Wednesday, 10 May 2017 00:00

Hizb ut Tahrir

Hizb ut-Tahrir ni chama cha kisiasa cha Kiislamu cha kilimwengu kilichoanzishwa mnamo mwaka 1953 miladi ndani ya Al-Quds, Palestina. Maana ya tamko ‘siasa’ Kiislamu ni kuyasimamia mambo ya watu ima kifikra au kivitendo ikiwemo kuamrisha mema na kukataza maovu. Kazi ambayo hufanywa na dola kwa nguvu ya dola, na hufanywa na vyama au vikundi kwa njia ya kifikra na kunasihi bila ya kutumia nguvu ya kivitendo. Hizb ut-Tahrir inajifunga na kufanya siasa kwa upande wa kifikra tu bila kutumia nguvu au mabavu. Lengo la Hizb ut-Tahrir ni kurejesha tena maisha ya Kiislamu kwa kupitia kurejesha tena dola ya Kiislamu ya kilimwengu Khilafah. Chama hichi kinafanya kazi zake ulimwengu wote kwa kuwa ni cha kilimwengu, zikiwemo nchi zenye Waislamu wengi na zenye Waislamu wachache.

Hizb ut-Tahrir ni chama huru kisichofungamana na taasisi, serikali wala jumuiya yoyote kijimbo, kitaifa, kieneo, wala kimataifa.

Njia inayoitumia Hizb ut- Tahrir katika kuleta mageuzi na kufikia lengo lake ni kwa njia halisi kutoka kwa Mtume Muhammad (SAAW). Njia inayojihusisha na kulingania fikra pekee bila ya utumiaji vitendo vya nguvu wala mabavu. Kwa hivyo, Hizb hujifunga na kazi ya kuonesha usahihi wa fikra za Kiislamu na kufichua uovu wa fikra mbali mbali potofu ukiwemo mfumo wa kibepari pamoja na fikra zake za uhuru, ilmaniya, demokrasia nk. Ndani ya njia hii ya kuleta mageuzi iliyothibiti kutoka kwa Mtume (SAAW) kamwe hairuhusiwi kutumia nguvu, wala mabavu kama kuuwa au kuhujumu kwa mabomu. Hizb ut-Tahrir imeshikamana na njia hii kwa kipindi chote cha miaka sitini tangu kuundwa kwake bila ya kutetereka hata kwa ukubwa wa unywele. Licha ya walinganiaji wa Hizb ut-Tahrir kukabiliwa na vitendo vya dhulma, mateso, udhalilishaji, mauwaji, kuvunjwa viungo nk. Kwa msingi huu Hizb ut-Tahrir haiwezi kamwe kufananishwa na harakati zinazotumia silaha wala wanamgambo wa aina yoyote. Yote haya kwa sababu ya msimamo halisi wa Kiislamu wala sio kwa sababu ya kuogopa madhalimu wala serikali za kidikteta zilizoenea ulimwengu mzima

Kwa mujibu wa sheria za Kiislamu, dola ya Kiislamu huasisiwa pahala palipokamilisha sifa na vigezo maalum vya ki-Sheria. Kwa kuzingatia hilo, Hizb ut-Tahrir inakusudia kuasisi dola ya Kiislamu katika nchi kubwa tu za Kiislamu kwa kuwa ndizo zenye vigezo hivyo vya ki-Sheria ikiwemo idadi kubwa ya Waislamu, nguvu, idadi ya watu, maliasili muhimu, uwezo wa kijeshi nk. Amma nchi nyengine zote ndogo ndogo na zilizokosa sifa na vigezo hivyo zikiwemo nchi zetu za Afrika ya Mashariki kamwe Hizb ut-Tahrir haikusudii kuasisi dola katika nchi hizi wala haikusudii kuingia ndani ya mapambano ya kisiasa dhidi ya serikali yoyote hapa, wala kwa namna yoyote. Kazi kubwa ya Hizb ut-Tahrir ukanda wa Afrika Mashariki ni kuwaelimisha Waislamu juu ya ufahamu sahihi wa Kiislamu na kuwataka wajifunge nao, na kuwaonesha wasiokuwa Waislamu uzuri na ubora wa Uislamu ili kuuelewa kama mfumo bora badili. Na haya yote hufanywa kwa njia ya kistaarabu ya migongano ya kifikra tu.

Katika kurahisisha mawasiliano baina ya vyombo vya habari na waandishi wa habari na Hizb ut-Tahrir, chama cha Hizb ut-Tahrir kina utaratibu wa kuweka wawakilishi wake rasmi kwa vyombo vya habari sehemu mbalimbali ulimwenguni, kama wanavyopatikana wawakilishi hao hapa Afrika Mashariki ndani ya Tanzania na Kenya. Wawakilishi hao wana jukumu la kutoa ufafanuzi, masahihisho, maelezo au kuondoa utata juu ya jambo lolote panapohitajika. Hizb ut-Tahrir inaamini kwa udhati kwamba chombo cha habari kuandika uvumi, tuhuma au yasiyo ya kweli dhidi ya Hizb ut-Tahrir bila ya kupata ufafanuzi kutoka kwa wawakilishi wake rasmi, huwa ni dhulma na kinyume na maadili rasmi ya uandishi. Aidha, Hizb ut-Tahrir inaamini jambo kama hilo ni kinyume cha maadili ya usimamiaji wa haki kwa kushindwa kumpa mtuhumiwa fursa ya kujitetea kwa tuhuma iliyoelekezwa dhidi yake. Kwa hivyo, kiuadilifu huwa ni jukumu la lazima kwa kila chombo cha habari kutupatia fursa ya kujitetea na kujibu tuhuma dhidi yetu.

Read 329 times
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…