Friday, 31 March 2017 00:00

Bila ya Khilafah ni Utumwa na Dhulma- 1

Written by 
Rate this item
(0 votes)

                                                         

Khutba ya Ijumaa 03 Rajab 1438 Hijri / 31 Machi 2017 Miladi

BILA YA KHILAFAH NI UTUMWA NA DHULMA- 1

 Alhamdullilah kwa Rehma za Mola wetu tumeingia tena ndani ya mwezi wa Rajab.  Mwezi mtukufu uliosheheni mengi ya kheri, lakini pia ndio mwezi ambao makafiri baada ya njama na mikakati ya muda mrefu walifanikiwa kuingusha dola ya Kiislamu ya mwisho ya Khilafah Uthmania. Tukio lililokhitimika  mwishoni mwa mwezi wa Rajab 1342  mwanzoni mwa Machi1924.

Kwa kuwa dola ya Khilafah ni nuru na ukombozi kwa Waislamu na walimwengu kwa jumla, hapana shaka muanguko wake umeacha athari, mashaka na maumivu kila mahala.  Kwa maneno mengine, kuangushwa Khilafah kumewarejesha wanadamu katika wimbi la dhulma na utumwa.  Dhulma kwa sura zake zote na utumwa wa kila aina, uwe wa kisiasa, kifikra, kiibada nk.

Kwa kuangushwa Khilafah Waislamu wamepata hasara kubwa kwa kukosa kutawaliwa kwa mujibu wa dini yao, jambo ambalo ni faradhi na ibada tukufu kwao. Na wasiokuwa Waislamu wamekula hasara kwa Uislamu kutotawala juu yao. Wamekosa kushuhudia haki, insafu na uadilifu wake na kuona tofauti baina ya tawala za mfumo wa kibepari zinazoongozwa kwa udikteta kwa jina demokrasia ambazo zimeitenga dini kando zikiongozwa kwa matakwa na sheria duni za mwanadamu anaefikiri kama wengine, kula chakula, kwenda haja na mwisho kufariki dunia. Mfumo wa kibepari na tawala zake ni miongoni mwa dhulma na utumwa mkubwa usiokuwa na mfano uliokuja kuangamiza baada ya kuangushwa Khilafah

Sababu ya kuzuka wimbi la kidemokrasia duniani na kuzuka mfumo wa kibepari ni kutokana vuguvugu la mapinduzi na mageuzi makubwa ya kisiasa ndani ya Ulaya baada ya nchi hizo kutawaliwa kwa muda mrefu na tawala za mabwanyenye waliomakinishwa na makasisi wa kanisa kwa kuhalalishwa kuwa ni chaguo la Mungu. Wanafikra na wanaharakati mbalimbali ndani ya Ulaya walianzisha kampeni ya karibu karne nzima kutaka mabadiliko ili kuwang’oa mabwanyenye hao na makasisi wao ili mamlaka yawe kwa raia, mabunge yao na kuunda tawala zinazoitwa za kidemokrasia kwa msingi wa usekula (dini kando na utawala).

Pamoja na mfumo wa kibepari na nidhamu yake ya kidemokrasia kudai kufanikiwa kuiondoa dini na ushawishi wa makasisi kando na utawala. Lakini kwa udhati ilichofanikiwa demokrasia ni kuleta nidhamu ya utumwa na dhulma kwa sura nyengine tu. Nidhamu ya kidemokrasia ni dhulma na  viongozi wake ni ‘miungu watu’ kwa sura nyengine badala ya makasisi waliokuwa wakihalalisha kwa jina la Mungu. Leo ulimwenguni kote ni kikundi cha watu ndio huweka na kuondoa sheria kwa maslahi ya mabepari, watawala na wapambe wao wakidai kuwakilisha matakwa ya wengi. Dhana ya Montesquieu ya mgawanyo wa mamlaka ya mihimili, uhuru wa mahkama, uhuru wa vyombo vya habari na kinachoitwa utawala wa sheria ni matamko kwa mujibu wa matakwa ya watawala ambao mara nyingi hulindwa na “kinga maalumu ya kutoshtakiwa” na kuungwa mkono na mabepari na wafuasi wa chama chake. Hii ni dhulma kubwa na utumwa usio na mithali inayowakabili wanadamu, Waislamu na wasiokuwa Waislamu.

