Monday, 17 July 2017 00:00

Ufisadi hautokomeshwa kwa maigizo ya kurudisha pesa

Hivi karibuni, vyombo vya habari hapa nchini Tanzania vimearifu suala la aliyekuwa Waziri wa nishati na madini na Mbunge wa Sengerema kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) William Ngeleja kurudisha pesa takribani milioni 40.4(Tsh) serikalini(TRA). Tunaweza kuliangazia suala hili katika picha ifuatayo:

  • Kimsingi huu ni muendelezo wa tamthiliya inayoendelea ya uchotwaji wa pesa za walala hoi takribani bilioni 306 katika akaunti yaTegeta Escrow ambayo ilifunguliwa kwa pamoja kati ya kampuni ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) kufuatia mgogoro wa kimkataba baina yao. Huu ndio uwajibikaji wa kiutendaji katika serikali za kidemokrasia ambapo mtu hulazimika japo si kikatiba kuwajibika kutokana na kashfa inayomuhusisha na huwa inalenga kupoza hasira za Wananchi.

 

  • Suala hili si geni kwani katika sakata lingine kama hili la mwaka 2012 lililohusisha Akaunti ya Madeni ya Nje(EPA) ilisemwa kuwa baadhi  ya watuhumiwa  wamerejesha pesa hizo, kisha ikafuatiwa na msamaha wa Rais kwa watuhumiwa hao, suala ambalo aliyekuwa Waziri wa Sheria Harrison Mwakyembe alilitetea na kusema“Rais alikuwa sahihi kwa kuwa viko vifungu ambavyo vinampa nafasi hiyo”(Mwananchi 31/05/2016)

 

  • Kwa mara nyingine inaonesha namna viongozi wa kidemokrasia wanavyotumiwa na matajiri wachache kuwadhulumu Walalahoi  katika nchi zao. Na lau si suala hili kuibuliwa tena   ni wazi kwamba pesa hizi zisingelirudishwa.

 

  • Dalili za mchezo mchafu kwa suala hili la Escrow zilionekana mapema pale mkuu wa nchi wa wakati huo ambaye kauli yake ndio ya mwisho inayotarajiwa kutetea maslahi ya wananchi aliposimama hadharani na kulieleza taifa kwamba fedha hizo hazina sifa za kuhesabika kuwa fedha za umma (https://www.youtube.com/watch?v=CZq-mVTlCoU). Imekuwaje tena leo hii wanapojitokeza waliozawadiwa kuzirejesha kwa umma (serikalini)?

 

  • Matukio kama haya ya kurudisha pesa kidogo sana kati ya nyingi zilizoibiwa na kutolewa kafara watu wawili au watatu kwa kufungwa jela yamekuwa ni kawaida hapa Tanzania na tumeona kamwe hayajazuia wizi wa mali ya umma. Hii inaonesha wazi kwamba tatizo sio ulafi wa mtu binafsi bali ni mfumo wa kidemokrasia ambapo kuwa kiongozi ni moja kati ya njia za kujitajirisha na sio kuwahudumia raia.

 

  • Hivyo tatizo hili ni la kimfumo ambapo takriban mataifa yote yanakabiliwa nalo na limekuwa ni moja kati ya changamoto kubwa za mfumo wa demokrasia, kama yanavyothibitishwa haya na aliyekuwa City Minister wa Uingereza Simon Kirby pale alipotamka bayana mbele ya wabunge kwamba “tatizo la kutakatisha fedha ni kubwa mno kwa nchi moja kuweza kukabiliana nalo”( cityam.com/261380/city-minister-simon-kirby-tells-mps-money-laundering......)

 

Mwisho tunasema kwamba mfumo wa ubepari hauna tena nafasi ya kuuongoza ulimwengu, mashaka na madhila yake yamekithiri kwa mwanadamu, kila ifanyikapo juhudi ya kuurekebisha tija yake ni kuongeza madhara yake. Kilichobaki ni walimwengu wote kwa umoja wao kuubadilisha mfumo huu na badala yake kuweka mfumo mwengine muafaka kwa maisha yao, nao si mwengine ila UISLAM.

 

Read 473 times
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…