Thursday, 17 May 2018 00:00

Hadhara Ya Kiislam

Maana ya hadhara ni mtazamo wa maisha wa umma unaobeba ufahamu jumla juu ya ulimwengu , uhai na mwanadamu. Na jawabu la nani  ameumba mwanadamu, uhai na ulimwengu. Kwa maana hiyo hadhara humfinyanga mwanadamu awe na fikra maalum na  aridhie kuishi maisha aliyopangiwa na Muumba au akubali kufuata mkondo wa usimamizi ulio tengenezwa na mwanadamu.

Ikiwa umma una beba mtazamo wa maisha kwa mujibu wa mfumo wa maisha wa ubepari yaani mfumo wenye kumpa mwanadamu mamlaka ya kujisimamia mambo yake kwa mwongozo  aliojitengenezea mwenyewe  , umma huo utakuwa unaishi kwa hadhara ya Kimagharibi. Na Ikiwa una beba mtazamo wa maisha kwa mujibu wa mfumo wa maisha wa Uislam ,yaani mwanadamu kujisimamia mambo yake kutokana na mwongozo wa Allah  ,utakuwa unaishi kwa hadhara ya Kiislam.

Hadhara lazima itokane na mfumo wa maisha ambao chimbuko lake ni imani/Aqidah ambayo huzaa nidhamu za maisha iwe za kiuchumi, kijamii na Kisiasa. Ili kukamilisha  na kutekeleza mahitaji ya kimfumo ya kuifanya jamii iwe na malezi ya mfumo huo , hadhara ndio inayochukuwa nafasi hiyo.

 Kwa hivyo  katika maisha yetu tunaishi tukifuata Hadhara za aina mbili tofauti zenye kutokana na mifumo miwili tofauti ambayo ni uislam na ubepari; yaani Hadhara  ya Kimagharibi na Hadhara ya Kiislamu.

Hadhara hubeba amali zote za mwanadamu anazotenda ikiwo mambo ya mila na desturi : mfano mavazi, chakula , makazi, ndoa , malezi, mahusiano ya kijinsia nk. Na haya yote yanajengwa ndani ya mfumo wa maisha husika:

Allah anasema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمْ الإِسْلاَمَ دِينًا

“Leo hii nimeikamilisha dini yenu na nikawapa nyinyi neema zangu na nikawaridhia uislamu ni mfumo wa maisha kwenu.”

Ili kuufanya mfumo wa ubepari uweze kutekelezeka  wanaadamu lazima wawe na mtazamo mpana wa kuishi maisha yao kwa mujibu wa misingi hiyo na kuongezewa na miito mbali mbali ya UN yenye kushajiisha kutimiza malengo ya kimfumo kama vile haki za mtoto,haki za binaadamu, haki sawa baina ya wanawake na wanaume .

Kwa hivyo si jambo la ajabu kwa nchi za Magharibi kufanya kampeni kubwa kupitia UN ya wanawake kupewa haki sawa na wanaume , Haki za mtoto  ,Haki za binaadamu nk.

Kwa hivyo wanawake kutembea nusu uchi na wengine hata uchi wa wazi wazi, wanawake kujichanganya na wanaume iwe katika  maskuli au vyuoni,  wanaume kuishi na mahawara, kutoheshimu wazee , kula nyama ya nguruwe,kucheza kamari na kunywa pombe ,kukuza biashara ya mahoteli na makasino , pamoja kukuza biashara ya Utalii, hayo ni matokeo ya Hadhara ya Kimagharibi.

Watu  wanaoishi maisha hayo huwa wamebeba hadhara ya Kimagharibi hata kama ni waislamu . Na huwa wanatekeleza mahitaji ya kimfumo ya Uhuru wa Kufanya watakavyo na Uhuru wa kumiliki.

Dunia imekumbwa na janga kubwa la kila aina ya maovu kutokana na maisha kubebwa na Hadhara ya Kimagharibi. Zinaa imetapakaa na wanaume hawaoni umuhimu wa kuoa, watoto wengi huzaliwa nje ya ndoa ,Wanawari malukuki kukosa bikira na kubeba ujauzito na wengi wao kuacha kusoma,  watoto kukosa adabu kwa wazee wao na wengi hawataki kuwatunza wazee wao , Wanawake kuwa na mamlaka makubwa katika ndoa zao na hata kutoziheshimu kamwe. Mauaji ya mitaani na hata mashuleni, vitendo vya ubakaji , madawa ya kulevya nk ni sababu toshelem kuwa Hadhara ya Kimagharibi ndio chanzo kikuu cha maovu hayo.

Si jambo jepesi kuyaondoa maovu ya dunia ilhali wasimamizi wa mfumo wa Kimagharibi ndio walio mstari wa mbele kuhakikisha watu wanatenda maovu hayo. Nchi zinazoendelea hukabwa roho watekeleze maagizo ya nchi kubwa ili na raia zao waishi maisha hayo ya Kimagharibi Mataifa makubwa hujidai eti wanataka dunia iwe na amani, utulivu na kuonyesha huruma ummah unapokumbwa na majanga hayo.

