Hatua za Kivitendo Zitakazo Chukuliwa na Khilafah Rashida ili Kuzuia Ukosefu wa Ajira

Ukosefu wa ajira ni mfano wa kadhia na matatizo mengineyo yaliyo sababishwa na mfumo huu wakilafi wa kiulimwengu wa kirasilimali, ikiwemo nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali inayotabikishwa ambayo huzalisha tu migogoro na majanga ya kiuchumi pekee, kwa kuwa iliunda nidhamu ya matabaka katika mujtama na kuongeza idadi ya wasiokuwa na ajira na kufilisi akiba za watu na kusambaratisha uchumi wa nchi nyingi duniani.

Ukosefu wa ajira ni nini na ni lipi suluhisho linalohitajika kuutatua?

Ukosefu wa ajira wamaanisha mtu kukosa uwezo wa kupata pato la kuendesha maisha ili kujipa kiwango stahiki cha maisha kwake. Maisha haya stahiki yanajumuisha mahitaji msingi ya chakula, nyumba na mavazi. Suluhisho la tatizo hili la ukosefu wa ajira lapaswa kuwa la kimsingi kuliko kuwa la kiviraka. Uhalisia wa maisha na maafa mabaya ya kiuchumi yamethibitisha kuwa hatua zilizo chukuliwa na madola ni za haraka, za muda na zenye mipaka. Muundo wa uchumi wa kirasilimali pamoja na benki zilizojengwa juu ya riba na kufungamanishwa na taasisi za kifedha, mikopo na ufichaji mali na noti za benki za lazima, ndiyo yanayojaza na kuongeza viwango vya ukosefu wa ajira licha ya madai ya kupungua kwake yakirudiwa rudiwa.

Suluhisho msingi la ukosefu wa ajira litakuwa kamilifu pekee katika nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu iliyojengwa juu ya misingi ifuatayo:

1- Utekelezwaji wa mfumo wa dhahabu na fedha badala ya mfumo wa noti za karatasi za lazima
2- Uharamishaji wa riba juu ya mikopo
3- Uharamishaji wa ufichaji mali

– Mfumo wa pesa za karatasi za lazima: Dola huendesha soko kwa kupitia kubuni migogoro iliyozaliwa na mfumo wa pesa za lazima, kama mfumko wa bei na nishati duni ya ununuzi na mporomoko wa kiuchumi na ufutaji wafanyikazi na waajiriwa ili kutatua kadhia hizi, kupitia moja ya suluhisho mbili:

* Kupitia uchapishaji pesa mpya endapo dola iko imara na pesa yake inatawala, basi itaijaza sokoni ili kuusukuma uchumi, na hili ndilo ambalo aliyekuwa Raisi wa Amerika Obama alilolifanya wakati wa mgogoro wa kiuchumi. Alichapisha mabilioni ya pesa za makaratasi ili kuongeza nishati ya ununuzi ya watu. Lakini wamiliki wa makampuni walishughulika na kugawanya bidhaa zao walizo zihifadhi na bidhaa zao ambazo hazijatumika wakati wa mporomoko wa kiuchumi, kabla ya uzalishaji wa bidhaa mpya, ambao wahitaji wafanyikazi wapya. Mpangilio huu sio suluhisho la tatizo la ukosefu wa ajira, bali ni suluhisho la uondoshaji bidhaa ambazo hazijatumika kabla ya oparesheni ya gurudumu la uzalishaji.

* Au dola iombe pesa kupitia uuzaji wa bondi na kuchukua mikopo kutoka kwa IMF na Benki ya Dunia. Hii ndiyo hali ya biladi nyingi za Kiislamu ambazo huanza kutoa ahadi baada ya ahadi ya utafiti ili kuzalisha uwekezaji mwingi ili kuuendesha uchumi na kufungua fursa mpya za kazi kwa mujibu wa madai yao. Lakini, “dawa hizi za kuondoa maumivu” hazitoki nje ya muundo wa kuongeza hazina za benki za riba na kampuni za hisa pasi na mbinu hii ya kuongeza mfumko wa bei sokoni kupewa umuhimu wowote.

Suluhisho linalopeanwa kupitia mfumo wa dhahabu na fedha katika tukio la mporomoko wa kiuchumi sio kuwafuta wafanyikazi na waajiriwa kama ilivyo katika mgogoro wowote wa kiuchumi katika mfumo wa kirasilimali, bali suluhisho ni kupunguza gharama ya uzalishaji, ikiwemo gharama za mishahara, na suluhisho hili halipelekei kifo cha gurudumu la uchumi wala ubadilishanaji wa mgogoro mmoja hadi mwengine, bali kinyume chake litaendelea hata kama ni pole pole. (Utapata ufafanuzi wa kina wa manufaa ya nidhamu ya dhahabu na fedha katika uchumi katika kitabu “Nidhamu ya Kiuchumi katika Uislamu” uk. 270 (Kiarabu))

