Malezi: Jukumu Pana na la Jamii Nzima

بسم الله الرحمن الرحيم

Mada ya malezi inagusa sehemu nyeti ya maisha ya wanadamu sio tu kwa kiwango cha familia bali kwa jamii nzima. Ni mada yenye mjadala mpana kwa wanasiasa, watunga sera za kijamii nk.

Kwa maneno mepesi, tunaweza kusema malezi ni kazi maalumu na endelevu ambayo mwanadamu humsaidia mwanadamu mwengine kwa kumpa nasaha, maelekezo, muongozo au kwa namna nyengine yoyote muwafaka ili kumwandaa mwanadamu huyo mwingine aweze kukabili maisha yake kwa ufanisi na kwa maadili yanayokubalika.

Kwa kuwa malezi ni jambo pana linalohusisha kumuongoza, kumnasihi na kumuonesha njia mwanadamu mwengine katika maisha yake ya kila siku, hapana shaka lina misukosuko mingi, ugumu, vipingamizi, linalohitaji umakini, maarifa, na ustahimilivu mkubwa. Mshairi maarufu wa Kiengereza John Wilmot (1647 – 1680) aliwahi kutamka kuhusiana na changamoto ya suala hilo:

“Kabla ya kuoa nilikuwa na nadharia sita kwa ajili ya malezi ya watoto, lakini sasa (baada ya kuoa) nina watoto sita na sina nadharia yoyote (zote nimeziacha) “

Licha ya ukweli kuwa malezi kwa sehemu kubwa hulenga watoto wadogo, kwa kuwa katika kipindi cha umri wao mdogo ndio huhitajika zaidi kumfinyanga na kumuongoza mwanadamu kwa mustakbali wake, lakini ukweli unabakia pale pale kuwa dhana ya malezi inatanuka na endelevu kwa marika yote ya wanadamu, muhimu tu, bado wanadamu hao wamo katika dunia. Kinachotofautiana baina ya malezi ya wadogo na wengine ni aina ya mbinu zinazotumika kwa mujibu wa kila rika ndani ya jamii. Mfano mzuri katika kiwango cha familia tunaona utofauti wa wazazi wanavyoamiliana kimalezi na mtoto wao mdogo, ni kinyume na namna wanavyotoa maelekezo na muongozo kwa watoto wao wakubwa.

Wote hupewa malezi lakini mbinu hotafautiana.
Ukweli kwamba malezi daima huwa ni suala endelevu pia linadhihirika kutokana na uwepo wa ala mbalimbali ndani ya jamii zinazotumika kila siku katika kufinyanga na kumuongoza mwanajamii awe na mwelekeo mahsusi. Mfano mzuri wa vyombo vinavyotoa malezi ni kama mitaala ya shule, sheria, vyombo vya habari kama redio, runinga , magazeti nk.

Wahenga husema “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”, maneno haya ya hekima yana kiasi fulani cha ukweli, yakimaanisha kwamba malezi na makuzi mema kwa mtoto ni dira muhimu katika kufinyanga maisha yake ya baadae na kuchangia kuwa mwanajamii mzuri.
Malezi mema yanaweza kwa kiasi fulani kupunguza malalamiko mengi katika jamii kutokana na watoto kukosa malezi na maadili na tabia zisizokubalika ndani ya jamii.

Takwimu za Tanzania zinaonyesha kwamba vijana ni zaidi ya asilimia 60% ya idadi ya watu wote. Ukichukua asilimia hiyo, ukajumuisha na idadi ya watoto waliopo utaona wazi wazi ni kwa kiasi gani mzigo mkubwa wa ulezi uliopo.
Malezi si suala linalopaswa kumalizia kwa wazazi, wafamilia na walimu, bali hupaswa kuenea kwa kila mmoja ndani ya jamii husika, kwa kuwa linahitaji mashirikiano na mshikamano wa dhati kwa jamii nzima.

Miongoni mwa udhaifu mkubwa unaotukabili na kuwa tishio kubwa katika kufanikisha malezi katika jamii leo ni uwepo wa tabia sugu ya ubinafsi (individualism). Ni aina ya mwenendo dhaifu ambao awali haukuwepo kamwe, au si kwa kiwango cha ulivyo leo. Na kimsingi dhana hii ni ya kimagharibi ambayo huzalisha tabia ya hatari si tu katika malezi bali katika mambo mengi ya ustawi wa jamii.

Ubinafsi huu ni kuhisi hali ya kujitosheleza binafsi katika mambo. Na katika suala la malezi, kutoa miongozo na nasaha humalizia kuonekana kuwa jukumu la wazazi, wanafamilia na walimu peke yao.

Wazazi na wanafamilia hujihisi na kuwa na tabia kwamba wao peke yao ndio wenye haki na jukumu la kutoa malezi kwa watoto au vijana wao. Na watoto nao au vijana huona nao wenye haki ya kuwapa miongozo, maelekezo, nasaha yaani malezi ni wale watu wao wa karibu tu.

Dhana hii ni ya kimakosa, suala la malezi ni la kila mmoja katika jamii. Kwa maneno mengine, leo umeondoka ile tabia ya jamii nzima kuona kila mtoto ndani ya jamii ni mtoto wao, bali kilichopo ni kila mmoja kukumbatia familia yake tukisahau kwamba watoto wetu huwa wanajumuika na watu wengi katika maisha yao ya kila siku kando na familia zao.
Huko nyuma kila mmoja ndani ya jamii alikuwa akijihisi kuwa mlezi, muelekezaji wa watoto au vijana wote ndani ya jamii bila ya kuzingatia kuwa na mahusiano nao ya kidamu au la.

Ni wakati sasa kuachana na mwenendo wa ubinafsi katika malezi, na badala yake kulibeba jukumu kwa upana na kipamoja ili kujenga jamii ya maadili mema na ufanisi.

Masoud Msellem

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!