Hukmu ya Swala Katika Msikiti Ambao Wameshiriki Makafiri Kuujenga

Swali:

Assalanu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh..

Niruhusu nijitambulishe binafsi, jina langu ni Nadya ni mmoja katika madarisaat nchini Indonesia. Ewe Sheikh nataka kuuliza; nini hukmu ya swala katika msikiti ambao wameujenga makafiri?

Allah Akulipe kheri Sheikh

Jawabu:

Waalaykum Salam Warahmatullah Wabarakatuh

Nyuma huko tulishaulizwa mfano wa swali hili na jawabu letu kwa muulizaji wakati huo tarehe 23/4/2018 lilikuwa kama hivi lilivyobainishwa hapa chini. Nakuekea kwa ajili yako swali hilo kiukamilifu na jawabu letu na lina maelezo ya kutosha Inshallah:

(Swali: Je inajuzu kuukubali msaada wa makafiri kwa ajli ya kujenga msikiti? Na je inajuzu swala katika msikiti waliosjiriki makafiri katika kutoa msaada katika ujenzi wake?

Jawabu: Swali hili lina pande mbili:

Upande wa kwanza: Je inajuzu kuukubali msaada wa kifedha wa kafiri kwa ajili ya msikiti?

Upande wa pili: Je inajuzu swala katika msikiti ambao zimetumiwa kwa ajili yake fedha kutoka makafiri?

Ama upande wa mwanzo, nao ni kukubali mchango kutoka kwa makafiri kwa ajili ya msikiti, suala hili lina rai kadhaa… Wako wanavyuoni wanaojuzisha hilo, kwa kutumia qiyasi cha kukubali zawadi kutoka kwa kafiri, na kwamba Mtume (SAW) alikubali zawadi kutoka kwa Mukaukis ambae ni mtawala wa Misri wa Kiroma… Na ninachokiona mimi kwamba zawadi kwa ajili ya mtu hutofautiana na mchango kwa ajili ya msikiti, wakia inatofautiana:

1.Hakika ya msikiti ni sehemu ya ibada kwa ajili ya Allah (SWT), kwa hivyo mchango kwa ajili ya msikiti hukubalika (hufahamika) kuwa ni kwa ajili ya Allah (SWT). Na katika hadithi kutoka kwa Abu Huraira amesema: Kasema Mtume (SAW):

«أيُّها النّاسُ، إِنّ الله طيِّبٌ لا يقْبلُ إِلّا طيِّبًا…» (مسلم).

“Enyi watu hakika Allah ni mzuri hakubali isipokuwa kizuri…” (Muslim).

Kwa hiyo haijuzu kukubali mchango kutoka kwa kafiri kwa ajili ya msikiti kwa sababu mali ya kafiri si nzuri.

  1. Na vilevile hakika Mtume (SAW) ameeleza katika hadithi zake tukufu kuwa mwenye kujenga msikiti hakika Allah humjengea yeye nyumba peponi:

-Ametoa Ahmad katika Musnad wake kutoka kwa Sa’ad bin Jubair, kutoka kwa Ibn Abas, kutoka kwa Mtume (SAW) kuwa amesema:

«مَنْ بَنَى لِلَّهِ مَسْجِدًا وَلَوْ كَمَفْحَصِ قَطَاةٍ لِبَيْضِهَا، بَنَى اللَّهُ لَهُ بَيْتًا فِي الْجَنَّةِ».

“Mwenye kujenga msikiti kwa ajili Allah ijapokuwa kama sehemu anayofukua fukua ndege kwa ajili ya yai lake (yaani msikiti mdogo sana), Allah humjengea msikiti Peponi”

-Ametoa Tirmidhy katika Sunan yake kutoka kwa Uthman bin Affan, amesema: Nimemsikia Mtume (SAW) anasema:

«مَنْ بَنَى لِلَّهِ مَسْجِدًا بَنَى اللَّهُ لَهُ مِثْلَهُ فِي الجَنَّةِ»،

“Mwenye kujenga msikiti kwa ajili ya Allah, atamjengea Allah mfano wake katika Pepo”. Tirmidhy akasema: Hadithi ya Uthman ni Hadith Hasan na Swahih. Na vile vile ameitoa Ibn Khuzaima katika Swahih yake kutoka kwa Uthman ibn Affan na ametoa Al-Daramy mfano wake.

