Vifurushi Vipya Vya Afya Tanzania ni Unyonyaji wa Kibepari

Habari :
Tarehe 28/11/2019 Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulizindua vifurushi vipya ambavyo vimezua mjadala nchi nzima kuhusu mustakabali wa huduma za afya kwa watu wa chini (masikini).

Maoni :
Vifurushi hivyo vipya vinajuulikana kwa majina ya ‘Najali’,’Wekeza’ na ‘Timiza’. Kimsingi kifurushi cha ‘Najali’ kinaonekana ni kwa ajili ya masikini kwani kina malipo kidogo kikiambatana na huduma chache pia, kifurushi cha ‘Wekeza’ ni kwa familia za kipato cha kati kwani kinahusisha malipo ya wastani na huduma za wastani vilevile, na kwa upande wa kifurushi cha ‘Timiza’ hiki ni kwa watu wenye uwezo kwani kinahusisha malipo makubwa na huduma nyingi kama si zote.

Katika vifurushi hivi vipya mtu mmoja anatakiwa kuchangia kati ya 192,000Tsh na 684,000Tsh kwa kifurushi cha kiwango cha chini kabisa cha ‘Najali’ na pia anatakiwa achangie kati ya 516,000Tsh na 984,000Tsh kwa kifurushi cha kiwango kikubwa cha ‘Timiza’

Familia ya wastani ya mume, mke, na watoto wanne inatakiwa kuchangia mpaka 900,000Tsh kwa kifurushi kidogo cha ‘Najali’, na kuchangia mpaka 2,220,000Tsh kwa kifurushi cha ‘Timiza’.

Kwa upande mwingine, kifurushi cha ‘Najali’ kinajumuisha siku 30 tu za matibabu kwa mwaka na ilhali kitawalazimu wateja kuchangia miaka miwili mfululizo ili waweze kupata huduma za uzazi na kujifungua.

Haya yote yanaonesha ubaya na uovu wa mfumo wa kibepari kwa kufanya huduma za kijamii kuwa ni biashara, jambo linalopelekea kuwagawa watu (kwa msingi wa kipato). Bila ya shaka hali hiyo itaongeza mgawanyo wa matabaka katika jamii ambayo ni tishio katika ustawi wa watu kama kitu kimoja.

Wakati taarifa zinaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi masikini duniani, basi vipi watu wake masikini wataweza kuchangia huduma hizo ghali za vifurushi hivyo vya bima ya afya? Huu ni unyonyaji wa wazi kwa watu wanyonge na maskini badala ya kufanya mambo rahisi kwao.
Huduma za afya nchini Tanzania zinakabiliwa na matatizo mengi, ikiwemo uduni katika huduma zenyewe, rushwa, miundombinu mibovu, upungufu wa wataalamu nk. Badala ya kukabiliana na kutatua matatizo haya kunaongezwa zaidi ugumu na vikwazo kwa walalahoi

Katika ubepari haijalishi ni kwa kiasi gani na ni watu wangapi wataathirika kwa kukosa huduma (mahitaji), bali kubwa linalozingatiwa ni ‘maslahi’ kutokana na makodi na tozo zingine.

Suala hili la bima za afya linaonesha wazi kushindwa kwa mfumo wa kibepari katika utoaji wa huduma za kijamii na kuyafanya maisha ya watu kuwa biashara. Bila ya kutaja kuwa Kiislamu, muamala wa bima umekosa sifa ya kuwa mkataba timilifu, kwa kuwa umejengwa juu ya hali zisizokuwa za uhakika

Katika Uislamu, huduma zote za kijamii ni katika masuala ya kipaumbele cha hali ya juu kwani mojawapo ya majukumu ya serikali ya Kiislamu (Khilafah) ni kusimamia masuala ya watu wake. Ni wajibu kwake kutoa madawa na kujenga hosipitali kwa watu wote kama huduma na si biashara, tena bure au kwa malipo hafifu sana ya kuchangia.

Imepokea na Muslim kutoka kwa Jabir (ra.) kuwa:
“Mtume wa Allah ﷺ alituma daktari kwa Ubay bin Kaa’b (kumtibu alipougua) akamfanyia upasuaji katika mshipa wake “
Pia Al-Hakim ameripoti katika kitabu cha Al-Mustadrak kutoka kwa Zaid bin Aslam, kutoka kwa baba yake ambaye alisema:
“Niliugua sana zama za (ukhalifa wa) Umar Ibn Khatab, hivyo, akaniletea daktari ambaye aliniwekea mlo maalumu (diet)”

Ulimwengu unahitaji Uislamu chini ya dola yake ya Khilafah kama mbadala wa mfumo wa ubepari, mfumo wa kikatili na usiojali ubinadamu unaochukulia kila kitu kwa lengo la kujiongezea maslahi, huku ukiwaacha masikini na jamii kiujumla katika tabu juu ya tabu.

Imeandikwa na Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania.
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir.
#UislamuNiUfumbuziSahihi

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!