Saturday, 24 June 2017 00:00

Tunaiaga Ramadhani na kuikaribisha Eid el Fitr ilhali Ummah wa kiislam bado una majanga

 

بسم الله الرحمن الرحيم

 Kwa sifa njema za Allah na neema zake mwaka huu Waislamu wengi kama si wote wameungana kuanza kufunga Ramadhani kwa pamoja. Jambo hili linalonesha kwamba  kufunga na kufungua kwa Eid kwa pamoja ni jambo linalowezekana lau watakuwa chini ya usimamizi wa dola ya Khilafah Rashidah ambayo itasimamia na kuchunga mambo yao                                                                                                

Waislamu tumefunga mchana na kusimama usiku wake, tukatoa sadaka kwa wingi, tukajikurubisha kwa Allah SW kwa kusoma Quran, tukanyenyekea kwake kwa dua, tukasaidiana katika wema na uchamungu, tukafutarishana kwa hali ya huruma na upendo. Jambo tunaloweza kusema halipatikani kwa wasiokuwa Ummah wa Kiislamu.                                                                                                             

Hakika mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi ulioteremshwa Quran ndani yake ili iwe uongozi kwa watu katika maisha yao, Allah (swt) anasema: Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Quran kuwa ni uongozi kwa watu na ubainifu wa uongozi na upambanuzi”.

 Kutokana na Quran Waislamu wakawa na nguvu, maendeleo na mwamko katika nyanja mbalimbali za maisha: kifikra, kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutawala nk. Sambamba na Waislamu kujifunga na nyumba za ibada Waislamu pia walikua majemedari washupavu katika uwanja wa vita. Kwahiyo wakaubeba Uislamu kwa jihadi na wakaifungua miji,  na Mwenyezi Mungu akawaongoa watu kwa sababu yao, na dunia ikawa na amani chini ya utawala wa Kiislamu  

 

Na pale utawala wa Kiislamu ulipotoweka katika dunia hii na kushika hatamu ubepari, ukaenea uharibifu na ufisadi bara na baharini, watawala waovu, umasikini wa kutupwa, maradhi ya hatari, jeuri, ubabe, rushwa iliyotapakaa, uporaji wa raslimali nk… Kwa hakika ulimwengu umesheheni kila aina ya viza na dhulma…

Na hivi ndivyo unavyomalizika mwezi wa funga, huku ukishuhudia majanga ya Ummah wa Kiislamu na majeraha yake. Ndani ya Tanzania Waislamu wanaswekwa ndani ya majela na maselo kwa kisingizio cha ugaidi bila kuhukumiwa, mauji holela ya raia wasio na hatia hasa katika Ukanda wa Pwani. Bila ya kutaja dhulma za mauaji ya Waislamu yanayoendelea kimataifa nchni Somali, Iraq, Libya, Syria, Yemen, Afrika ya Kati, Burma, na miji mbalimbali ikiwa katika madhila na tabu zisizoelezeka..EnyI ndugu hivi kweli inakubalika  Ramadhani itujilie na ituondokee nasi tumo katika hali hizi mbaya?!

 

Tukiwa tunaiaga Ramadhani, tunamuomba Allah (SWT) azikubali funga zetu, visimamo vyetu, na kutusamehe madhambi yetu.  Aidha, wakati tunaikaribisha Eid el Fitr, licha ya macho yetu kuangazia mayatima, mafakiri na masikini ili kuwafariji na kuingiza furaha nyoyoni mwao, pia tuwe na hima ya kutekeleza wajibu tuliowajibishwa na Allah Sw kuhukumu kwa sharia yake katika maisha yetu na kubeba risala ya Uislamu kwa walimwengu ili kurejesha amani na utulivu kwa ulimwengu huu uliogubikwa na hali mbaya isiyo na mfano. Inafaa  tukumbuke  kauli na maana ya kauli ya Allah Mtukufu aliposema: “Na yeyote mwenye kupuuza ukumbusho wangu basi huyo ana maisha ya dhiki na tutamfufua siku ya Qiyama kipofu”

 

Mwisho, kwa heshima na taadhima kubwa tunatanguliza mkono wa Eid kwa Waislamu wote duniani, siku kuu itakayoingia siku chache zijazo InshaAllah. Tunamuomba Allah SW aijalie iwe bishara ya kheri kwa Ummah wa Kiislamu.      Amiin

                                                             

Hizb ut –Tahrir Tanzania

28 Ramadhan 1438 AH     23/06/2017

Read 530 times

Media

Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…