Wednesday, 31 May 2017 00:00

Uislam mfumo wa ukombozi kwa wanadamu

Ndugu wapendwa waislamu na wageni wote waalikwa katika kongamano hili, tukiwa tunaukaribisha mwezi mtukufu wa ramadhani, Allah (SWT) anasema katika Quran, 2:185 (Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Quran kuwa ni uongozi kwa ajili ya watu). Muongozo ambao ni chimbuko la mfumo wa usilamu.

Kwa bahati mbaya leo dunia yetu hii inatawaliwa na muongozo usio huu wa Quran, muongozo wa mfumo wa Ubepari ambao umemtia utumwani mwanadamu na kumletea maafa makubwa tangu kuasisiwa kwake zaidi ya karne mbili zilizopita. Maafa yasiyo mithilika yaliyoshuhudiwa na yanayoendelea kushuhudiwa na mwanadamu duniani kote kama vile vita kuu ya dunia ya kwanza nay a pili, ukoloni mkongwe na ukoloni mambo leo hasa katika zile nchi zinazoitwa za ulimwengu wa tatu, biashara ya utumwa ijulikanayo Trans Atlantic slave trade iliyoshamiri mwishoni mwa karne ya 17 na 18, mabomu ya nyuklia ya Hiroshima na Nagasaki yaliyoteketeza maisha ya wanadamu zaidi ya laki mbili, vifo vya baharini vinavyoendelea vya wanaoitwa wakimbizi wanaotoka barani Afrika na bara Arabu kuelekea nchi za magharibi, vita vya wenyewe kwa wenyewe hasa barani Afrika na bara Arabu,mtikisiko na mgando wa uchumi duniani wa mwaka 2008 na umasikini uliokithiri duniani ambapo zaidi ya watu bilioni tatu duniani wanaishi chini ya dola 2.5 na bilioni 1.3 wanaishi katika hali ya umasikini wa kutupwa. Afrika pekee idadi ya binadamu wanaoishi katika umasikini uliokithiri ni milioni 544.

Mfumo huu wa ubepari kuanzia itikadi yake umemnyima mwanadamu uwezo wa kufikiri kindani kunako ng’aa ili kufikia imani sahihi juu ya kuwepo kwa Muumba wake, pale ulipofunga mjadala juu ya imani yake ya kisekula kuwa ulazima ni kutenganisha dini na dunia na sio kujadili hili au nini dini, maisha, uhai, binadamu mwenyewe n.k.  Ukamlazimisha kwa hadaa kupitia fikra yake ya uhuru wa kuitakidi ukamuonesha kuwa ni jambo bora kwake kushika fikra hii, ila ukambainishia kuwa ni suala la kibinafsi. Kama alivyosema Profesa wa Kimarekani, Stephen Hawking “Mungu anaweza kuwa yupo, ila sayansi inaweza kuelezea maumbile”

Itikadi hii haimpi mwanadamu majibu sahihi ya kukinaisha kwa mujibu wa maumbile yake ya kuwa yeye muda wote anakiri kuwa ni dhaifu na kila kilichomzunguka kuwa ni dhaifu na vyote huhitajia mwenye uwezo usio na kikomo, ambaeni Muumba wake. Ikamuacha binadamu katika fazaa na kukosa utulivu mkuu unaohitajika. Na hatimae itikadi hii ikazaa maafa makubwa hasa katika nchi zijulikanazo kama zilizoendelea na nchi zetu pia kwa kukosa utlivu mkuu (unaotokana na  itikadi ya kiakili iliyo sahihi anaouhitajia mwanadamu) na kukosa kufungamanisha maisha haya ya duniani na yajayo baada ya kifo. Maafa hayo ni kama ya kujiua, ambapo Marekani ina wastani wa vifo 44,193 kila mwaka(vinavyoigharimu dola bilioni 51), Uingereza vifo 6188 katika mwaka 2015, Japani zaidi ya vifo 25,000 katika mwaka 2014 kwa wastani wa vifo 70 kila siku!, Uganda ni ya nne kwa vifo katika Afrika, Afrika ya kusini ni ya nane kwa vifo duniani, Tanzania kutoka mwaka 1995 hadi 2000 kumerikodiwa idadi ya vifo 3420. Na idadi ya kushitua zaidi kwa mujibu wa ripoti ya WHO ya mwaka jana watu laki nane hujiua kila mwaka!

