Thursday, 27 July 2017 00:00

Tatizo la Mimba kwa Wanafunzi limekosa Suluhisho Thabiti

Idadi ya wasichana wenye kupata mimba wakiwa bado wanafunzi ima katika shule za msingi au sekondari inazidi kuongezeka siku hadi siku. Kwa hapa Tanzania kwa mujibu wa Ripoti ya mwaka 2016 ya Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu (Human Rights Watch) zaidi ya asilimia 40 ya wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo ya sekondari husababishwa na sababu kadhaa ikiwemo “mimba za utotoni”. http://www.mwananchi.co.tz/Serikali-isiwatupe-waliopata-mimba-shuleni/1596774-3814982-ncx5yp/index.html

 Hali hiyo sio hapa Tanzania pekee, bali kila mahali ambapo mfumo wa kidemokrasia umejikita barabara na kushtadi fikra yake ya “uhuru wa kibinifsi” inayowasukuma raia kufanya kila aina ya uchafu. Mathalani Ulaya na Marekani masuala hayo mpaka yamekuwa ni ya kawaida.

 Suala la mimba za wanafunzi limezuwa mjadala mkubwa hapa Tanzania hususan karibuni kufuatia kauli ya Raisi iliyon’gang’ania msimamo wa kutowaruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea na masomo katika shule za Umma. Huku kwa upande wa wanaharakati wanaotetea haki za mtoto wa kike wanashinikiza serikali kuwaruhusu wanafunzi hao kuendelea na masomo.

 Qadhia hii hutizamwa kwa ufinyu na sio katika msingi na upana wake, kama chanzo cha tatizo, nafasi ya elimu, nani wa kuwajibika nk. Bali wadau wanazunguuka hapo kwa hapo kwa kujadili  kijtawi tu cha tatizo na matokeo yake. Yaani qadhia imebakia katika kuruhusiwa au kutoruhusiwa wanafunzi hao kuendelea na masomo mashuleni.

Kimsingi serikali na wanaoitwa wanaharakati wote wanaogelea katika dimbwi moja la maji machafu- kwa kuwa tatizo limezaliwa na mfumo wa kidemokrasia ambao fikra zake hatari ndizo zilizoleta naqama hii katika jamii. Kwa hivyo, haiwezekani suluhisho likatokana na dimbwi hilo hilo lililozaa tatizo.

 Udhaifu mkubwa wa mfumo huo ni kukipima kila kitu katika upande wa kimaslahi. Hivyo, ni wazi wabebaji fikra zinazotokana na mfumo huo huyatazama mambo katika kipimo hicho hicho pamoja na msukumo wa kujipatia kiwango kikubwa cha starehe. Na kwa hiyo kila jambo huendeshwa ili kuyafikia haya.

 Uislamu chini ya dola yake ya Khilafah Rashidah italifanya tatizo hilo na mengineyo kuwa historia kwa kuchukua hatua thabiti zenye kugusa roho ya tatizo na sio matawi ya tatizo.

Kwanza, serikali ya Khilafah itawafinyanga raia wake kwa thaqafah ya Kiislamu inayokataza uzinifu na kila chenye kuchochea uchafu huo. Mathalan, serikali haitaruhu chochote chenye kuchochea zinaa kama mikusanyiko holela baina ya wanawake na wanaume, miziki, madanguro,  kutembea uchi,  zinazoitwa kumbi za starehe nk.

 Aidha, katika serikali ya Khilafah wasichana watafundishwa na walimu wanawake, na shule za wavulana walimu wao watakuwa wanaume. Vilevile wanafunzi waliobaleghe watatenganishwa na wale ambao hawajabaleghe.