-Na ametoa Ibn Hiban katika Swahih yake  kutoka kwa Abu Dhar amesema: Kasema Mtume (SAW):

: «مَنْ بَنَى لِلَّهِ مَسْجِدًا وَلَوْ كَمَفْحَصِ قَطَاةٍ بَنَى اللَّهُ لَهُ بَيْتًا فِي الجنة»

“Mweye kujenga msikiti kwa ajili ya Allah ijapokuwa ukubwa wake kama sehemu anayofukua fukua ndege, Allah atamjengea nyumba Peponi”. Sanad yake ni sahihi.

Na kwa sababu Hadithi inaonyesha kuwa mwenye kujenga msikiti kwa ajili ya Allah na Allah atamjengea yeye nyumba Peponi, na haliwi hili isipokuwa ni kwa ajili ya Muislamu, kwa hiyo kilichokusudiwa katika maneno (Mwenye kujenga nyumba kwa ajili ya Allah) ni Muislamu huyo, kwa sababu kafiri lau atajenga nyumba hawi katika watu wa Peponi.

3.Na vilevile hakika washirikina katika zama za ujinga (Jahiliyyah) walijifakharisha kwamba wao ni katika wanao amirisha Msikiti Mtukufu. Allah akateremsha Aya Tukufu:

﴿أَجَعَلْتُمْ سِقَايَةَ الْحَاجِّ وَعِمَارَةَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ كَمَنْ آمَنَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَجَاهَدَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ لَا يَسْتَوُونَ عِنْدَ اللَّهِ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِين﴾

(Hivyo mumefanya kuwanywesha maji mahujaji na kuamirisha Msikiti Mtuku ni kama mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho na akapigana jihadi katika njia ya Allah, hawalingani hawa mbele ya Allah, na Allah hawaongoi watu madhalimu). Imeelezwa katika tafsiri ya Qurtubi:

(Kauli yake Taala:

﴿أَجَعَلْتُمْ سِقايَةَ الْحاجِّ…﴾

 “Hivyo mumefanya kuwanywesha maji mahujaji…” Kinachokusudiwa katika lugha ya Kiarabu: Hivyo mumefanya wanaowanywesha maji mahujaji au wenye jukumu la kuwanywesha maji mahujaji ni kama mwenye kumuamini Allah na akapigana jihadi katika njia yake. Na inafaa kukadiriwa kuondolewa (al-hadhf ) katika maneno (Mwenye kuamini), yaani “Hivyo mumefanya amali ya kuwanywesha maji mahujaji ni kama amali ya mwenye kuamini).

Na imeelezwa katika tafsiri ya Al-Nasfy: (Hivyo mumefanya kuwanywesha maji mahujaji na kuamirisha Msikiti Mtukufu ni kama mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho na akapigana jihadi katika njia ya Allah, hawalingani hawa mbele ya Allah, na Allah hawaongoi watu madhalimu) kunywesha maji (assiqaayah) na kuamirisha (al-imarah) ni machimbuko yanayotokana na saqaa na amara ni kama kukinga (aswiyaanah) na ngao (wiqaayah) na hapana budi yenye kutegemea (mudhwaaf) iliyoondolewa ambayo kukadiriwa kwake ni:

﴿أَجَعَلْتُمْ سِقَايَةَ الْحَاجِّ وَعِمَارَةَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ كَمَنْ آمَنَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَجَاهَدَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ لَا يَسْتَوُونَ عِنْدَ اللَّهِ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِين﴾

“Hivyo mumefanya wenye kuwanywesha maji mahujaji na wenye kuamirisha Msikiti Mtukufu ni kama mwenye kumuamini Allah..” Na maana yake ni kupinga washirikina kuwalinganisha na waumini na kulinganisha amali zao zenye kuporomoka kwa amali zao zenye kuthibiti, na kuwafanya sawa kati yao na kujaalia kuwafanya sawa ni dhulma kwa dhulma yao ya ukafiri, kwa sababu wao wameweka kusifiwa na fahari katika sehemu si zake…)

Na yote haya yanabainisha yule mwenye kukubaliwa kuamirisha Msikiti Mtukufu “na msikiti wowote ule” ni yule mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho, yaani ni Muislamu. Nalo humaanisha kwa ufahamu wake (mafhuumih) ni kutokubali mchango wa kafiri kwa ajili ya kujenga masikiti.

Kwa hivyo lile ninalolitia nguvu (urajjihuhu) ni kutokubali mchango wa makafiri kwa ajili ya kuamirisha misikiti. Na nasema lile ninalolitilia nguvu (urajjihuhu) kwa sababu baadhi ya wanavyuoni wanajuzisha mchango kutoka kwa kafiri kama nilivyotaja mwanzo wa jawabu.