Mfumo huu kupitia itikadi yake ukamgawanya pande mbili; roho na mada(kiwiliwili) na kumkosesha uzani katika kushibisha ghariza zake. Wakapatikana watu wa kiroho – watu wa din –na watu dunia. Dunia inaendelea leo kushuhudia aibu kubwa kwa mfano, kuripotiwa kwa idadi kubwa ya kunajisiwa kwa watoto wadogo na watu wa dini wa kanisa fulani.

Ama mfzaiko, ushenzi na ukatili unaofanywa na watu wanaoitwa wa dunia kutoka na fikra ya uhuru(freedom) unaendelea pia kumdhalilisha binadamu kwa kumnyang’anya utu na heshima yake adhimu aliyotunukiwa na Muumba wake. Uhuru wa kumiliki, kibinafsi, kujieleza na kuitakidi. Aina zote hizi za uhuru ndizo zilizozaa na kuendeleza husuda za kiuchumi kwa mataifa yaliyoendelea dhidi  ya nchi changa(kama inavyodhihirika wazi katika kadhia za global warming, ubinafsishaji, biashara huru, soko huru n.k), ushoga, umalaya,ubakaji, ujambazi, utekaji, rushwa, mporomoko wa maadili, mauaji, maafa ya Charlie Hebdo, kupatikana akina Geert Wilders, kashfa za panama papers n.k.

Muumba wa mbingu na ardhi na wanadamu anasema  katika Quran 14:1 “Kitabu tumekiteremsha kwako ili uwatoe watu kutoka gizani kwenda kwenye nuru”. Hivyo basi mfumo wa Uislamu ambao chimbuko lake ni kitabu kitakatifu cha Quran umekuja kumkomboa mwanadamu kutoka utumwani wa kila aina na kumfungua minyororo yote iliyomzonga. Kutoka utumwa wa kiitikadi wa binadamu kuabudu vitu vya kushikika au kuabudu mawazo na fikra za binadamu mwenziwe na kunyanyua heshima yake na utu wake juu ya kila kitu duniani kwa sifa yake kama binadamu.Ukamkomboa  mwanadamu kutoka katika maafa yote yanayoletwa na mifumo ya kibinadamu.

Kihistoria Uislamu kwa sifa yake kama ni mfumo wenye itikadi na masuluhisho yote ya matatizo ya binadamu umeweza kumkomboa mwanadam wa karne ya saba AD na bado Uislamu unao na utaendlea kuwa nao uwezo huu hadi siku ya mwisho wa dunia hii.

Usilamu uliwakomboa warabu wa majangwani kwa sifa yao kama ni binadamu na si vyenginevyo.  Warabu walioishi katika zama za dola mbili kuu za Kiroma na Kifursi, dola ambazo hazikuona umuhimu wowote kuivamia na kuitawala jamii ile ya warabu. Warabu hawa waliishi gizani kwa karne kadhaa katika kipindi kiitwacho cha ujahilia. Wakipigana na kuana ovyo na kurithishana uadui kizazi baada ya kizazi, wakila nyamafu, walikuwa hawahishimu jirani, mwanamume akioa ndugu wawili kwa wakati mmoja, wakinywa pombe, wakizini zina za kila aina, riba ilitapakaa, dhulma na udhalilishaji vilienea, binadamu akiuzwa na kununuliwa kama bidhaa tu sokoni, urongo na ujinga vilienea, matijiri hawakutumia mali zao kwa ajili ya masikini, walizika watoto wao wa kike wakiwa hai kwa hofu ya aibu. Haya ndio mafungamano yao ya kijamii yalivyokuwa. Baya zaidi waliabudu vitu vya kimada kama masanamu waliyoyaweka katika nyumba takatifu ya Al-kaba. Kwa hakika ilikua ni jamii iliyokufa kifikra na ni jamii duni kwa hali zote za ubinadamu. Heshima yao kubwa ilikua tu ni walizinzi wa Al-kaba na watoaji huduma kwa mahujaji wa hija za kijahili wakati ule.

