivyokichukua mpaka akirejeshe kiko vilevile’. (Tirmidh).

Kitakapoharibika kile kilichoporwa katika mikono ya mporaji au kikabadilika hali yake, kama kitambaa kilichoporwa kikiwa kimeshonwa au madini yaliyoporwa yakiwa yameyeyushwa au mnyama aliyeporwa ikiwa ameshachinjwa. Hapo hutolewa thamani ya kilichoporwa na yule mnyang’anyi.

2).Atakapojenga jengo mporaji katika ardhi aliyoipora huwa hana haki ya kumiliki mali hiyo bali alienyang’anywa ana haki ya kumtaka mnyang’anyaji huyo abomoe jengo hilo kwa gharama zake na kama yatatokea madhara katika ardhi wakati wa kufanya hayo atalazimika kulipa fidia. Mtume (SAAW) amesema, ‘Jasho la dhalimu halina haki’.

Na kile alichokifanya mnyan’ganyi huyo katika ardhi hiyo iwe ni kilimo au jengo huwa si milki yake. Si ardhi wala jengo. Na haikubaliki kununua kutoka kwa mporaji ardhi iliyoporwa wala jengo alilojenga katika ardhi hiyo.

3).Wale walionunua ardhi kutoka kwa mporaji kwa vyovyote watakavyokuwa katika mdorongo (mfuatano) yaani huyu kanunua kwa mporaji na huyu kanunua kwa alienunua kwa mporaji na kuendelea, wote madhali wanajua kuwa ardhi hiyo imeporwa wote watakuwa makosani na haikubaliki Kisheria kununua ardhi hiyo. Na ardhi inabaki kuwa ni mali ya yule alienyang’anywa.

4). Itakapobadilika hali ya ardhi iliyoporwa kama kwa kujenga juu yake, zipo khitlafu juu ya Wanazuoni katika hukumu ya majengo. Kwa upande wa thamani ya majengo ikiwa ni kubwa au ndogo kwa mujibu wa ardhi yenyewe na kwa upande wa mjengaji, jee! ni yule yule mporaji au mnunuzi wa ardhi iliyoporwa ndie aliejenga?.

Na rai ninayoiona mimi na ndio ninayoichukua. 1- Ni haramu kununua jengo kutoka kwa mporaji au kutoka kwa yule aliyeipata kutoka kwa mporaji, kwa njia ya kugaiwa au kupewa zawadi au kutunukiwa au amechukua kama sehemu yake katika utawala.

Mfano, Dola limepora ardhi ya watu fulani na ikazigawa kwa watu wenye sehemu katika utawala, hukumu yao ni kama dola lililopora yaani hukumu yao ni moja kwa moja ya waporaji, na hao haijuzu kununua kutoka kwao.

2- Atakaponunua mtu mwengine akiuziwa na dola kwa bei ya soko la kawaida na akajenga juu yake jengo ambalo thamani yake imepita thamani ya ardhi, hakika jengo hili itakubalika Kisheria kwa mtu wa tatu kununua jengo hilo kutoka kwa mtu wa pili. Na jengo hili milki yake huwa ‘imehifadhiwa’ na kwa sababu haki ya mmiliki wa asili alieporwa imeanguka katika ardhi husika na inakuwa katika yale inayostahiki kulipwa thamani ya mali. Kama ambavyo mali iliyoporwa imegeuka kuwa katika hali nyengine, inakuwa dhamana yake ni thamani yake wala si kitu chenyewe. Na kwa vile mporaji ni Serikali huwa ni dhamana wa kulipa thamani ya ardhi yote na kulipa fidia ya madhara yote yatakayotokea wakati ardhi hiyo imo kwenye mamlaka ya mporaji. Thamani ya ardhi iliyoporwa huwa katika dhamana ya Serikali na kwa hivyo inakubalika Kisheria kwa mtu wa pili kununua jengo lililo katika ardhi iliyoporwa kwa sharti zifuatazo;

(a)- Iwe Serikali ndio mporaji wa ardhi hiyo, yaani iwe ni katika dhulma iliyofanywa na Serikali na kwa ajili hiyo huwa ndio iliyopora thamani ya ardhi na kwa hiyo mnunuaji kutoka upande wa pili halazimiki kulipa kima cha mali hiyo.

Ama ikiwa mporaji wa mwanzo ni mtu sio Serikali hubaki dhima ya kulipa thamani ni ju ya mnunuzi wa mwanzo na wa pili na kuendelea.

(b)- Iwe mtu wa pili amenunua ardhi hiyo kutoka Serikalini kwa bei ya soko la kawaida.

(c )- Iwe jengo hilo linalonunuliwa lina thamani kubwa zaidi kuliko thamani ya ardhi hiyo. Na kwa hayo, jawabu la swali linakuwa ni kama ifuatavyo-:

Haisihi kununua kutoka kwenye dola lililopora, lakini inasihi kununua kutoka kwa yule ambae amenunua kutoka Serikalini kwa sharti mbili-:

(1)- Ikiwa amenunua ardhi hiyo kutoka Serikalini kwa bei ya soko la kawaida, sawasawa iwe ni jumuiya au mtu binafsi. Yaani hakuipata ardhi hiyo kama ni tunza, zawadi ama kupewa tu bila ya kutoa thamani yoyote bali ni kwa hukumu ya nafsi yake katika utawala au mfano wake.

(2)- Iwe jengo lililojengwa juu ya ardhi hiyo lina thamani kubwa zaidi kuliko thamani ya ardhi hiyo. Na kuongezwa sharti ya tatu ikiwa alienunua kutoka Serikalini ni Jumuiya. Katika hali kama hii mpaka isihi kununua kutoka kwenye Jumuiya, inapasa iwe Jumuiya hiyo imesimama Kisheria, kwa mfano isiwe ni Shirika la ubia.

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!