Tuesday, 06 June 2017 00:00

Tujikurubishe zaidi kwa Allah kwa ibada yetu tukufu ya Ramadhani

Hisia ya kukiri utambuzi wa kutambua kuwepo Allah Ta’ala ni jambo la kimaumbile kwa wanadamu wote katika zama zote tangu aumbwe mwanadamu wa mwanzo. Na hali hiyo itaendelea kuwemo ndani ya  mwanaadamu wakati wote licha ya kushamiri harakati mbalimbali zinazoitwa za ‘kimaendeleo’ za kupinga suala zima la dini kwa kisingizio cha ‘kutosheleza sayansi na teknologia’

Hisia hii ni ile hali ya kumkereketa mwanadamu ndani ya nafsi yake na kuhisi moja kwa moja kuwepo Muumba wa ulimwengu na Muumba wa viumbe vyengine ikiwemo yeye mwenyewe . Muumba ambaye ana mamlaka yasiyo na mipaka juu ya mwanaadamu na alivyovizunguka mwanadamu.

Dhihirisho la hisia hii humpitikia mwanadamu kwa kuhisi na kuona waziwazi udhaifu alionao kimaumbile, kwa kuingiliwa katika mambo yake na mipango yake licha ya kujipanga vyema na  kujiwekea mikakati kabambe  lakini ghafla hupanguka    huupoteza kazi  mali  watoto  hishma  na hatimaye huumwa mwanaadamu huyu mpaka  kufa. Yote haya humpa mwanaadamu utambuzi wa ndani juu ya udhaifu wake na kukiri kuwepo Allah Ta’ala, Mwenye nguvu, Mamlaka na Uwezo usio na mipaka. Na hii ndio maana ya ‘Fitra (maumbile)

Hata hivyo, baadhi ya wanaadamu huonekana kwa nje kutokana na kibri na majivuno kuukana ukweli wa kuwepo Muumba, lakini jambo hili ndani ya nafsi zao kwa ndani haliwezi kupingika. Na kimsingi huwa ni kujidaganya tu kwa nje mbele ya macho ya watu.

Anatusimulia Taala kuhusu Fir-aun na kaumu yake:

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنْفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ:

Na wakazikataa (aya zetu) kwa dhulma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi zao zina yaqini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa mafisadi ! (Tmq 27:14)

Kadhalika Khalifah wa nne, Imam Ali RA. anasema:

‘Allah ana hoja mbili kwa wanaadamu. Hoja ya nje (Dhwaahirah) na hoja ya ndani (Baatwinah). Hoja ya nje ni Mitume na Manabii na hoja ya ndani ni akili’

Darwin muasisi na mwanadharia wa nadharia ya ‘evolution’ inayonasibisha chanzo cha mwanaadamu ati ni sokwe, aliwahi kuulizwa alipokuwa mahtuti kitandani siku chache kabla ya kifo chake. Anaonaje kuhusu maumbile mazuri ya vitu mbali mbali inawezekana kazi ya kutengeneza vitu hivyo ni kazi ya akili ya mwanaadamu na kweli si kazi ya Mungu?

Darwin akamkodolea macho Duke of Argyle kwa makini na akamjibu:

‘Hali hiyo ya (kuwepo Mungu) imekuwa daima ikinipitikia kwa nguvu kubwa, lakini wakati mwengine ilikuwa kana kwamba ikiniondokea’ (Hayward.Alan, God Is, uk.113)   

Baada ya mwanaadamu kudiriki utambuzi huu wa kuwepo Allah Ta’ala huwa hana budi kuhitaji aina fulani ya ibada ili kuonyesha utiifu na unyenyekevu kwa Muumba wake anayeyatawala maisha yake. Na kutokana na ukweli huu ndio maana katika zama zote mwanaadamu amekuwa akijifanyia aina mbali mbali za ibada kudhihirisha utiifu na unyenyekevu wake kwa Mungu anaemuabudu. Hali hii ilikuwa ikidhihirika hata katika zama za vitisho, ubabe na mabavu ya mfumo batil wa Ukomonisti uliokuwa mpinzani mkubwa wa dini. Lakini kubwa uliloweza kufanya mfumo  huo ni kuwaondoa raia wao kutoka katika ibada zao za zamani na badala yake kuwapeleka katika ibada mpya ya kuyasujudia masanamu ya viongozi wa kikommunisti. Kwa hivyo kwa udhati Ukomunisti ulishindwa kuzuia dhana ya kimaumbile ya ibada kwa watu wao bali ulichoweza ni kubadilishia aina ya ibada na si zaidi ya hilo. Yaani  waache kumuhishimu Mungu muumba  na badala yake  wakahishimu  waasisi wa fikra za komonisti

