Ramadhani: Mwezi wa Quran na Kuondoa Vizuizi Vya Kuenea Kwake

Ramadhani ndio mwezi ambao kitabu kitukufu Quran Kareem kiliteremshwa ili kuwa ni muongozo kwa wanadamu wote. Amesema Allah Taala:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِنْ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ
“Mwezi wa Ramadhani ndio mwezi ambao imeteremshwa Quran ili kuwa muongozo kwa wanadamu na ni upambanuzi baina ya haki na batil (TMQ 2:185)

Ili kuhakikisha kitabu hiki kinafanya kazi inayotakikana ya kuwaongoza wanadamu Waislamu waliotangulia waliutendea haki mwezi huu kwa kuufanya kuwa ni mwezi wa mapambano ya kuondoa vizuizi vya kuwafikia watu muongozo wa Quran. Ili uadilifu wa Uislamu ambao unatakiwa kusimamia watu wote uweze kufika mashariki na magharibi.

Aidha, lengo hili la kuteremshwa Quran kuwa muongozo ndilo lililomsukuma Mtume wetu SAAW kuongoza mapambano makali ndani ya mwezi wa Ramadhani katika vita vya kwanza (Vita vya Badr) vilivyotokea tarehe 18 Ramadhani 2 Hijiria ili kuondoa vizuizi vya kuwafikia watu nuru ya muongozo huo. Baada ya ushindi huo Waislamu hawakusita kupambana kuondoa vizingiti ili kuipa nafasi Quran imuongoze mwanadamu bila ya kizuizi. Tareekh ya Kiislamu imesheheni simulizi kuhusu mapambano aina hiyo.

Moja miongoni mwa mapambano hayo ni ufunguzi/fathi ya Andalusia (Spain na Ureno) chini ya Jemedari Tariq bin Ziyad aliyeongoza mapambano makali ndani ya mwezi wa Ramadhani mwaka 92 Hijiria/ 711 miladiyya. Mapambano hayo yalijiri ndani ya Ramadhani na kukamilika ndani ya mwezi wa Shawwal.

Twariq bin Ziyad alikuwa msaidizi wa Musa bin Naswir ambaye alikuwa ni Gavana wa eneo la Maghrib / Morocco. Jemedari huyo wa Kiislamu katika ufunguzi huo wa Andalusia alianzia na wanajeshi takribani 7000, kisha akaomba kuongezewa askari, na Gavana Musa bin Naswir akatuma idadi ya askari 5000 kwa merikabu wakiongozwa na Twarif bin Malik, hivyo idadi ya askari wa Kiislamu ikawa 12000. Kwa upande wa makafiri wa Andalusia wao walikuja kwenye vita wakiwa na askari takriban laki moja, wengi wao wakiwa wamepanda vipando na silaha bora zaidi, wakiongozwa na Jemadari wao aliyejulikana kama Luthriiq aliyekuja katika medani ya vita akijifakhiri kwa kuvaa mavazi ya nguo zilizopambiwa maadini ya dhahabu na kipando chake kikikokotwa na nyumbu wawili.

Vita vilianza kupiganwa katika bonde la Burbat, eneo muhimu kistratejia ya kivita, nyuma yake kulikua na mlima mkubwa na upande mwingine ni sehemu ya bahari, ambapo kulikuwa na meli ambayo ndani yake kulikuwa na kikosi chini ya Jemadari Twaarif bin Malik.

Mapambano hayo yalidumu takriban siku nane, huku kukiwa na maiti na majeruhi wengi upande wa Waislamu, inakadiriwa takriban wanajeshi elfu tatu wa Kiislamu walipoteza maisha. Aidha, upande wa maadui kulishuhudiwa maelfu ya wanajeshi kuuwawa na kupatikana majeraha wengi .

Mwisho wa mapambano hayo Mola SW alijaalia nusra na ushindi upande wa Waislamu mwanzoni mwa mwezi wa Shawwal. Ama kiongozi wa Andalusia inasemekana aliuwawa, wengine wanasema alikimbia upande wa kaskazini mwa Andalusia, na utajo wake haukuwepo tena baada ya vita hivi. Katika vita hivyo licha ya wapiganaji walikuwa na swaumu ya Ramadhani walipigana kwa uhodari mkubwa kwa msukumo wa uchamungu waliokuwa nao (Al-Bidayh Wanihayah, juzuu ya tisa uk. 138)

Ushindi huu wa Waislamu ndani ya Andalusia ukaleta nuru ya muongozo wa Quran nchini humo na kubadili maisha ya watu kwa kuwainua kifikra na kielimu, jambo lililoacha athari yake mpaka leo. Aidha, ufunguzi huu ukawa ukurasa mpya wa maendeleo makubwa ya kielimu na kiteknolojia. Vyuo vikuu vikubwa barani Ulaya vikajengwa katika miji ya Cordoba na Valencia vilivyokuwa chachu kubwa ya maendeleo.

Huo ndio utukufu wa Ramadhani, mwezi uliowasukuma Waislamu kuondoa kila aina ya kizuizi cha kufikisha nuru ya muongozo wa Quran na kutetea matukufu yao na kuufikisha ujumbe wa Uislamu mashariki na magharibi.

Hali hiyo kamwe haitajirudia mpaka pale yatakaporejea tena maisha ya Kiislamu chini ya utawala wa Khilafah Rashidah, ambapo dola hiyo itakomboa maeneo yote na kuufanya mwezi wa Ramadhani sio wa kula vinono tu, ilhali damu za Waislamu zikimwagwa, na matukufu ya Kiislamu yakidharauliwa.
Amesema Allah Taala :

وَكَذَلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطًا لِتَكُونُوا شُهَدَاءَ عَلَى النَّاسِ وَيَكُونَ الرَّسُولُ عَلَيْكُمْ شَهِيدًا

“Na hivyo ndio tumekufanyeni Umma bora (wasat) ili muwe mashahidi baina ya watu na Mtume awe shahidi juu yenu” (TMQ 2:143)

#RamadhanNaMuongozoWaQuran

Risala ya Wiki No. 40
12 Ramadhan 1440 Hijri /17 Mei 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

http://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!