Tumeingia Ramadhani Hali Yetu Bado Ile Ile

Tunamshukuru Allah Rahima na Rehma zende kwa tumwa Karima, na aali zake Kirama na swahaba zake Adhima.
Ama baada ya hayo,

Umma wa Kiislamu tumeingia mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mara nyengine tukiwa hatuna msemaji wala mtetezi anayeweza kutufanya kuwa wa moja na kufahamiana katika ikhtilafu zetu hata ndogo ndogo.

Tumeingia mwezi wa Ramadhani na Ummah wa Kiislamu tukitofautiana katika ibada tukufu ya funga. Baya zaidi si kwa sababu za ikhtilafu za kifiqihi ambazo kimsingi Uislamu unazikubali, bali kwa michoro ya mistari (mipaka) iliyochorwa na makafiri wakoloni ambao hadi leo ndio wanaoendeleza tofauti hizi na kuzidhamini.

Tumeingia katika mwezi wa Ramadhani na wengi katika Umma wa Kiislamu wanafunga na hawajui nini watafutari ikifika magharib. Lakini kwa shauku yao ya dini na taqwa yao hufunga hivyo hivyo inshallah, ilhali watawala katika miji ya Waislamu na baadhi ya Waislamu walioruzukiwa riziki kunjufu wakivuruga na kumwaga vyakula. Yote haya ni kwa sababu hatuna Khilafah itakayosimamia mafukara na masikini katika Ummah wa Kiislamu.

Tumeingia mwezi wa Ramadhani ilhali Waislamu wa Palestina, Yemen, Somalia, Turkistan Mashariki wakiendelea kukabiliwa na mateso na maangamizi. Upande wa maangamizi ya Syria wamekusanyika Assad kwa msaada wa Marekani, Urusi, China, Saudia, Iran, Uturuki nk. Kwa sababu tu wamekataa demokrasia na kutaka mfumo wa haki wa Kiislamu. Bila ya kutaja maelfu ya Waislamu dunia nzima ikiwemo hapa Tanzania waliosekwa magerezani kwa kisingizio cha ugaidi, wakiendelea kushikiliwa bila ya kesi zao kusikilizwa wala kuachiwa huru.

Tumeingia mwezi wa Ramadhani bado Quran haijafanya kazi kivitendo kuwaongoza watu duniani kama Allah Taala alivyoisifia kuwa ni Muongozo kwa watu wote, na sio kwa Waislamu peke yao. Na ili Quran iwe Muongozo kivitendo ni lazima iwepo dola ya Kiislamu ya Khilafah itakayotawalisha Quran kwa watu wote, huku kwa wasiokuwa Waislamu wataruhusiwa kuendelea na mambo yao ya kiibada, na hawatolazimishwa kuingia ndani ya Uislamu kwa nguvu. Bali watalinganiwa kwa khiyari lakini kutokana na uadilifu na neema ya Uislamu wengi wao wataingia katika dini kwa makundi na kwa khiyari.

Tumeingia mwezi wa Ramadhani, huku ibada hii ikitekwa nyara na baadhi ili kumakinisha fikra hatari za kisekula na dini mseto . Fikra ambazo ni za makafiri na hazina nafasi yoyote ndani ya Uislamu. Wanaoidandia ibada hii kwa maslahi ya wanasiasa wa kidemokrasia na kuleta ukuruba baina ya dini, wanajua fika kwamba ibada hii ni ya Waislamu na Uislamu na iko kando na wanayoinasibisha, lakini wanatenda hayo kwa dhihaka na dharau na kufuru tu ya uadui wao kwa Umma wetu na dini yao. Allah Taala Anasema:
وَلَنْ تَرْضَى عَنْكَ الْيَهُودُ وَلاَ النَّصَارَى حَتَّى تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ
“Hawatokuwa radhi juu yako Mayahudi wala Manasara mpaka ufuate mila yao..” (TMQ 2:120)

Tunamuomba Allah Taala Ajaalie Ramadhani ijayo tuwe chini ya bendera moja, dola moja na kiongozi mmoja (Khalifah) atakaeutangazia Umma wa Kiislamu dunia nzima siku moja ya kufunga na kufungua pasina kuzingatia michoro ya kijahili iliyochorwa na makafiri wakoloni inayoitwa mipaka.
Na kauli yetu ya mwisho tunasema Al-hamdulillahi Rabbil-aalaimina

07 Ramadhani 1440 Hijri / 12 Mei 2019
#RamadhanNaMuongozoWaQuran

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!