Siku ya Demokrasia Duniani: Maadhimisho ya Nidhamu Iliyoshindwa

بسم الله الرحمن الرحيم

Kila tarehe 15, Septemba ya kila mwaka ni siku iliyoteuliwa na Jumuiya ya Kimataifa (mabepari wakoloni) kuwa ni siku ya maadhimisho ya demokrasia duniani.
Siku hiyo imeteuliwa kama kawaida ya mabepari wakoloni wanavyoteua maadhimisho ya qadhia na vitu mbalimbali ili kuwapumbaza watu kuhusu mambo hayo ambayo mara zote huwa yamewashinda katika usimamizi wake. Kwa mfano; walivyoshindwa katika kusimamia ustawi wa mwanamke wakabuni ‘siku ya wanawake duniani’, hivyo hivyo kuna ‘siku ya amani’, ‘siku ya wafanyakazi’ nk.
Siku ya demokrasia hutumika kutafakari kiwango cha demokrasia ulimwenguni, changamoto zake na namna ya kukabiliana nazo ili kuikuza na kuiimarisha kila mahala.
Demokrasia ni nidhamu ya kiutawala (political system) katika mfumo wa kibepari (capitalism ideology), na mabepari wenyewe walivyoifafanua kuwa ni nidhamu ya watu kujitawala, waliyojipangia kwa sheria walizojitungia na kwa dhamira ya kuwanufaisha watu hao.
Msingi mkuu (aqidah) wa nidhamu hiyo ni kutenganisha dini na maisha (usekula) yaani kuondoa haki ya utungaji wa sheria kutoka kwa Muumba na badala yake kuipeleka kwa viumbe (wanadamu) dhaifu.
Dhana ya demokrasia iliasisiwa na wayunani wa kale (wagiriki) na ikaja kuboreshwa na kutabikishwa na mabepari baada ya mapinduzi ya kifikra na kisiasa barani Ulaya kisha ikaenezwa kila mahala.
Demokrasia imejengwa katika nguzo kuu nne kwazo husimama juu yake: ‘uhuru wa kuabudu’, ‘uhuru wa kujieleza’, ‘uhuru wa kumiliki’ na ‘uhuru binafsi’.
Amma ‘uhuru wa kuabudu’ humaanisha kuwa mtu ana haki ya kuamini na kushika dini au imani yeyote, na ana haki ya kubadili dini hiyo wakati apendao au kutoamini dini yeyote kabisa.
Uhuru huu unapingana na Uislamu, licha ya kubaki ukweli kwamba Uislamu haulazimishi wasiokuwa Waislamu kuingia katika Uislamu, lakini hauruhusu mara mtu anapokuwa Muislamu kuacha dini hiyo.
Hivyo, ni wazi kuwa haijuzu kwa Muislamu kukubaliana na ‘uhuru wa kuabudu’ bali hana budi kupambana kifikra dhidi ya nguzo hii.
‘Uhuru wa kujieleza’ wenyewe humaanisha mtu kuwa huru kueleza, kutoa maoni na kutangaza mtazamo wake juu ya jambo lolote pasi na vikwazo au vizuizi vyovyote. Na hii pia ni kinyume na Uislamu, kwani Muislamu amewajibishwa asilinganie au kueleza jambo lolote linalopingana na Uislamu au linaloharibu umoja wa Ummah. Ni kupitia uhuru huu ndio hutumika kumtukana Mtume(SAW) na dini kwa jumla. Ni wazi pia uhuru huu hauna nafasi katika Uislamu.
‘Uhuru wa kumiliki’ huwa ni mtu kuwa na haki ya kumiliki kitu chochote atakacho kwa namna yeyote ilimradi asivunje haki zinazotambuliwa na mabepari kuwa ni haki za watu wengine. Hii inagongana na Uislamu kwa sababu inatoa ruhusa ya mtu kumiliki kitu chochote sawa kiwe kimehalalishwa au kimeharamishwa na Allah (SWT).
‘Uhuru wa kibinafsi’ humpa mtu haki ya kuishi maisha yake ya kibinafsi pasi na kuingiliwa. Humaanisha kuwa mtu ana haki ya kuoa au kuolewa na mtu wa jinsia moja, ana haki ya kuzini, kulewa na kula, kunywa na kuvaa chochote, na mengine mengi pasi na kuingiliwa. Uhuru huu ndio huzalisha mashoga, wasagaji, wabakaji nk. na haupo katika Uislamu. Kwa kuwa Muislamu hupaswa kujifunga na yaliyoruhusiwa na sharia na kujiepusha na maharamisho.