– Uharamishaji riba juu ya mikopo, benki za riba ni muhimu katika nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali, kwani riba imekuwa ndiyo msingi wa biashara, ukulima na viwanda. Mikataba baina ya wakopeshaji na mabenki ni mikataba ya riba kwa sababu yanauza pesa kwa pesa, na kwa sababu yanazipatiliza juhudi za watu kwa riba iliyo lazimishwa pasi na kuanikwa katika aina yoyote ya hasara. Katika nidhamu ya kiuchumi ya Uislamu, Bait ul Mal hukopesha pesa ziso riba, baada ya kuangalia uwezekano wa kutumia pesa. Anayetaka kukopa huzihitaji imma kukimu maisha, au kwa ajili ya ukulima. Ama kwa hitajio la kwanza, Uislamu umedhamini hili kupitia kumhakikishia kila raia wa dola haki ya kuishi. Hitajio la pili limetimizwa na Uislamu kupitia kukopesha pesa kwa wahitaji bila ya riba. Omar ibn al-Khattab (ra) aliwapa wakulima pesa za kutosha nchini Iraq kutoka kwa Bait ul Mal, hadi ardhi zao zianze kuzalisha. Watalinganishwa na  wakulima kama wao, wanaohitaji pesa, ili kujitosheleza kimaisha. Mtume (saw) alimpa mtu kamba na shoka ili akakate kuni na kuziuza ili ajikimu kimaisha.

– Uharamishaji wa ufichaji mali, pesa zilizozuiwa na wamiliki matajiri wa uchumi wa kirasilimali zilipelekea kujiondoa katika soko na kusitisha mzunguko mikononi mwa watu, ambao unapelekea upungufu wa uzalishaji wao kwa sababu hitajio la bidhaa limepungua na kusimamisha gurudumu la uchumi na hili hueneza ukosefu wa ajira katika mujtama kutokana na uchache wa mapato mikononi mwa watu. Katika nidhamu ya kiuchumi ya Uislamu, ufichaji mali umeharamishwa; pesa ni ala ya ubadilishanaji baina ya pesa kwa pesa, baina ya pesa kwa juhudi, na baina ya juhudi kwa juhudi. Kipimo hiki cha ubadilishanaji na maadamu ala hii inapatikana kwa watu, hii itasukuma kazi mbele na itaruhusu watu katika mujtama na matumizi yao jumla yatakuwa katika muundo wa duara la kuendelea linalo endeleza utajiri wa kiuchumi wa mtu binafsi na jamii. (Kwa kuwepo haja ya kusoma kuwa kuna tofauti kubwa kati ya ufichaji na akiba, utapata ufafanuzi katika kitabu “Nidhamu ya kiuchumi katika Uislamu” uk. 251 (Kiarabu). Kifungu cha 142 cha Kielelezo cha Katiba ya Dola ya Khilafah: “Ufichaji mali umeharamishwa hata kama Zakah inatolewa.”

Hizi ni baadhi ya suluhisho msingi ambayo nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu imeziweka sio tu kuondoa ukosefu wa ajira lakini pia kumaliza aina zote za ufisadi na utawala wa sera za kiuchumi za kirasilimali juu ya nchi.

Ni mbinu zipi na hatua zipi za kivitendo zitakazo chukuliwa na Khilafah Rashida ili kuzuia ukosefu wa ajira?

1- Kutafuta usawa wa kiuchumi kupitia kuwapa raia mafukara pekee wa dola mali za dola katika Bait ul Mal ambazo si katika zilizo kusanywa kutoka kwa Waislamu, bali kutoka katika mali ya ngawira hadi kupatikane usawa wa kiuchumi katika utoaji huu. Pindi Mtume (saw) alipoona mianya katika umilikaji wa mali baina ya Muhajireen na Answar, yeye (saw) aliwagawanyia pesa za ngawira (Fai’) Muhajireen pekee, ambazo yeye (saw) alizipata kutoka kwa Bani An-Nadhir, ili kutafuta usawa wa kiuchumi. Imesimuliwa kuwa pindi Mtume (saw) aliposhinda kwa amani dhidi ya Bani al-Nadhir, na Mayahudi hao kufurushwa, Waislamu walimuomba Mtume (saw) kuwagawanyia (ngawira) baina yao. Aya ikateremshwa:

…وَمَا أَفَاءَ اللَُّ عَلَىٰ رَسُولِهِ مِنْهُمْ فَمَا أَوْجَفْتُمْ عَلَيْهِ
“Na mali aliyo leta Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwao hamkuyakimbilia mbio [hamkuyapata kwa kupigana]”
[Al-Hashr: 6]

Mwenyezi Mungu (swt) ameufanya ugawanyaji uwe mikononi mwa Mtume (saw) Aligawanya miongoni mwa Muhajireen, na hakuwapa Maanswari chochote isipokuwa wanaume wawili. Walikuwa mithili ya Muhajireen katika ufukara.

