Friday, 19 January 2018 00:00

Januari 1492 Mwisho Wa Utawala Wa Kiislam Hispania

Umma wa Kiislamu unakumbuka tukio la kuangushwa kwa ngome ya mwisho ya dola ya Kiislamu katika ardhi ya Hispania ndani ya mji wa Granada zaidi ya 500 iliyopita.  Kuanguka huko kukawa ndio kumalizika kwa kijisehemu cha utawala wa Kiislamu katika ardhi hiyo.  Sehemu hiyo ya dola  iliyokuwa ikiitwa kwa kiarabu Imarat Gharnāṭah/ utawala wa Granada ilianguka mnamo tarehe 2 Januari 1492 milladiya, baada ya kiongozi wa mwisho wa Grenada Muhammad XII kushindwa na kusalimu amri kwa utawala wa Ufalme wa Kikatoliki wa Ferdinand na Isabella("The Catholic Monarchs/ Los Reyes Católicos).

Uislamu uliingia ndani ya ardhi ya Hispania/Andalusia tangu 711 milladiya zama za Khilafah ya Umawiya pale Jemadari wa Kiislamu Tariq ibn Ziyad alipovuka bahari na kikosi cha askari wake kuingia katika rasi ya Iberia. Kuingia kwake ilikuwa baada ya raia wa eneo hilo ambalo kwa sasa linajulikana kama Hispania kumuomba Khalifa wa Waislamu wa wakati huo awakomboe kutoka kwenye makucha ya utawala dhalimu waliokuwa wakiishi chini yake wa Mfalme Roderick

Utawala wa Kiislamu katika ardhi ya Hispania ulipeleka nuru kwa watu wote wa Ulaya. Vyuo vya fani mbalimbali vilifunguliwa katika ardhi ya Hispania na kuifanya nchi hiyo kushamiri elimu na ustaarabu kiasi cha kusheheni wageni wengi kwa ajili ya kuja kupata maarifa mbalimbali. Uvumbuzi mbalimbali za kisayansi ulifanyika katika vituo vya kisayansi vilivyokuwepo katika ardhi hiyo.

Hispania ilipata maendeleo makubwa chini ya utawala wa Kiislamu. Pia ilirejesha utulivu na amani kwenye eneo  lililozeoeleka kwa mauaji kila kukicha. Aidha, iliondoa husuma sugu ya kimadhehebu baina ya wakiristo  iliyokuwa imeota mizizi  sio tu katika Hispania bali katika bara lote  la Ulaya kwa wakati huo.  Bila ya kutaja utawala wa Kiislamu ulivyoleta uadilifu  wa kijamii baina ya raia wakiwemo mayahudi waliokuwa wanaishi katika khofu na hali ngumu sana  chini ya mateso na dhulma kutoka kwa utawala wa kikatoliki.

Historia ya Uislamu ndani ya ardhi ya Hispania ni muhimu kwa Waislamu kuitambua kwa kina, huku wakijifunga na  uwajibu wa kuulingania Uislamu  ili siku moja inshaAllah ardhi hiyo irudi tena katika milki ya Waislamu chini ya dola ya Kiislamu ya Khilafah Rashidah

 Imeandikwa na Kaema Juma

Mwanachama wa Hizb ut-Tahrir Tanzania, Mwalimu, Mtafiti, Msomi katika tasnia ya habari, Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, kijamii na kihistoria pia ni Mwanaharakati wa kijamii.

Read 658 times
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…