Hili ndilo ninalolitilia nguvu. Na Allah ndie mjuzi zaidi na Mbora zaidi wa hekima) Mwisho.  Haya ni kuhusu upande wa kwanza…

Ama upande wa pili nao ni kujuzu swala katika hiyo misikiti. Hakika swala inajuzu. Ametoa Bukhari kutoka kwa Jabir bin Abdillah amesema: Kasema Mtume (SAW):

«أُعْطِيتُ خَمْسًا لَمْ يُعْطَهُنَّ أَحَدٌ مِنَ الأَنْبِيَاءِ قَبْلِي: نُصِرْتُ بِالرُّعْبِ مَسِيرَةَ شَهْرٍ، وَجُعِلَتْ لِي الأَرْضُ مَسْجِدًا وَطَهُورًا، وَأَيُّمَا رَجُلٍ مِنْ أُمَّتِي أَدْرَكَتْهُ الصَّلاَةُ فَلْيُصَلِّ، وَأُحِلَّتْ لِي الغَنَائِمُ، وَكَانَ النَّبِيُّ يُبْعَثُ إِلَى قَوْمِهِ خَاصَّةً، وَبُعِثْتُ إِلَى النَّاسِ كَافَّةً، وَأُعْطِيتُ الشَّفَاعَةَ»

 “Nimepewa mambo matano ambayo hakupewa Mtume yeyote kabla yangu: Nimenusuriwa dhidi ya hofu kwa mwendo mwezi mzima, na ardhi imefanywa msikiti na safi (yenye kuweza kusafisha) kwa ajili yangu na mtu yeyote katika umati wangu ikimdiriki swala basi na aswali, na nimehalalishiwa ngawira, na Mtume alikuwa anatumwa kwa watu wake maalumu mimi nimetumwa kwa watu wote, na nimepewa uombezi”. Na ameitowa Muslim kwa maneno: Kutoka kwa Jabir bin Abdillah Al-Answary amesema: Kasema Mtume (SAW):

«أُعْطِيتُ خَمْسًا لَمْ يُعْطَهُنَّ أَحَدٌ قَبْلِي، كَانَ كُلُّ نَبِيٍّ يُبْعَثُ إِلَى قَوْمِهِ خَاصَّةً، وَبُعِثْتُ إِلَى كُلِّ أَحْمَرَ وَأَسْوَدَ، وَأُحِلَّتْ لِيَ الْغَنَائِمُ، وَلَمْ تُحَلَّ لِأَحَدٍ قَبْلِي، وَجُعِلَتْ لِيَ الْأَرْضُ طَيِّبَةً طَهُورًا وَمَسْجِدًا، فَأَيُّمَا رَجُلٍ أَدْرَكَتْهُ الصَّلَاةُ صَلَّى حَيْثُ كَانَ، وَنُصِرْتُ بِالرُّعْبِ بَيْنَ يَدَيْ مَسِيرَةِ شَهْرٍ، وَأُعْطِيتُ الشَّفَاعَةَ».

“Nimepewa mambo matano ambayo hakupewa yeyote kabla yangu, alikuwa kila Mtume anatumwa kwa watu wake maalumu  mimi nimetumwa kwa kila mwekundu na mweusi, na nimehalalishiwa ngawira hajahalalishiwa yeyote kabla yangu, na ardhi imefanywa kwa ajili yangu kuwa nzuri, safi (yenye kuweza kusafisha) na msikiti, basi mtu yeyote ikimdiriki swala aswali namna alivyo, na nimenusuriwa dhidi ya hofu baina ya mwendo wa mwezi mzima, na nimepewa uombezi”

Kwa hivyo sehemu yoyote katika ardhi inajuzu kuswali hapo pindi pakiwa safi (twaahir)… kwahivyo swala itakuwa ni sahihi katika msikiti wowote hata kama umegharimiwa kifedha na makafiri. Kutokusihi kukubali fedha kutoka kwa kafiri kwa ajili ya kuamirisha msikiti hakumaanishi kutokubali kuswali humo msikitini. Hayo ni kutokana na tuliyoyabainisha hapo juu.

Haya ndiyo ninayoyatilia nguvu katika mas-ala haya. Allah ndie Mjuzi zaidi na Mbora zaidi wa hekima.

Ndugu yenu Atta bin Khalil Abu Rashta.

27, Muharram 1440H

07, October 2018

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!