Tuesday, 06 June 2017 00:00

Mchanga wa madini ni changa la macho

Ubepari na nidhamu yake ya kisiasa ya kidemokrasia ni uhuni, usanii na mchezo wa kuigiza ambapo mtawala huchezea taratibu, kanuni na hata sheria kuwafikiana na maslahi na matakwa yake kwa lengo la kughilibu wasio na uchambuzi wa mambo na kujitafutia umaarufu wa kisiasa. Hilo linadhihirika kwa mara nyengine tena katika qadhia ya mchanga wa maadini.

Raisi kamuuzulu Sospter Muhongo, Waziri wa Maadini kwa mujibu wa dhana inayoitwa “Uwajibikaji wa Kiuwaziri” (Ministerial Responsibility).  Dhana hii hukusudiwa kujiuzulu Waziri au mkubwa yoyote katika watumishi wa Umma (Public official) pale panapotokea makosa ama yanayotendwa na yeye binafsi (individual) katika utendaji wake wa kila siku, au  hupaswa kujiuzulu kwa niaba ya makosa yanayotendwa na watendaji wa chini yake (vicariously) ndani ya Wizara yake.

Chimbuko la dhana hii ni sheria za kiengereza (Common Law), na hufuatwa zaidi na serikali zinazofuata nidhamu ya kiutawala wa kiengereza (Westminster System).

Dhana hii hubeba sifa ya kuwa ni ‘ada ya kikatiba’ (Constitutional Convention) ambayo ni aina ya taratibu au makubaliano yasiokuwa rasmi na yasiokuwa na nguvu ya kisheria kwenye mahkama, isipokuwa hutumika kama msingi wa kimaadili mema zaidi katika utawala, na sio kwa msukumo wa nguvu ya sheria.

 

Raisi ameitumia dhana ya “Uwajibikaji wa Kiuwaziri” dhidi ya Waziri Muhongo lakini hakuitumia dhana hiyo hiyo kwa Waziri wa TAMISEMI wakati Bashite alipofanya ugaidi wa mwaka katika kituo cha Clouds, na pia kutolewa ushahidi bungeni juu ya nia yake ya kuwateka baadhi ya wabunge. Aidha, Raisi hakuitumia dhana hiyo kwa Waziri wa Ndani, wakati Mbunge Bashe alipotamka Bungeni kuwa Usalama waTaifa walimteka yeye  pamoja na wenzake.

Nia yangu sio kusema nani alistahiki kujiuzulu au nani hakustahiki katika mawaziri, kwa kuwa mfumo mzima wa kidemokrasia umeoza na wala hautokaa sawa kwa kujiuzulu mtu fulani, na kwa maelezo hayo inatosheleza kuthibitisha hilo.

Ninachokikusudia hapa ni kubainisha wazi wazi kwa kupitia qadhia hii, namna watawala wa kidemokrasia  wanavyocheza na  taratibu na sheria pale wanapojiskia tu kwa mujibu wa matakwa yao. 

 

Lakini kwa upana zaidi, suala la mchanga wa maadini si jipya limeanza katika miaka ya 90’s kwa mujibu wa ripoti ilivyotamka. Kama ni hivyo, mbona raisi hapendekezi mabadiliko ya kikatiba kuondoa kinga ya maraisi (Immunity) ilhali chama chake kina wabunge wa kutosha, na bila ya shaka wabunge wa upinzani watamuunga mkono kama kweli mpambanaji wa ufisadi huo!  Lakini wapi! hilo hatofanya na wala hatofikiria kamwe! ili kujilinda yeye na kuwalinda wengine. Kwa kuwa demokrasia ni mfumo wa kulindana. Lakini hata angefanya hivyo pamoja na hatua yake ya kuwauzulu mawaziri kamwe haitoweza kutataua qadhia ya maadini.

Msingi wa tatizo la maadini ni msingi sawa wa qadhia nyengine kama Escrow, Richmond nk. Nao ni udhaifu wa sera ya kiuchumi ya kibepari,  ambapo sera hiyo huruhusu kumilikishwa watu binafsi mali za Umma.  Licha ya kuwa sera hiyo kuwa na madhara makubwa, pia katika mchakato wake huzuka mianya mingi tu ambayo hupelekea wizi na ufisadi.  Suluhisho ni kuondoa ubepari na kushika mfumo mbadala, na sio kuja na suluhisho la matawi badala ya msingi.na  ikumbukwe   utajiri wa madini dunia nzima  upo chini ya  mabepari wachache   walio tunga sheria  za kimataifa    ili kudhibiti  madini  kwani madini yankuwa ndani ya nchi lakini sio milki ya nchi hiyo

 

Katika Uislamu chini ya dola ya Khilafah hakungetokea hata harufu ya tatizo kama hili, kwa kuwa ni haramu kwa mtu binafsi au taasisi kumilikishwa aina zote za mali za Umma yakiwemo maadini, bahari, mitambo ya kuzalishia umeme, visima vya mafuta, mito, mbuga za wanyama, vyanzo vikubwa vya maji, madaraja, barabara nk.

 Jee haujafika muda wa kila mtu makini kuona  wazi wazi  maangamizi ya Ubepari kwa wanadamu katika sekta zote iwe siasa, jamii, uchumi nk. ?

 

Masoud Msellem

Mwakilishi Kwa Vyombo Vya Habari

Hizb ut Tahrir Tanzania

Read 301 times
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…