Lakini hali hii duni ya binadamu ghafla ilibadilika, tena kwa kipindi kifupi mno kwa mujibu wa historia ya maendeleo ya binadamu katika mfumo wa ubepari au hata ujamaa. Kutokana na nguvu ya kifikra – itikadi – ya Uislamu, ilibadilika hali hii na kuwa ya kung’aa na endelevu. Ukombozi na mabadiliko haya vililetwa na Mtume Muhammad (SAW) ndani ya miaka ishirini na tatu tu. Kipindi alichoshushiwa wahyi  wa Uislamu na kuupeleka kwa jamii ya warabu(kama nukta kianzio). Mfumo huu wa Uislamu ukawanyanyua warabu hawa ukawapatia izza, heshima, utu na nguvu za kueneza thamani hizi bara Arabu yote. Kama alivyoweka bayana Ja’afar Ibn Abi Talib mbele ya mfalme Najash, vitabu vya historia ya thaqafa ya kiislamu vimeeleza haya kama kitabu kiitwacho Sirat Ibn Hisham juzuu ya kwanza uk 336 na pia kitabu kiitwacho Al-Raheeq Al-Makhtum uk 84 cha Swafiyuu Al-Rahman Al-Mubarakfury. Na pia ukombozi huu na mabadiliko haya yameelezwa na wasomi kadha wa kimagharibi katika vitabu vyao, wakikiri namna Muhammad(SAW) alivyoleta ukombozi na mabadiliko na maendeleo endelevu kwa mwanadamu.

Kwa vile binadamuu habadiliki, ghariza zake na mahitaji yake ya kiviungo yanabakia kuwa ni yale yale wakati wote, zama zote na pahala popote. Hivyo basi, mfumo huu wa Uislamu unamfaa kumkomboa mwanadamu wa karne hii ya ishirini na moja duniani kote. Unamfaa kumkomboa katika nyanja zote kiitikadi, kiuchumi, kisiasa, kijamii nk.

Kiitikadi, ambayo ndiyo fikra kiongozi na kitegemeo kwa mwanadamu katika kuutekeleza na kuubeba mfumo, Uislamu ukamlazimisha mwandamu atumie akili yake kutafakari  juu ya maumbile yote anayoyaona yaliyomzunguka akiwemo yeye mwenyewe, na bila ya kumtenza nguvu ili kufikia itikadi (imani) ya kumuamini Muumba wake, naye ni Allah(SWT) aliyeumba kila kitu. Quran 2:219 “Hivyo hivyo Allah anakubainishieni aya(dalili) ili mufikiri”. Na pia Quran 2:256 “Hakuna kulazimishwa(mtu kuingia) katika dini – ya Uislamu”. Hivi ndivyo mfumo wa uislamu unavyomkomboa mwanadamu kiitikadi, itikadi ambayo inawafikiana na maumbile yake ya kuwa yeye ni dhaifu na muhitaji na ni itikadi ya kiakili. Maana yake binadamu kuamini kuwa kuna Muumba wake na yeye binadamu ni kiumbe na kila kitu ni kiumbe, vyote vimeumbwa na Muumba mmoja tu naye ndie anaye viendesha. Naye ndie aliyeumba uhai na umauti. Na hii ndio maana ya roho(haikusudiwi siri ya maisha hapa, ambayo ni Allah tu ndie ajuae), siyo roho iliyozaliwa na fikra ya kisekula ya kumgawa mwanadamu pande mbili, ambazo zimemtumbukiza mwanadamu katika dimbwi la maafa na aibu. Kwa itikadi hii ndivyo mfumo wa  Uislamu ulivyoshibisha ghariza ya mwanadamu ya kuabudu kwa kumbainishia fungamano lake na Muumba wake na kumjaza mwanadamu utulivu maridhawa maishani mwake kwa kubeba itikadi hii sahihi.

Mfumo wa Uislamu ukatandika masuluhisho ya matatizo ya binadamu katika nyanja zote zilizosalia maishani. Huku ndiko kushibisha ghariza za kubakia (survival instincts) na ghariza za kijinsia(sexual instincts)na mahitaji ya kiviungo. Kwahiyo mfumo wa Uislamu ukamkomboa mwanadamu kutoka katika maafa yote yaliyobainishwa hapo awali na mfano wake, pale ulipoweka nidhamu zote za maisha kwa haki na uadilifu na kuwa ni rehema kwa mwanadamu ulimwenguni kote. Na ukailazimisha serikali yake kuutekeleza kivitendo na kuubeba kwa mataifa mengine ulimwenguni.

