Rajab Na Muhanga Wa Wanawake Kwa Dini Yao

Matukio makubwa ya kitareekh ndani ya mwezi huu wa Rajab licha ya kutupa mawaidha mengi katika dini yetu, pia yanatukumbusha katika historia ni kwa kiasi gani akinamama, dada na mabinti wa Kiislamu walivyojitolea muhanga mkubwa kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu. Walijitolea kwa muhanga wa mali, nguvu na hadi kufikia kutoa uhai wao kwa ajili ya Mola wao.

Kwa kuanzia, tukitupia macho kisa cha Miiraj, safari ya miujiza ya Mtume SAAW iliyofanyika mwezi wa Rajab mwaka mmoja kabla ya kuundwa dola ya mwanzo ya Kiislamu mjini Madina, tunaona miongoni mwa mambo aliyokutana nayo Mtume SAAW katika safari hiyo ni kaburi lililokuwa likitoa harufu nzuri ya ajabu ! Alipouliza Mtume SAAW kuhusu kaburi hilo, alielezwa na Jibril As. kwamba lilikuwa ni kaburi la mwanamke msusi katika zama za Firaun aliyeshikilia imani ya tawheed kwa uthabiti na kudhihirisha msimamo wake wa haki mbele ya Fir-aun. Fir-aun akaamuwa kuwauwa watoto wa msusi huyu ili kumlazimisha asalimu amri ya kurudi katika ukafiri. Lakini msusi huyu alisimama kidete bila ya kutetereka hadi Fir-aun akamuuwa, na mama huyu kufa kifo cha shahid. Muhanga huu wa aina yake ni kwa ajili ya kumpwekesha Mola, Muumba wa ulimwengu.

Aidha, ni katika mwezi huu wa Rajab, ndani ya mwaka wa tano wa Utume ndio mwezi uliofanyika tukio la hijra ya Uhabeshi. Ilikuwa ni kuhama kwa ajili ya kukimbia mateso na vitimbi vya maqureish. Kati ya Waislamu kumi na mbili waliokuwemo katika safari hii, wanne walikuwa wanawake. Waislamu hao walisafiri masafa marefu baharini kwa ajili ya Uislamu wao. Wanawake waliokuwemo katika msafara huu ni Ruqayyah bint Muhammad (binti wa Mtume SAAW, na mke wa Uthman bin Affan, Sahla bint Suhail, Umm Salama na Layla Bint Abi Asmah. Safari hii ya mwanzo ilisahilisha kutokea safari ya pili ya Waislamu kuja Uhabeshi ambayo ilijumuisha Waislamu wengi zaidi chini ya Jaafar bin Abu Talib RA.

Kwa upande mwengine tusisahau pia ni katika mwezi wa Rajab mwaka wa tisa hijria ndipo vilipotokea vita vikubwa na vikali vya jihad. Vita vya Tabuk. Vita vilivyokuwa mtihani mkubwa kwa Waislamu. Kwa kuwa vilitokea kipindi cha kiangazi, kwenda eneo la mbali, kukabiliana na jeshi kubwa la waroma na isitoshe maandalizi yake hayakuwa na vifaa vya kutosha. Vita ambavyo Mwenyezi Mungu mwenyewe kavipa jina ndani ya Quran kwamba ni ‘saa nzito’ (saat u l-usra). Waislamu walitakiwa wachangie kadiri wawezavyo katika maandalizi ya jeshi. Ni katika hali kama hiyo ndipo akinamama na mabanati wa Kiislamu walipochangia vito, mikufu, bangili, herini, mapambo yao na vitu mbalimbali vya thamani ili kusaidia katika upatikanaji wa vifaa vya vita. Imepokewa kutoka Umm Sinan, mwanamke wa kabila la Aslam kwamba aliona pande la kitambaa mbele ya Mtume SAAW katika nyumba ya Aisha ra. ambacho ndani yake kilisheheni vito na vitu mbalimbali walivyochangia wanawake wa Kiislamu ili kusaidia kukabiliana na gharama za maandalizi ya jeshi la Tabuk (Waqidi, Maghazi, Vol. 3, p. 991-992)

Leo muhanga wa wanawake katika dini yao unahitajika kuliko wakati wowote. Kwa sababu tunapita katika kipindi ambacho Waislamu hatuna kinga ya kulinda maisha yetu, heshima yetu, mali zetu na dini yetu, yaani dola ya Kiislamu ya Khilafah. Basi ni wajibu mama zetu, dada zetu na mabanati zetu warejee katika msimamo wa kitareekh wa kujitolea muhanga kwa ajili ya Mola wao.

Masoud Msellem
28 Machi 2019
#RajabFarajaKwaWalimwengu

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!