 Khilafah itahamasisha ndoa ili kuziba mwanya wa kushibisha matamanio kwa njia za kiholela na haramu. Katika kulifikia hilo itaweka mazingira mwanana hususan ya kiuchumi ili wanaume wamudu kubeba majukumu ya kifamilia zao.  Leo kwa  masikitiko makubwa chini ya mfumo batil wa kidemokrasia/ubepari unaotawala leo suala la ndoa unalidharau na kuonesha kama ni kipingamizi cha masomo ya wanafunzi na ati wanafunzi hao bado watoto wadogo. Cha kushangaza mfumo huu hauna mipango wala mikakati thabiti ya kumlinda na zinaa mwanafunzi huyo. Na wala hawana majibu thabiti wanapohojiwa  jee kama  wanafunzi hao watoto, mbona wanajihusisha na mambo ya wakubwa.

 Khilafah itawajenga raia watende yaliyo ya halali na kujiepusha na ya haramu kwa msingi wa uchamungu. Yaani  lengo  ni kutafuta radhi za Allah Taa'la pekee.  Hivyo, katika hali hiyo inatarajiwa raia wataishi hapa duniani ilhali fikra zao zikiitizama pepo ambayo upana wake ni upana wa mbingu na ardhi iliyoandaliwa wachamungu.

Lakini pale raia hao watapokengeuka na kujitumbukiza katika uchafu kama zinaa na mwengineo, Uislamu chini ya nidhamu yake ya kuadhibu tayari imeweka adhabu mbali mbali. Serikali ya Khilafah itatekeleza adhabu kwa wazinifu ili iwe fundisho kwa wengine. Na kamwe serikali haitabwaga jukumu lake la kuwasomesha raia wake bali wataadhibiwa kwa mujibu wa makosa yao, baada ya adhabu hiyo hawatonyimwa haki yao ya kupata elimu.

 Bila ya kusahau Khilafah kukabiliana na suala nyeti la umaskini. Baadhi ya tafiti zinaonyesha kwamba wanafunzi wengi wanaopata ujauzito wanatoka katika familia masikini. Na umasikini ni tatizo linalotengenezwa na kuhamasishwa na mfumo wa kibepari licha ya kuwa Allah Taala kujaalia rasilimali na utajiri mkubwa katika ulimwengu tunaoishi.

 Chini ya mfumo wa ubepari rasilmali zimekusanywa kwenye mikono ya wachache. Hivyo, serikali ya Khilafah itahakikisha utajiri unawaenea raia wake wote kwa kutabikisha nidhamu thabiti ya kiuchumi iliyofafanua aina za umiliki. Yaani mali za kibinafsi, mali za Umma na mali za serikali bila ya kuingiliana na  kuleta dhulma ya mmoja kupora milki ya mwengine, kinyume na hali tuliyonayo leo ambapo mali za Umma kama maadini, mafuta nk. humilikishwa watu binafsi na kuubakisha Umma jumla katika dimbwi la umasikini wa kutupwa. Au mali kama hizo kumilikiwa na serikali ilhali jukumu la serikali ni kusimamia mchakato wa uvunwaji wake na uuzwaji wake tu kisha faida irudi kuwanufaisha Ummah mzima. Leo nani asiyeona wazi wazi namna serikali za kidemokrasia chini ya fikra chafu ya ‘soko huria’ inavyowakabidhi wezi wanaoitwa wawekezaji utajiri wa Umma kisha wakiridhika kupata mirahaba duni na kutoa muhanga maisha ya raia jumla.  Kisha wanasiasa hao hao ndio hupaza sauti bila ya aibu wala haya kwamba nchi bila ya misaada haiwezi kwenda.

 Ulimwengu unahitaji mfumo wa Kiislamu chini ya dola ya Khilafah ili kuukomboa na mashaka mbali mbali ikiwemo mimba nje ya ndoa, dhulma za kiuchumi nk.

 

Imeandikwa na Ramadhan Said Njera

Mjumbe wa Afisi ya Habari -

Hizb ut- Tahrir Tanzania

 

 

04 Dhu al-Qi'dah 1438 Hijri | 27/07/ 2017 Miladi

http://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Read 766 times
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…