Mazingatio ya Ramadhani -4

بسم الله الرحمن الرحيم

Ramadhani Yatukumbusha Suluhisho la Kiislamu katika Suala la Chakula

Mwezi mtukufu wa Ramadhani licha ya kuwa ni katika ibada kubwa na tukufu tuliyoletewa na Muumba wetu kwa ajili ya kushibisha hisia yetu ya kimaumbile ya kumuabudu Mola wetu Muumba, pia ina mafunzo na mazingatio mengi katika masuala ya kila siku ya muamalati (mtangamano)

Moja kati ya mambo hayo ni kutukumbusha suluhisho katika upatikanaji na usambazaji wa neema kubwa ya chakula. Chakula ni miongoni mwa mahitajio ya lazima ya kibaologia (organic needs) ya mwanadamu. Lau mwanadamu anakikosa atafariki. Mahitajio mengine kama hayo ni maji, hewa nk.

Ndani ya Ramadhani namna tunavyoshinda na njaa kwa ajili ya kumnyenyekea Muumba wetu, kila mmoja wetu anapata hisia ya wazi juu ya ulazima wa chakula.

Uislamu umechukua hatua msingi na sera thabiti kuhakikisha uwepesi katika upatikanaji wa chakula. Iwe sera za ukulima, usambazaji, ununuzi, kumlinda mlaji kisharia nk. ili kuwaondolea wanadamu dhiki ya kupata hitajio hilo nyeti na la lazima katika maisha yao.

Awali ya yote Uislamu umeweka msingi thabiti katika aqidah yake, yaani katika imani yake unaamini kwamba rasilmali ya chakula iliyopo duniani ni ya kutosheleza kuhudumia mahitajio ya wanadamu wote. Kwa hivyo, wanadamu bilioni 7 waliopo duniani hakuna sababu ya kulala na njaa. Bali Uislamu unaona tatizo la njaa na ukosefu wa chakula kwa wanadamu duniani ni kukosekana sera thabiti na za kiudilifu za ubepari katika usambazaji wa neema hiyo. Hali hiyo imepelekea kuweko watu milioni 16 duniani wenye kukabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula.

Uislamu umekuja na hatua na sera mbalimbali ili kuhakiksha uwepesi katika upatikanaji wa hitajio la chakula kumfikia kila mwanadamu.

Katika upande wa kibinafsi na kifamilia, Uislamu umewajibisha baba mzazi kulisha watoto na familia yake. Na lau anafariki, warithi wake huwa ni wajibu kuihudumia familia. Na pale familia inapoelemewa na kuzidiwa na jukumu hilo kwa unyonge, dola ya Kiislamu ya Khilafah huingilia kati kuwasaidia.

Pili, katika upande wa kuhamasisha ukulima, Uislamu unahimiza kuhuisha ardhi iliyokufa (Ihya-al mawat). Ardhi iliyokufa ni ile isiyo na mwenyewe na ambayo hakuna mwenye kunufaika na ardhi hiyo. Uislamu unampa haki ya milki ya kisharia mwenye kuihuisha kwa kuifanya kuwa milki yake. Mtume SAAW anasema:

“Mwenye kuhuisha ardhi iliyokufa basi huwa milki yake”.

Matamshi katika hadithi hii yako kijumla/ amm. Kwa hivyo, umiliki huu anaupata Muislamu au dhimmiy. Yaani raia asiyekuwa Muislamu ndani ya dola ya Kiislamu ya Khilafah ( Nidhamu ya Kiuchumi ndani ya Uislamu, Taqiudin an-Nabhan)

Tatu, Uislamu unazuiya kuhodhi ardhi bila ya kuitumia kwa kilimo zaidi ya miaka mitatu. Hata kama ardhi hiyo ni milki yako. Khalifah Umar bin Khattab katika zama zake alimnyang’anya ardhi Bilal ibn al-Harith al-Muzni baada ya kushindwa kuitumia ardhi hiyo ndani ya miaka mitatu. Uislamu unalazimisha uwajibu wa ardhi kutumika kwa kilimo ili inufaishe jamii na kusaidia kusahilisha upatikanaji na uzalishaji wa chakula badala ya kuwapo tu bila ya matumizi.

Nne, Uislamu ukapiga marufuku kukodisha ardhi kwa ajili ya ukulima. Kutoka kwa Rafia ibn Khadeej anasimulia kuwa Mtume SAAW amekataza ukodishaji wa ardhi (Bukhar) Badala yake Uislamu ukataka mmiliki wa ardhi amma aitumie kwa kilimo yeye binafsi, afanye ubia na mwenziwe (musaqata) au ampe mtu mwengine aitumie lakini sio kuikodisha ardhi. Hilo husaidia kuepusha kuifanya ardhi kama bidhaa katika kilimo.

Tano, Uislamu ukaharamisha kumilikishwa mtu binafsi vyanzo vikubwa vya maji kama chemchem kubwa, mito, maziwa, barabara, miundombinu mingine nk. na ukayafanya hayo kuwa ni milki ya Umma mzima ili iwe wepesi kufaidika katika uzalishaji, usambazaji, usafirishaji wa rasilmali hizo katika kilimo nk. Pia, Uislamu ukapiga marufuku kumilikiwa kibinafsi maeneo makubwa ya malisho ya wanyama ili kuepusha uhaba wa ardhi ya malisho. Jambo ambao huleta uhaba wa ardhi na kuibua uhasama baina ya wakulima na wafugaji kama tunayoshuhudia leo Tanzania, Kenya nk. Yote hayo ni kutokana na maeneo ya malisho kumilikishwa watu binafsi, matokeo yake kuwapelekea wafugaji kutangatanga na wanyama wao hadi wakati mwengine kukimbilia maeneo ya ardhi ya ukulima. Hali inayoripua vita na ugomvi mkubwa unaongamiza roho na mali baina ya jamii za wakulima na wafugaji.

Sita, katika upande wa usambazaji wa chakula, Uislamu umepiga marufuku kuhodhi soko la chakula (ihtikar). Iwe kwa wafanyabiashara wachache kupewa kibali peke yao kuagiza chakula au kukificha ili kukipandisha bei. Jambo hili ni maarufu leo chini ya mfumo batil wa kibepari. Na katika kumlinda mlaji, Uislamu ukaharamisha aina zote za kughushi chakula kwa kuchanganyisha kizuri na kibaya. Mahkama ya Qadhi Muhtasib itamlinda mlaji asighushiwe na pia itazilinda mali za Umma ikiwemo mito, maziwa, na maeneo ya malisho ya wanyama yasinyakuliwe na kuporwa na watu binafsi

Haya ni baadhi tu kutoka mfumo wa Kiislamu na suluhisho lake katika kuwarahisishia raia kupata chakula. Kinyume kabisa na mfumo wa kibepari unaotawala dunia leo, uliojaa uoza na dhulma katika sera zake za usambazaji, kiasi cha kuonekana chakula kana kwamba kiko hafifu kulinganisha na idadi ya wanadamu iliyopo duniani.

24 Ramadhan 1441 Hijria – 17 Mei 2020M

Masoud Msellem

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!