Mfumo huu ukaweka nidhamu ya kiuchumi iliyo bora kabisa yenye kumfaa binadamu wa leo wa karne ya ishirini na moja. Nidhamu adilifu yenye kumpatia kila mwanadamu aliyeamua kuishi chini ya serikali ya mfumo huu mahitaji yake yote ya msingi kama kula, kuvaa na pakuishi. Na pia kumuekea mazingira muafaka na mepesi kufikika ili kukidhi mahitaji yake ya ziada. Nidhamu ya uchumi inayogawanya rasli mali kwa ummah mzima na kwa uadilifu. Nidhamu ya uchumi isiyombinya mnyonge wala kumdhulumu tajiri kwa utitiri wa kodi.

Mfumo wa Uislamu ukaweka nidhamu ya kisiasa na uongozi ya uadilifu kwa mtindo wa checks and balance . Katika nidhamu hii ubwana ni wa Allah Muumbaji, maana yake ubwana ni wa sheria na sio kuwa juu ya sheria. Na mamlaka humilikiwa na umma, maana yake ni umma ndio wenye haki ya kumchagua kiongozi wamtakae. Na sio kama ilivyo katika udanganyifu wa mfumo wa ubepari ambapo kupitia demokrasia hudanganya watu eti ndio wenye haki kuchagua kiongozi wamtakae, wakati uhalisia ni kuwa kundi la watu fulani tu ndio lenye maamuzi ya nani awe kiongozi kwa maslahi yao na si kwa maslahi ya rai wote. Katika nidhamu hii ya mfumo wa Uislamu kiongozi huwa kiongozi kweli, ana watumikia raia wote kwa haki na uadilifu, kwasababu itikadi ya mfumo huu imeshamfafanulia mwanadamu mafungamano ya maisha haya na maisha ya baada ya kifo. Kiongozi anayesimama mbele ya mahkama kwa kushitakiwa na kutii shaeria kama ilivyotokezea kwa baadhi ya viongozi huko nyuma kama Ali (R.A).

Mfumo huu ukaondosha fazaa katika jamii kwa kuweka nidhamu bora ya kijamii. Ukampangia mwanadamu vipi ataweza kushibisha ghariza zake za kijinsia. Ukabainisha mafungamano na mahusiano ya mwanamke na mwanamume na nmna ya kuyaendea maisha ya kila mmoja. Ukabainisha maisha ya mke na mume na familia. Katu mwanadamu hakuachwa holela ashibishe ghariza zake za kijinsia holela na kumtoa katika ubinadamu kama ilivyo katika mfumo wa ubepari.

Kwa umma wa kiislamu wote hapa nyumbani na kwengineko ulimwenguni tajiri na masikini, msomi na mwanafunzi, maimamu na wafuasi, wanaume na wanawake sote tuna wajibu wa kubeba ulinganizi, kwani mfumo huu ili umkomboe mwanadamu kimsingi na kikweli na kumuendeleza maishani lazima usimame kiserikali katika moja ya nchi kubwa za waislamu.

Mfumo wa Uislamu hauna haja ya kukopa popote, iwe kwenye ubepari au ukomunisti ili kuleta ukombozi wa kweli wa mwanadamu. Kwani mfumo huu ni mfumo uliokamilika katika hali zote kwasababu unatoka kwa Muumba wa mwanadamu anaeyajua matatizo yake yote. Na ndie aliyemshushia mfumo huu kwa utatuzi.

Mfumo wa Uislamu ndio hasa unaomfaa mwanadamu na wenye uwezo wa kumkomboa na kumrejeshea hadhi na thamani yake iliyofisidiwa na kupotezwa na mfumo wa ubepari leo duniani. Na pia ndio kila mwenye busara asiekuwa muislamu hupata hamu ya kuutafiti mfumo huu kwa kuepukana na propaganda na hatimae kuikiri itikadi(imani) yake, kuwa tayari kubeba ulinganizi wake ili mfumo huu usimame kiserikali na kueneza nuru yake ulimwenguni.

Mada iliyokuwa iwakilishwe kwenye kongamano la kukaribisha Ramadhani ambalo lilizuiwa na serikali.

 

Read 352 times Last modified on Friday, 02 June 2017 05:40
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…