‘Vunja Jungu’ Sio Yetu’

Mwishoni mwa mwezi wa Shaaban huwa kuna hekaheka za matendo yanayoitwa ‘vunja jungu’. Fikra ya ‘vunja jungu’ japo haina mashiko yoyote katika Uislamu lakini hunasibishwa na Uislamu, kwa kuwa inafungamanishwa na kumalizika kwa mwezi wa Sha’aban na kuingia mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambayo hii ni miezi ya Kiislamu.
Nyuma ya fikra ya ‘vunja jungu’ humaanisha kufanya haraka kutenda matendo katika dakika za mwisho hususan siku chache kabla ya kuingia Ramadhani, matendo ambayo ni vigumu kuweza kuyatenda kwa usahali ndani ya Ramadhani, (japo ukweli huwa yamekatazwa wakati wote). Matokeo ya fikra ya ‘vunja jungu’ ni watu wakiwemo baadhi ya Waislamu kimakosa kujitosa katika maovu na maasi mbalimbali kinyume na Uislamu, wengine kwa bahati mbaya huhisi ni sehemu ya Uislamu.

Dhana ya ‘vunja jungu’ husukumwa na fikra tatu kubwa:
Kwanza, fikra ya ilmania/kisekula, fikra dhaifu, batil na ya kijuha isiyoingia akilini kwa hoja za kidini wala za kiakili. Fikra hii ambayo ndio imani msingi/aqida ya mfumo wa kibepari unaotawala ulimwengu leo huhubiri uwepo wa Muumba kuwa umefungwa katika baadhi ya maeneo, yaani katika majengo ya Ibada, siku na nyakati maalum. Matokeo ya fikra hii ni watu kuona kuna baadhi ya maeneo au wakati fulani ambapo Muumba huwa yupo na waja wake, na kuna baadhi ya wakati na maeneo fulani Muumba huwa hayupo.

Hivyo, fikra ya vunja jungu huona kuwa Shaaban sio mwezi wa Mungu, bali Ramadhani ndio mwezi wa Mungu na uchaMungu wa kujinyenyekeza kwa Muumba. Hii ni fikra ya hatari sana, na kamwe haipo katika Uislamu, bali kimsingi haingii akilini kwa mwanadamamu yoyote kusema kuwa Muumba wa ulimwengu, wanadamu na viumbe vyote awekewe mipaka? Huyo atakuwa Mungu wa aina gani anaewekewa mipaka na kiumbe alichokiumba.

Kwa udhaifu wa fikra hii ambayo ndio fikra kiongozi (chimbuko la mambo yote) ya mfumo wa kibepari/demokrasia, yatosha kuporomosha mfumo wote wa kibepari kwa kukosa uwezo na sifa ya kumsimamia mwanadamu ipasavyo. Kwakuwa kinachojengwa juu ya msingi dhaifu, nacho huwa dhaifu.

Jambo la pili, ni matumizi ya fikra ya ‘uhuru wa Kibinafsi’ (personal freedom) ambayo ni miongoni mwa nguzo za mfumo wa kidemokrasia na ambayo hulingania kuwa mtu atende atakalo katika kujifaragua katika maisha yake binafsi. Fikra hii humuonesha mwanadamu kana kwamba yeye ndio muamuzi wa matendo yake, kwa lipi kutenda na lipi kuacha kutenda katika maisha yake kibinafsi. Kwa fikra hii ndio watu huzini, kulewa, kuwa mashoga, wanaume kujishabihisha na wanawake nk. wakidhani kuwa wanatumia uhuru wao kibinafsi. ilhali watu hao hao wanapokua kazini hunyenyekea, huheshimu na kushikamana na sheria za kazi kama zilivyo, lakini wanachojisahaulisha ni kwamba katika dunia hii wao ni viumbe tu , miongoni mwa viumbe dhaifu ambavyo hustahiki kufuata na kunyenyekea maagizo yote ya Muumba. Maagizo ambayo kamwe hayamtii dhiki mwanadamu kwa kuwa yanawafikiana na maumbile yake katika kushibisha mahitajio yake yote msingi.

Tatu, ni fikra ya hatari ambayo lau hatuwapi udhuru wa ujinga kwa Waislamu wanaotenda mambo ya ‘vunja jungu’, basi sharia ya Kiislamu ingewatoa katika mila / Uislamu. Kwa kuwa ‘vunja jungu’ humaanisha kwamba Ramadhani ni jambo zito, dhiki, usumbufu na lenye kunyima raha na utamu wa maisha, kiasi kwamba wao huona ‘wakomoe’ kwa mara ya mwisho ndani ya hatima ya mwezi wa Shaaban. Ilhali katika sharia ya Kiislamu hakuna zito lililoletwa kumkwaza mwanadamu. Kwa kuwa mfumo wa Uislamu ni Rehma kwa mwanadamu. Itakuwaje Rehma kisha ilete dhiki?

Hizo zote ni fikra chafu, hatari na hazina nafasi katika Uislamu wala katika hali halisi. Uislamu umetuwekea wazi kwamba Muumba hana mipaka, yupo wakati na mahala popote. Aidha, sisi wanadamu ni watumwa, na Muumba wetu ndio bwana, na fungamano la mtumwa na bwana ni amri na kunyenyekea tu.

Aidha, Uislamu ni dini inayowafikiana na maumbile ya mwanadamu, kamwe haikuja kumtia mwanadamu uzito wala dhiki katika kushibisha mahitaji yake, yawe ya kibaologia kama chakula, maji nk. au ya kighariza kama ya kiibada, kuendeleza kizazi nk. Bali Uislamu umekuja kupanga utaratibu mwanana na mzuri kwa wanaadamu ili wakidhi mahitajio yao yote bila ya pingamizi wala dhiki.
Tuingieni mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa moyo mkunjufu na kutaraji malipo/ (iimaan wa ihtisaban). Na tuiage Shaaban kwa furaha na kuendelea kujifunga na Uislamu. Tukiivuruga Shaaban ndio kuivuruga Ramadhani.
ْ
وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ
“Na wala (Mwenyezi Mungu) hakuweka juu yenu uzito katika dini”
(TMQ 22:78)

Risala ya Wiki No. 38
18 Sha’aban 1440 Hijri / 24 Aprili 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
http://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!