Kwa kupitia nguzo hizo za uhuru huu ndiyo kumezalishwa kitu kinachoitwa “Tamko la haki za Binadamu” kwa azimio la Umoja wa Mataifa ndani yam waka 1948. Tamko hilo kwa makusudi limelazimiswa kuwa la watu wote (universally) licha ya ukweli kuwa wanadamu hutofautiana kutokana na mila, desturi na dini katika kupima mambo.
Nguzo hizo za uhuru zimeleta maafa makubwa katika ulimwengu kama kudharau dini na kuzitusi kiasi cha wafuasi wao kupigana kuzitetea, kuzuwa matusi na kashfa na husuma baina ya watu, kutamalaki biashara za ulevi, ukahaba, kamari, wizi, udanganyifu katika uchumi, ushoga, usagaji, ukosefu wa maadili na kuleta vurugu katika jamii za wanadamu.
Aidha, nguzo hizo za uhuru licha ya nidhamu ya kidemokrasia kuzitetea na kuonesha zina ufanisi kwa kudhamini mfumo wao, ukweli usio na shaka ni kuwa dhana ya uhuru ni uongo na udanganyifu wa wazi. Kwa kuwa kila aina ya uhuru imewekea mipaka maalumu kwa namna moja au nyengine. Kazi ya mipaka hiyo ni kuhakikisha kila uhuru hautokuwa tishio na hatari kwa mfumo wao.
Kuna mifano mingi ya kuthibitisha hayo, katika nchi takriban zote ulimwenguni kuna sheria za kudhibiti matamshi ya kashfa baina ya watu, kuna mipaka katika kumiliki, kuna mipaka katika umri wa kuanza mahusiano ya kijinsia, kuna mipaka katika kutoa maoni kwa kisingizio cha usalama wa taifa nk. Kwa hivyo, nguzo za uhuru ni kuwalaghai wasiojua kwa undani wa mfumo wa demokrasia. Hoja ya mipaka hiyo inayotolewa na vinara wa mfumo huo wa kidemokrasia, ni kuwa hakuna uhuru usio na mipaka. Kama ni hivyo, kwanini hawakubali kuwa suala la uwepo wa mipaka lipo kila mahala, na kwa kila watu kwa mujibu wa mila na desturi zao. Sasa kwanini walazimishe vipimo vya mipaka yao ndio lazima vifuatwe na kila mtu?
Demokrasia kupitia itikadi yake (creed) ya kutenganisha dini na maisha (secularism) licha ya kumdogosha mwanadamu kifikra kwa kummbakizia fikra isiyoingia akilini, ati ya kumuhubiria mwanadamu kwamba Muumba ana mamlaka msikitini na kanisani tu lakini hana mamlaka katika katika Bunge na katika utendaji wa kisiasa. Pia fikra ya usekula imemtenga na kumdhulumu mwanadamu kwa upana kwa kumnyima suala la kumuabudu Muumba wake, jambo ambalo mwanadamu ana hisia ya ndani ya kulihitajia.
Inatosha kwa kila mtu makini hata asiyekuwa Muislamu kujitenga na kujiepusha na nidhamu fisidifu ya kidemokrasia kwa kuwa ni nidhamu ya kikoloni inayoeneza kila aina ya mashaka na tabu kwa ubinadamu.
Na inatosha kwa Muislamu kutokana na imani yake kuona wazi wazi namna demokrasia inavyomnyima Allah Taala haki ya kutunga sheria za kusimamia wanadamu na badala yake inafanya shirki ya wazi kwa kumpa haki hiyo kiumbe dhaifu mamlaka asiyostahiki.
Ni wajibu kwa kila Muislamu kufanya kazi ili nidhamu ya kiudilifu ya Kiislamu ichukuwe mkondo wake kuja kuwanusuru Waislamu na wanadamu kwa jumla
Said Bitomwa
Risala ya Wiki No. 87
04 Safar 1442 / 21 Septemba 2020 Miladi

 

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!