Masomo na Da’awa, Yote ni Majukumu Yetu

Kauli ya ‘elimu ni ufunguo wa maisha” ni maarufu iliyochukua nafasi kubwa katika fikra za wengi ndani ya jamii yetu. Kila unaemuona si mkubwa si mdogo, wake kwa waume, wazee kwa vijana wameshughulishwa na kutafuta au kuwekeza katika elimu ya kisekula kwa ajili ya nafsi zao au familia zao wao.

Ni kweli kabisa na hatupingi kwamba suala la elimu ya mazingira yaliyotuzunguka ni jambo lililopewa kipaumbele katika Uislamu na miongoni mwa vitu vya mwanzo kabisa alivyopewa mwanadamu wa kwanza ulimwenguni. Allah (swt)anatusimulia haya kuhusu kisa cha baba yetu Nabii Adam [AS]

وَعَلَّمَ آدَمَ الأَسْمَاءَ كُلَّهَا ثُمَّ عَرَضَهُمْ عَلَى الْمَلاَئِكَةِ فَقَالَ أَنْبِئُونِي بِأَسْمَاءِ هَؤُلاَء إِنْ كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Na Mwenyezi Mungu akamfundisha (nabii) Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya malaika na akasema niambieni majina ya vitu hivi ikiwa mnasema kweli”[TMQ 2: 31)

Amma ufaradhi wa elimu ya kidini unajitokeza pale aliposema Mtume wetu Muhammad (saaw) katika Hadithi yake maarufu:

‘’Kutafuta elimu ni faradhi kwa kila Muislamu mwanamume na Muislamu mwanamke”.

Hata hivyo, kuna ufahamu wa kimakosa katika suala la elimu, na hii ni kutokana na kuanguka Uislamu katika medani ya kiutawala na pia kupigiwa debe fikra batili za mfumo wa kirasilmali /kibepari hususan aqiida yake msingi ya kuitenganisha dini na maisha [ilmaniya/secularism].

Athari ya hayo ikapelekea kuitenga dini na maisha kwa mujibu wa fikra hiyo. Yaani ikapatikana dhana ya ‘elimu ya kidini’ na ‘elimu ya kidunia’ (kisekula). Ikaonekana ili mtu afaidike kivitendo maishani kwa kupata ajira nzuri na kuheshimika katika jamii lazima asome masomo ya kisekula ambayo ni elimu ya kidunia.

Amma kusoma kuhusu udhu, urithi ndoa, bei na manhaj ya ulinganizi wa Kiislamu na mfano wake hii ikachukuliwa kuwa ni elimu ya akhera. Ilhali ukitowa vitendo vichache vya ibada haswa za kiroho moja kwa moja kama swala, swaumu, dhikri nk. vilivyobakia vyote kama bei, urithi, ndoa na uqadhi haya ni mambo ambayo mwanaadamu anafaidika nayo kwanza hapa duniani kivitendo.

Baadhi ya Waislamu kwa masikitiko makubwa wakaathirika sana na ufahamu huo wa kimakosa kiasi cha hata kudharau na kukebehi mafundisho ya dini yao na kuekeza na kuthamini zaidi masomo ya kisekula pekee kwa kudhani kewamba wataongeza rizki, kupata vitu vya kimada na kuonekana kwenda sambamba na maendeleo.

Katika hili lazima ieleweke wazi kwamba Uislamu unaitizama elimu katika upande wa elimu ya faradhi na elimu ya mubaha. Elimu ya faradhi ni yale yote anayopaswa kuyajua kila ‘mukalaf’ (balegh na akil) anayefungwa kushikamana na maamrisho ya dini katika kutekeleza au kujiepusha, kwa sababu kila mukalaf huwa kafungika na kushikamana na hukmu shariiyah zote.

Amma elimu isiyokuwa hiyo huingia katika mlango wa mubaha (iliyoruhusiwa), isipokuwa tu kwa nafasi yake kama dola ya Khilafah kutakapokuwa kuna upungufu wa wataalamu wa fani nyeti au upungufu wa fani fulani katika kuwahudumia raia, hapo huwa ni jukumu na wajibu kwa dola kuhakikisha kutafuta namna ya kupata wataalamu hao ili kujaza pengo kwa kuwahudumia raia.

Hili huingia katika upande wa kuwa dola ni mas-ul wa kuyasimamia mambo ya raia kwa ujumla wake. Kadhalika Uislamu haulifungamanishi kamwe suala la rizq na suala la elimu kama baadhi wanavyodhani.

Kwa hivyo, kutokana na ufahamu wa kimakosa unaogongana na Uislamu ambao chimbuko lake ni mfumo wa kibepari uliotuathiri leo imekuwa ni vigumu sana kwa walio wengi katika vijana wa Kiislamu katika elimu ya kati au elimu ya juu ya chuo kikuu kukuelewa kuhusu kubeba majukumu ya Uislamu likiwemo kuulingania na kuibeba da’awa ya Kiislamu isipokuwa wachache tu. Wengi hutoa visingizio kwamba hawana muda, wamezongwa na mitihani nk.

Hali hii imekita katika bongo za vijana wengi wa Kiislamu kiasi cha kubeba ufahamu kwamba ati ukijishughulisha na mambo ya dini na da’awa itakuwa sababu ya kutofaulu masomo yako. Jambo ambalo si kweli! lakini liwe kweli, nani mwenye haki ya kutoa tafsiri ya kufaulu na kutofaulu? Kuna wangapi waliodharau mambo ya dini na kujishughulisha na masomo peke yake lakini mwisho walifeli. Japo mtu anaweza kuhoji kwamba wapo pia waliodharau mambo ya dini lakini wakafaulu!!! Ndio tunakubali walifaulu mitihani yao ya shule lakini mbele ya Allah Taala jee wamefaulu?

Sisi tukiwa Waislamu tuliobeba mfumo wetu bora na ukombozi kwa wanaadamu wote inatupasa tuelewe kwamba ni muhimu kufaidika na elimu hizi, kwa kuwa Uislamu wetu umeruhusu [mubaha]. Lakini pia tukumbuke ni wajibu kuusoma Uislamu wetu na kubeba majukumu yake ikiwemo ulinganizi majukumu kwa kuwa hizo ni faradhi kama faradhi nyingine tunazozijua kama swala, saumu, hijja nk.

Ni wajibu tutoe kipaumbele katika suala la ulinganizi/ daawa kwa kuulingania Uislamu kama mfumo mbadala wa ubepari ili kuuwezesha Uislamu wetu kusimamia maisha ya wanadamu wote.

#UislamuNdioUfumbuziSahihi

Risala ya Wiki No. 64

03 Rabi’ al-thani 1441 Hijri 30/11/2019 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

http://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!