Wednesday, 14 February 2018 00:00

Suluhisho La Malezi Ya Watoto

 

لِلَّهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ يَهَبُ لِمَنْ يَشَاءُ إِنَاثًا وَيَهَبُ لِمَنْ يَشَاءُ الذُّكُورَ

أَوْ يُزَوِّجُهُمْ ذُكْرَانًا وَإِنَاثًا وَيَجْعَلُ مَنْ يَشَاءُ عَقِيمًا إِنَّهُ عَلِيمٌ قَدِيرٌ

 Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu, anaumba apendavyo, anamtunikia amtakaye watoto wa kike, na anamtunikia amtakaye watoto wa kiume. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza’

(TMQ 42: 49-50)

Allah Ta’ala anatuzindua kwamba, mtoto ni miongoni mwa neema na tunu kubwa anayomtunikia kwa mja wake anaemtaka kwa Rehma zake. Kwa msingi huo suala la malezi ya mtoto huwa ni wajibu kwa lengo la kuitunza neema hiyo tukufu, ambayo lau itakosa malezi mazuri itakuwa kama shamba inayokosa matunzo ambayo kuuangamia kwake huwa ni jambo la kutarajiwa.

  Kwa hivyo, kumpa malezi mazuri mtoto huwa ni lazima kwanza, katika upande wa huduma za kimada (vitu vitu) kama chakula, nguo, matibabu nk. Lakini pia ni lazima kwa upande wa pili katika maadili, yanayofinyanga haiba/shakhsia (personality) ya mtoto kwa mustakbali wake na kwa Umma mzima.

 Leo kilio juu ya watoto kukosa malezi mazuri kinasikika kila pembe kutoka kwa wazee, wanajamii, wanasiasa na taasisi mbalimbali. Wote huungana juu ya suala moja tu, juu ya watoto wetu kukosa malezi mazuri kiasi cha watoto hao kugeuka ‘bomu la kutega’ dhidi yetu.

 Hata hivyo, tukiliangalia suala la malezi kwa upana wake tutagundua kwamba mtoto hukabiliwa na malezi ya aina mbili: Malezi ya wazee wa mtoto katika familia na malezi ya jamii kwa ujumla wake.

Malezi haya yote aina mbili ni yenye kutegemeana daima, na tukitaka tupate watoto wenye malezi mazuri ya kweli, basi tusiyatenganishe malezi haya kwa kuwa huu ndio uhalisia ulivyo.

 Tukiangalia kwa umakini zaidi tutaona kwamba, mtoto mara nyingi kama si zote, hujumuika zaidi na jamii hata kuliko na watu wake wa familia. Kwa mfano, mtoto huchukua muda mwingi kuwa shuleni, michezoni na pia madrassa, ukilinganisha na muda anaobakia na familia yake nyumbani.

  Hivyo ni wazi kwamba malezi ya jamii yanachukuwa sehemu kubwa na muhimu kwa maisha ya mtoto. Na sehemu hiyo hujenga athari muhimu kwa maisha yake kuliko malezi ya kifamilia. Japo kwamba kweli malezi ya familia nayo yana unyeti wa aina yake.

Ili kuweza kupatikana watoto wenye malezi mazuri kunategemea na jamii namna ilivyo, kwa maneno mengine, kutengenea kwa mujtamaa/jamii kimaadili ndiko kwa kiasi kikubwa kutengenea mtoto katika jamii husika. Na kinyume chake, kuharibika jamii ndio pia sababu kwa kiasi kikubwa kuharibika kwa watoto wetu.

Na kwa uhalisia maana ya ‘jamii/mujtamaa (society)   ni mjumuiko wa watu, fikra, hisia na nidhamu ya kimaisha inayoendesha maisha yao. Hii maana yake lau ndani a jamii watu wote wawe  Waislamu lakini wakawa wameathiriwa na fikra za kidemokrasia na nidhamu inayosimamia maisha yao si ya Kiislamu, hubakia watu hao kuwa Waislamu, lakini mujatamaa wao si wa Kiislamu.

 Leo Umma wetu wa Kiislamu tumesibiwa na uovu mkubwa wa kuishi katika mujtamaa/ jamii isiyokuwa ya Kiislamu, jambo ambalo hutuathiri katika malezi ya watoto wetu na Uislamu wetu kwa jumla.

 Utatuzi wa suala la malezi na mengineyo, licha ya sheria kututaka tujizatiti na malezi katika hali yoyote,  lakini kwa suluhisho la kudumu ni wajibu tujipinde tukiwa kama wazee kwa upande mmoja, na kama Waislamu kwa kwa upande mwengine, kurejesha tena jamii ya Kiislamu. Jamii itakayodhamini usalama wa malezi yetu ambayo yatasimama  juu ya vipimo vya Kiislamu pekee. Na jambo hilo litawezekana tu kwa kurejesha tena dola ya Kiislamu ya Khilafah.  

 Khatib Ali

                       

Read 1119 times
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…