Thursday, 23 February 2017 00:00

Ndoto za ‘Uhuru’ na ‘Mgawanyo wa Madaraka’

Written by 
Rate this item
(0 votes)

 

Habari:

Karibuni vyombo vya habari vimeripoti hatua ya serikali ya Tanzania kuzuiya TV ya TBC kupeperusha hewani moja kwa moja mikutano ya vikao vya Bunge kwa kisingizo cha gharama kubwa.

 Maoni:

Msimamo huu wa serikali umelaaniwa na kupata upinzani mkali kutoka kwa raia na taasisi mbalimbali nchini hususan zile zinazojinasibu na masuala ya utetezi wa  haki za binadamu. Qadhia hii inaonekana kuwa ni jaribio la serikali kuficha fedheha na madhambi yake ambayo katika serikali iliyopita yaliijeruhi serikali kwa kiasi kikubwa. 

Qadhia hii ni matusi, kejeli na kebehi kwa raia jumla. Pia ni dalili ya udhaifu, udikteta na woga wa serikali inayojinadi kujali raia. TBC ni taasisi ya Umma inayolengwa kuuhudumia Umma kwa kutumia kodi za wananchi.  Hali hiyo imejiri ilhali serikali hii ikijionesha  ati iko mstari wa mbele kutaka kuboresha huduma za jamii kwa raia na kupambana na uzembe. Cha kushangaza ! serikali hii ati imeshindwa kufahamu na kutambuwa kuwa miongoni mwa huduma msingi kwa raia ni kupata taarifa kwa wakati muwafaka hususan  za kisiasa na mwenendo  mzima wa serikali. Kisingizio cha gharama kubwa katika hili hakina uhalali. Kama vile ambavyo kimekosa uhalali katika utoaji wa huduma nyengine.

Tukio hili linafedhehi uwongo wa nidhamu ya kidemokrasia inayodai kudhamini kile kinachoitwa “uhuru wa maoni”. Bali kiukweli uhuru huu hupigiwa kampeni pale tu usipogongana na kuhatarisha maslahi ya serikali na wanasiasa. Lakini uhuru huo unapogongana na maslahi yao  hupigwa teke na kutupiliwa mbali, licha ya katiba zao kunadi kuwa ni haki msingi kwa raia kupata, kutafuta na kupashwa taarifa mbali mbali zinazogusa maisha yake.

Kwa upande mwengine,  tukio hili pia linaonesha wazi wazi kutokuwepo uhalisia wa ile dhana ya ‘mgawanyo wa madaraka’ na uhuru baina ya mihimili mitatu ya dola. Yaani serikali, Bunge na Mahkama. Dhana hiyo itabakia kuwa ndoto ya mchana tangu isiyo na uhalisia tangu ilipoasisiwa na mwanafikra wa Kifaransa Baron de Montesquieu mwaka 1748 hadi mwisho wa siku.

Tunashuhudia namna serikali inavyodhibiti harakati za Bunge kwa kuliwekea mipaka katika kuangaziwa shughuli zake katika Tv moja kwa moja.  Pia hata baada ya serikali kutoa msimamo huo bungeni, na kupata upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya wabunge, bado serikali haikusita, bali  ilimwaga askari polisi bungeni kudhibiti wabunge wa upinzani. Kitendo kilichokemewa vikali na wadau mbali mbali wa demokrasia kuwa ni uingiliaji kati na kulitisha Bunge lisifanye kazi zake ipasavyo. 

Kila mwanadamu makini anafahamu kuwa demokrasia imejengwa juu ya fikra za kindoto zisizo na uhalisia. Ndio maana ikawa chanzo cha mashaka na mabalaa tunayoyapata leo ulimwengu kote. Ubinadamu ni kitu kitukufu, hivyo unahitaji mfumo  mtukufu uliojengwa juu ya msingi wa kuwafikiana na uhalisia. Mfumo huo ni Uislamu pekee.

Read 356 times Last modified on Thursday, 23 February 2017 03:48
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…