Krismasi’ Fursa Adhimu ya Kuwalingania Wakiristo Uislamu

Wakati siku ya Krismasi ipo mlangoni ni vyema kukumbusha kuwa sikukuu hii ya wakiristo na nyengine kama ‘Pasaka’ hutumika kama mbinu ya kuleta ‘ukuruba baina ya Uislamu na Ukiristo’, pamoja na jamii za wafuasi wa dini mbili hizi. Kwa kusisitiza kauli za ‘kuishi pamoja’, ‘maelewano’ na ‘mashirikiano ya kidugu’. Aidha, kwa kaulimbiu kuwa dini zote zinatoka kwa Mungu na chimbuko la Ibrahim As.

Fikra hii ni ya kikafiri, hatari na haramu katika Uislamu kuibeba, kuilingania au kuipigia debe, na kimsingi inawadhuru Waislamu kwa kuwa dini yao ndio ya haqi. Tunasema hakuna ukuruba baina ya haqi na batil, wala baina ya Uislamu na ukafiri kwa namna yoyote. Ukuruba unaoruhusiwa baina ya Waislamu na wasiokuwa waislamu sio katika masuala ya kidini, bali katika miamala mingine kama ya kiuchumi kama vile biashara, mikataba nk, kwa sharti haiko kinyume na Uislamu.

Waislamu ni wajibu kujiepusha mbali na fikra na mtazamo huu wa ‘ukuruba wa kidini’ na kuupiga vita kwa nguvu zote za kifikra. Badala yake kwa kuwa sisi ni Ummah bora wenye mfumo wa haqi unaokubaliana na maumbile tunapaswa kuijadili Krismasi kwa kuleta mijadala ya kistaarabu kwa ukristo na wakristo kwa kuwalingania na kuwavuta kuja katika Uislamu kwa kutumia hoja za kiakili. Tunasema kwa hoja za kiakili, kwa kuwa wao wakiristo hawakikubali kitabu chetu kitukufu cha Quran, na sisi hatuamini kitabu chao cha biblia. Bali tunakiri na kuamini kwamba kilikuweko kitabu cha injili alicholetewa Nabii Issa As. Ila hiki cha leo sicho.

Mtume SAAW kamwe hakuiwacha fursa ya kuwalingania wakiristo kadiri ilivyowezekana hata katika mazingira magumu, kama alivyomlingania Addas, mtumishi wa kikristo katika shamba la mizabibu la Rabia, alipokuwa Mtume SAAW akirejea Makka kutoka Taif akiwa na majeraha baada ya kupigwa mawe. Aidha, alizidisha kuwalingania makafiri wa kikristo baada ya kusimamisha dola ya Kiislamu ndani ya Madina. Kama alivyosimamisha hoja nzito dhidi ya ujumbe mkubwa wa wakiristo 60 wa Najran uliokuja Madina mwaka wa tisa Hijria chini ya kiongozi wao Abu-Masih. Na wakiristo walipojikanganya na kuzikataa hoja zake, Allah Ta’ala akamtaka Mtume SAAW afanye maapizano nao kwa kiapo maalum (mubahala) cha kuomba laana kwa muongo. Quran Tukufu inatukumbusha:

فَمَنْ حَاجَّكَ فِيهِ مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَكَ مِنْ الْعِلْمِ فَقُلْ تَعَالَوْا نَدْعُ أَبْنَاءَنَا وَأَبْنَاءَكُمْ وَنِسَاءَنَا وَنِسَاءَكُمْ وَأَنْفُسَنَا وَأَنْفُسَكُمْ ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَلْ لَعْنَةَ اللَّهِ عَلَى الْكَاذِبِينَ (آل عمران: 61).
“Watakaokuhoji katika haya baada ya kukufikilia ilimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zenu na wake zetu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mungu iwashukie waongo.”(Tmq 3:61)

Jambo hilo pia wakiristo wa Najran walilikataa. Kiongozi wao akawaeleza wenzake:

“Enyi manasara! Mimi naona nyuso ambazo, lau zitaomba jabali liondoke lilipo basi linaweza kuondoka. Kwa hivyo msiapizane nao msije mkaangamia”.

Kisha wakamueleza Mtume SAAW: ‘Ewe Abul-Qasim tumeonelea tusiapizane na wewe’. Mtume akawambia: ‘Basi silimuni’ wakakataa kusilimu kisha wakakubali kulipa jizya.

Katika kipindi hiki cha Krismas tuchukuwe fursa mwanana kuwaonesha wakiristo juu ya udhaifu wa fungamano lao duni kwa Muumba. Kwa kuwa unyenyekevu wao hudhihirika siku ya krismasi, jumapili au baadhi yao jumamosi, tena katika baadhi ya ibada chache za kiroho. Na kipindi chote kilichobakia katika maisha yao hawana suluhisho lolote kutoka katika dini yao linalotatua matatizo yanayomkabili mwanaadamu. Amma yawe matatizo ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na mengineyo. Aidha, kuwaonesha wakiristo kwa hoja kwamba Issa as. hakuwa Mungu, kwa kuwa Mungu hazaliwi, kwa kuwa yeye alizaliwa na mwanaadamu, na kinachozaliwa ni kiumbe, na kiumbe hakina budi kufa, na Mungu kwa kuwa ni Muumba kamwe hafi, na akifa huwa si Mungu.

مَا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلاَّ رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ كَانَا يَأْكُلاَنِ الطَّعَامَ انظُرْ كَيْفَ نُبَيِّنُ لَهُمْ الآياتِ ثُمَّ انظُرْ أَنَّى يُؤْفَكُونَ (المائدة:

“Hakuwa Masihi mwana wa Mariamu ila ni Mtume.(na sio Mungu) Wamekwishapita Mitume kabla yake. Na mama yake ni mwanammke mkweli. (nae pia si Mungu). Wote wawili walikuwa wakila chakula (kwa kuwa ni wanaadamu). Angalia tunavyowabainishia Aya, kisha angalia vipi wanavyogeuzwa.’(Tmq 5:75)

#UislamuNiUfumbuziSahihi

Masoud Msellem

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!