Kutokana na hitajio la kimaumbile la mwanaadamu juu ya ibada ya Alaah Taala, zama zote Allah amekuwa akituma Mitume AS. Kwanza, kwa lengo la kuwafafanulia wanaadamu sifa zake kwa ufafanuzi na upana wake ili sifa hizo asipewe mwengine au kupewa sifa zisizokuwa zake. Pili, kuwafahamisha wanaadamu masuluhisho ya matatizo yao yote maishani mwao. Na mwisho,  kuwafundisha aina ya ibada sahihi ili mwanaadamu apate utulivu kwa kumnyeyekea Mola wake na kukidhi kiu yake ya kimaumbile  ya kumuabudu Muumba wake.

Kwa mnasaba huu ndio maana Mtume wetu Muhammad SAAW ambae ni Mtume wa mwisho akapewa aina mbali mbali za ibada kama Swala, Hijja, Saumu nk. Ili kutokana na ibada hizo tuonyeshe unyenyekevu wetu kwa Muumba wetu Allah Taala na tutosheleze kiu yetu ya kimaumbile ya kumuabudu Muumba wetu.

Kwa hivyo, kwa Rehma za Allah na Utukufu Wake ametupa ibada  aina mbali mbali ili tuweze  kukata kiu yetu hiyo ya kuhisi kuwepo kwa  Mungu muumba  na  swaumu  hii tukufu  ya Ramadhani ikiwa ni moja ya ibada adhimu aliyotuletea ili tupate ladha ya unyekekevu na nyoyo zetu zipate utulivu kwa kumuabudu yeye Mola wetu pekee  na kukata kiu hiyo

 

Tukasisitizwa kushikamana na ibada hii kutoka  kwa Abu Huraira, aliposema Mtume SAAW: ‘Inapoingia Ramadhani Milango ya mbingu (pepo) hufunguliwa, na milango ya Jahannam hufungwa, na mashetwani hufungwa minyororo.           (Bukhari)

Akasimulia tena Abu Huraira kwamba Mtume SAAW, anasema:

‘Ameangamia ambae ninapotajwa mbele yake hakuniswalia, na ameangamia ambae amefikiwa na Ramadhani na ikamalizika kabla ya kusamehewa dhambi (zake), na ameangamia ambae amewadiriki wazazi wake wawili katika uzee wao na hakuingia peponi.’

(Ahmad, Tirmidh , Ibn Huzayma na Hakiim)

Kwa hivyo, tuingieni katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kwa kujizatiti kufunga na kufanya

kila aina ya ibada ndani yake ili kujikurubisha Kwake kwa dhamira moja tu ya kustawisha fungamano letu na Mola wetu  ili tukate kiu hiyo ya kimaumbile ya kuhisi kuwepo kwa ALLAH na kupa akili haki yake  kwani  nayo inakiri uwepo wa MUngu muumba  na ibada hii isiwe ni kwa ajili ya pupa ya vyakula vitamu  kwa  wale  wenye kuvipata wala maslahi mengine yoyote ya kidunia   kama zinavyo  sambazwa dhana  za kiafaya  katika ibada hii  bali iwe ni kwa kutafuta radhi za Allah Taala huku tukitaraji Pepo yake na kuogopa Moto wake.

 

وَأَنْ تَصُومُوا خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

                           ‘Na mkifunga ni kheri kwenu ikiwa mnajua’ (Tmq 2:184)

Read 790 times
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…