Ufaransa iko msitari wa mbele wanawake kupinga wasivae Hijjab wakiwa makazini baada Mahakama ya Ulaya kutoa hukumu hiyo mwezi Machi 217, lakini kabla ya hapo 2010 tayari Ufaransa ilioshaanza mkakati wa kuliondoa vazi hilo la Stara kwa wanawake. www.theguardian.com/world/2017/mar/14.

Ndani ya Amerika kumeshtadi ongezeko la mauaji ya wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu. Katika jimbo la Colorado ,  Skuli ya Columbine,mwaka 2018,  wanafunzi wawili (2) waliuwa wanafunzi wenzao kumi na tatu(13) . https://learningenglish.voanews.com/a/for-teens-school-shootings-are-common/4268667.html

Yote hayo yanakuja kutokana na ukosefu wa malezi mema ya wazee kwa watoto wao. :Lakini wazee hao hawapati fursa ya kuwalea watoto wawe na maadili mema kwasababu watakuwa wanawaingilia Uhuru wao na ni kinyume na mfumo na Hadhara ya Kimagharibi.

Hapa Tanzania kwa kuiga na kulazimishwa tuishi maisha ya Kimagharibi , Serikali imeruhusu mambo kadhaa yanayoshajiisha jamii kukosa maadili kuanzia watu wazima na vijana wadogo , huku kila mmoja akijuwa mtindo wa mila tunaofuata una kwenda kinyume na mila zetu na una ufisadi mkubwa kwa  jamii yetu..Vijana wadogo wa kike na kiume wana uhuru mkubwa kwa wazee wao; wanamilikishwa simu kubwa kuwasiliana wanakotaka, shule zenyewe ni mchanganyiko wa wanaume na wanawake kukuza urafiki wanawake na wanaume bila kuulizwa na wazee, na mengine kadhaa. Kipi kinachoshangaza mimba kabla ya ndoa kuwa nyingi kupindukia?

Wanafunzi waopata mimba katika shule za sekondari  ni ya kutisha . takwim zinaonyesha kwa mwaka 2016 watoto waliopata mimba na kuacha shule kwa mwaka huo  ni elfu nane(8,000) https://www.hrw.org/news/2017/02/14/tanzania

Litaepukwa vipi janga kama hilo wakati ummah unaelekezwa kuishi maisha ya Kimagharibi yenye msisitizo wa kufanyika zinaa yenye kupindukia?

Uislamu ni mfumo wa maisha uliokuja kumtazamisha mwanadamu mahusiano yake na Mola aloumba Ulimwengu,Mwanadamu mwenyewe na Uhai. Ukammuekea misingi ya kuwa Hana Uhuru wa mambo yafuatayo:-

  1. Kuabudu Mola mwengine isipokuwa Yeye
  2. Kuamua atakalo isipokuwa hukumu ya matendo yake yawe  kwa mujibu wa Sharia ya Allah
  3. Kusema akavyo isipokuwa yale aliyoruhusiwa na Mtunga sharia ambaye ni Allah
  4. Kumiliki atakavyo isipokuwa yale aloruhusiwa kwa mujibu wa Sharia ya Allah

Na Hadhara Kiislamu ikawa ni ile  inayotokana na mfumo wa Kiislamu tu . Kwa hivyo Muislamu anatakiwa abebe na awe na matazamo wa maisha unaoendana na hukumu za sharia za Allah pekee. Kattu Abadan hatakiwi maisha yake kuyapeleka kwa kuchanganya hadhara mbili ; uislamu na ubepari/demokrasia.

Kwa hivyo hadhara ya kiislamu imekuja kumtatulia mwadamu yo yote awe muislamu au asiyekuwa muislamu aishi maisha ya furaha hapa duniani na akhera na kuondoa kila fitna ambayo tunazishuhudia hii leo zinazotokana na mfumo na hadhara ya Kimagharibi . kwa maana hiyo Uislamu ni Hadhara Mbadala ya kumfanya mwadamu awe salama duniani na akhera.

Allah anasema: قُلْ لِلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ذَلِكَ أَزْكَى لَهُمْ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ

وَقُلْ لِلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ

“Waambie waumini wa kiume wasinyanyue nyuso zao, na wazihifadhi tupu zao, kwa kufanya hivyo kutawatakasa na maovu.Hakika ya Allah anayajuwa kila wanayoyafanya..Na uwaambie na waumini wa kike wainamishe nyuso zao na kuhifadhi tupu zao”

Na aya mbali mbali zimetubainishia yalio halali na haramu katika miamalati ya biashara, mapambo na mavazi, umuhimu wa kulea watoto wakue na malezi ya kumuogopa Mola wao, umuhimu wa kuwatunza wazee, vyakula vya halali na Haramu , hatari wa mchanganyiko wa wanaume na wanawake, nk

UISLAMU NI HADHARA MBADALA

Muandishi: Suleiman Ame

 

 

 

 

 

 

Read 710 times
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…