Dola ya Kiislamu ya Khilafah inatawala kwa sharia za Kiislamu lakini sio dola ya ‘kiunguungu’ (Theocratic regime) ikiwa na maana kwamba mtawala wake upo uwezekano wa kukosea na kutenda dhambi kwa kuwa ni mwanadamu. Na ndio maana Khalifah wa pili Abubakar Ra baada ya kuchaguliwa aliwakhutubia Waislamu kwa kusema: “…..Nimechaguliwa kuwaongoza lakini mimi si mbora wenu, nikiongoza vyema nisaidieni na nikikosea ninyoosheni….” Khalifah hulazimu achungwe katika maneno na matendo yake, akikosea akosolewe na ikibidi hata kuwajibishwa kwa kuondoshwa.  Khalifah anapotawala kwa sheria za Kiislamu huwa ni mtekelezaji wa sheria hizo kama alivyo Muislamu mwengine yoyote, kamwe hana hadhi wala kinga mbele ya sharia na wala hana haki ya kutumia ngazi ya utawala kuwalinda wapambe, ndugu au marafiki zake kwa namna yoyote. Itakumbukwa Khalifah Abu Abakar Ra. alipoletewa shauri (kesi) ya sahaba mkubwa wa Mtume SAAW, msaidizi na mshauri wake aliyekuja kuwa Khalifah baada yake (Umar al-Khattab), shauri  hilo lilikuwa juu ya nani mwenye mamlaka ya kumlea mtoto baina ya Umar na mke aliyeachana nae. Khalifah Abu bakar alitoa hukmu ya shauri hilo dhidi ya Umar bila ya kujali nafasi ya Umar, hadhi wala nafasi yake, bali alichojali ni haki kwa mujibu wa Uislamu na sheria zake. Katika hukmu hiyo Abubakar alitamka maneno ya kihistoria kwa kusema: “Ewe Umar  kwa mtoto huyu  kufyonza mate ya mama yake (akiwa kwa mama yake)  ni bora kuliko asali utakayompatia wewe (chini ya malezi yako)”

Uislamu umeweka utaratibu wa kisheria kuhakikisha Khalifah halewi madaraka hapandi kibri na jeuri ya kudhulumu raia katika utendaji wake. Umemuwajibishia kiongozi kuwa mchamungu kama Waislamu wengine. Yaani jukumu lake la utawala na kuwatumikia raia yumo ndani ya ibada ambayo atahisabiwa Siku ya Kiama kwa mujibu atakavyolibeba. Aidha, umefaradhisha kwa Waislamu wote jukumu la kuamrisha mema na kukataza maovu likihusisha pia kwa watawala. Ikiwa na maana kuwa Waislamu wote wawe wanasiasa wakati wote na sio kwa msimu fulani kufahamu namna nchi inavyoendeshwa katika miamala yake mbalimbali ili kiongozi na watendaji wake wakikosea wakosolewe. Pia Umma huchagua chombo maalumu kinachowawakilisha (Majlis Umma) ambacho miongoni mwa kazi zake ni kuichunga serikali na watawala wasimame juu ya mstari wakati wote.  Pia Uislamu umeweka mahkama maalumu inayoitwa mahkama l- madhalimu ambayo kazi na jukumu lake pekee ni kumuangalia kwa umakini mkubwa Khalifa, wasaidizi wake na watumishi wote wa Umma namna wanavyoyasimamia na kuyaendesha mambo bila ya kulindana, kudhulumu au kutumia madaraka yao vibaya. Mahkama hii licha ya kuwa kiongozi wake kuteuliwa na Khalifah, lakini haki ya Khalifah kutengua uteuzi wake hubatilika pale Qadhi huyu anapochunguza shauri/kesi miongoni mwa mashauri dhidi ya Khalifah, wasaidizi wake au yoyote miongoni mwa watendaji wake mpaka atakapomaliza. Na kamwe mahkama hii haisubiri watu kupeleka malalamiko rasmi bali huanza uchunguzi mara moja inapopata namna fulani ya fununu ya kuwepo dhulma.

Enyi Waislamu na wanadamu kwa jumla, huu ndio utawala wa Khilafah  ambao leo Waislamu na wanadamu kwa jumla  wanauhitaji uje kuwaokoa na dhulma na utumwa mambo leo kwa jina la demokrasia,  huku watawala wake wakilewa madaraka, kulinda maswahibu zao  na kutumia nguvu na mabavu katika kumakinisha matakwa yao.

 

http://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Read 1855 times Last modified on Friday, 31 March 2017 13:33
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…