2- Mpangilio mpya wa mali ya Ummah ambayo ni ruhusa ya Mtungaji sheria kwa kundi kushiriki pamoja katika utumizi wa mali hiyo (ya Ummah). Na vitu vilivyo fafanuliwa kuwa mali ya Ummah ni vitu ambavyo Mtungaji sheria amevitaja kama vile vinavyotumiwa kwa ushirika na kundi, na kuwazuia watu binafsi kutokana na kuvimiliki peke yao na ni aina tatu:

(A) Huduma za jamii, kiasi ya kuwa ikiwa hazitapatikana katika mji au kikundi watatoka nje kwenda kuzitafuta, kama maji, malisho, huduma za jamii, nk.
(B) Madini yasiyo malizika.
(C) Vitu ambavyo kimaumbile haviwezi kumilikiwa na watu binafsi, kama barabara, mito, maziwa, bahari, shule za dola, mahospitali, nk.

Kifungu cha 140 cha Kielelezo cha Katiba ya Dola ya Khilafah:
“Kila mtu miongoni mwa Ummah ana haki ya kutumia chochote katika mali ya Ummah, na hairuhusiwi kwa Dola kumruhusu mtu kumiliki au kuitumia kibinafsi.” (Ili kuregelea hukmu za mali ya Ummah na kunufaika kutokana nazo soma Kielelezo hicho cha Katiba na Dalili zake Muhimu kuanzia Kifungu cha 137 hadi Kifungu cha 140)

3- Uislamu umefanya utoaji mahitaji kwa Ummah kuwa jukumula dola kwa sababu Ummah una haki ya kusimamiwa. Dola inajukumu la utoaji mali na huduma kwa raia ikiongezewa na ugavi wa mali hii kwa wanajamii wote ili kila mmoja aimiliki nakuitumia. Bukhari amesimulia kuwa Ibn Umar (ra) amesema:
Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: « الإِمَامُ الَّذِي عَلَى النَّاسِ رَاعٍ وَهُوَ مَسْؤُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ » “Imamu aliye juu ya watu ni mchungaji na yeye ni mwenye kuulizwa juu ya raia wake.”

Hii ni kinyume na yale tunayoyaona leo. Mnamo 2018, utajiri ulimwenguni ulikusanyika mikononi mwa mabilionea 26, ambao ni sawa na ule unaomilikiwa na wanadamu waliosalia!! Kifungu cha 124 cha Kielelezo cha Katiba ya Dola ya Khilafah:
“Tatizo msingi la kiuchumi ni ugavi wa mali na manufaa kwa raia wote wa dola, na kusahilisha utumizi wao wa mali hii na kunufaika kwayo kupitia kuwawezesha kufanya bidii kwayo na kuimilki.”

4- Mtungaji sheria mwingi wa hekima aliwajibisha juu ya mwanamume mwenye uwezo kufanya kazi na kutoa mahitaji msingi (nafaqa) kwa nafsi yake na wale alio na majukumu juu yao. Mtoto mchanga ni wajib kupewa nafaqa, na ikiwa mrathi wake hawezi kufanya kazi, jukumu linaanguka kwa Bait ul Mal endapo hakutakuwa na mtu yeyote aliye na jukumu la utoaji nafaqa yao. Uislamu umeufanya usaidizi kwa mtu mlemavu au anayechukua hukmu ya mlemavu kuwa wajib juu ya Dola kwa mujibu wa Kifungu cha 153 cha Kielelezo cha Katiba ya Dola ya Khilafah: “Dola hudhamini ubunifu wa nafasi za kazi kwa wale wote wanaobeba uraia wake”.

5- Ushajiishaji wa kuhuisha ardhi ya ukulima. Ukosefu wa ajira huondolewa kupitia ajira kwa masikini walio na uwezo wa kulima. Dola hugawanya ardhi zilizokufa kwa wale wasiomiliki ardhi au wanaomiliki sehemu ndogo. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alimpa Bilal Al Muzni ardhi baina ya bahari na jabali. (Ili kuregelea sheria za ugavi wa ardhi zilizokufa na kuzihuisha – Kifungu cha 134, 135, 136 vya Kielelezo cha Katiba ya Dola ya Khilafah).

6- Dola kuanzisha vituo na taasisi za utafiti wa sayansi ya kiteknolojia, hususan kwa kuwa sera ya viwanda imefungika kikamilifu na teknolojia. Endapo dola itawakumbatia wanasayansi na wenye vipaji na kuwapa maisha stahiki, tutaona uvumbuzi ukijitokeza baada ya kuzikwa au kuhama, na Waislamu watarudi pale wanapostahiki kuwa miongoni mwa mataifa katika viwango vyote vya kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kithaqafa.

Na hadi ukosefu wa ajira utakapo kwisha na Waislamu kunufaika kutokana na rasilimali za biladi yao, na matatizo yote ya kiuchumi kutatuliwa, mageuzi ya kimsingi na mapinduzi ni lazima yapatikane, ili jambo hili lienee kila mahali, na jambo hili ni utawala wa Kiislamu, ili wanadamu wafurahie uadilifu, wema na uchungaji wa kisawa sawa kwa mujibu wa hukmu za kishari’ah, na Dola ya Khilafah Rashida iwe ndiyo muundo wa yale tunayowasilisha; Uislamu kama badala kwa urasilimali unaokufa, na Mwenyezi Mungu ifanye kurudi kwake iwe hivi karibuni.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Rana Mustafa

Kwa hisani ya Jarida la Uqab: 29  http://hizb.or.tz/2019/06/01/uqab-29/

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!