Friday, 12 January 2018 00:00

Vituko Vya Demokrasia na Wanasiasa wake

Ziara ya ikulu na matamshi ya Edward Lowassa, Waziri mkuu mstaafu na mjumbe wa kamati kuu ya Chadema kuusifia utawala wa Raisi Magufuli hapana shaka limeshangaza wengi katika wafuatiliaji wa siasa za Tanzania.

Mshangao huliibuka kwa kuwa asili Chadema ni chama cha Uingereza kama ulivyo Muungano wa Jubilee Kenya. Hivyo, mgongano wake na CCM ambacho ni chama cha Marekani daima hutarajiwa kuwa mkubwa. Kwa kuwa Marekani ambae ndie bwana wa Tanzania kwa sasa inajizatiti kuhifadhi ubwana wake usimtoke ili iendelee kunyonya rasilmali, ilhali Uingereza, bwana wa zamani ina shauku kubwa kuirejesha tena Tanzania, ngome yake ya kihistoria.

Karibuni tulishuhudia Maalim Seif Sharrif kutoa matamshi yanayofanana na ya Lowassa kusifia utawala wa Raisi Magufuli, lakini hilo halikutushangaza, kwa kuwa asili chama cha CUF ni chama cha Marekani, yaani vyama vya CCM na CUF viko chini ya bwana mmoja, na migongano yao huwa ni maslahi ya ndani. Ndio maana Marekani hakuwaacha mkono CUF, kaipatia nafasi ya kudumu kikatiba kuwa mshirika katika serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar.

Matamshi ya Lowassa yamezalisha mtaji mkubwa wa kisiasa kwa CCM na yamekitosa kisiasa kwa kiasi fulani chama cha Chadema, hata isemwe kuwa ni matamshi yake kibinafsi au Chadema itengeneze kisingizio cha kulazimisha na kusema kumtetea, lakini kwa nafasi na haiba ya Lowassa ndani ya Chadema na kwa muda huu, matamshi yake yana tafsiri ya madhara makubwa kisiasa na lau hayakutendwa kwa makusudi basi ni uzuzu wa hali ya juu kisiasa.

Aidha, matamshi hayo yamekuja wakati ambao upepo wa kisiasa uko upande wa Chadema na ukiwa dhidi ya CCM, kwa Chadema kuibana na kuifedhehi CCM na serikali yake ndani na kimataifa kufuatia hotuba ya karibuni ya Mbunge Tundu Lissu. Hotuba iliyokuwa msumari wa moto katika jeraha la CCM na serikali yake baada ya kauli ya Askofu Kakobe iliyowavua nguo.

Maswala kadhaa yanaweza kuibuka kufuatia qadhia hii hususan matamshi ya Lowassa. Jee katenda yale kwa msukumo gani? khofu ya maslahi yake kuwa hatarini, kabadilika na anaandaa mazingira ya kurudi CCM, maamuzi dhaifu ya chama chake, upeo duni wa kisiasa nk.

Katika hilo viwe viwavyo, katika demokrasia hakuna cha kushangaza, kwa kuwa ni mfumo uliojengwa juu ya msingi wa vituko na fikra ya kushangaza ya ‘usekula’ ambayo humuekea mipaka Mungu Muumba katika mamlaka yake ? Basi ikiwa msingi wa siasa hizo ni vituko, tutegemee nini ?

Zaidi ya hayo, demokrasia ni nidhamu yenye kipimo cha hatari katika matendo, nacho ni ‘maslahi’. Yaani mtu hutenda jambo au huacha kutenda ikiwa kuna maslahi. Kwa hilo pekee yatosha kwa mtu makini na mwenye nia njema kujiepusha na mchakato wa kidemokrasia.  Si ajabu kwa mwanademokrasia awe kiongozi au mwengine yoyote kutenda lolote litakalodhamini maslahi yake. Kwa kuwa uwepo wa mwanasiasa au kiongozi huyo ndani ya mchakato wa siasa hizo ni kutafuta hayo maslahi. Hivyo, ni jambo la kawaida kuuza hata kinachoitwa misimamo ya kisiasa kufikia malengo ya kimaslahi. Ni vipi mwanasiasa huyo kama kuna fursa ya kudhamini au kulinda maslahi yake aiwache?

 Pia nidhamu ya kidemokrasia inashikilia fikra za Machieveli zinazohubiri msimamo usemao: ‘njia yoyote ni halali ikiwa itakufikisha kwenye lengo’. Katika demokrasia na waumini wake wanaweza kutenda chochote hata kiwe na madhara kiasi gani ili kufikia wanakodhamiria. 

Kwa maumbile ya demokrasia tuliyotaja, ni wazi nidhamu hiyo ni tete, imekosa nishati, haina msimamo na iko mbali na kujitolea muhanga, licha ya wanasiasa na waumini wake kudai kuwa wana msimamo na wanatoa muhanga.

Muhanga wa kweli ni uliojengwa juu ya msingi thabiti wa kiroho, kitu ambacho hakipo ndani ya demokrasia. Demokrasia imeitupilia mbali thamani hiyo ya kiroho na wameifanya dini ni kitu duni kiasi cha kudai Uungu unamalizia makanisani au misikitini. Maana ya muhanga ni kutoa kila chako kuanzia muda, mali hata uhai kwa lengo unalokusudia kufikia. Katika demokrasia hata kama hudai kutoa muhanga, jambo hilo sio kweli, kwa sababau muhanga na maslahi ni vitu visivyowiva chungu kimoja.

Hata pale unapoona mwanademokrasia kana kwamba anatoa muhanga ni kwa lengo la kupata maslahi yake zaidi na sio kuwatumikia watu.  Na wengine hujifanya kutoa muhanga kwa muda mfupi, na mara wakiona hakuna muelekeo wa wanalokusudia hurudi nyuma. Na kimsingi hawana budi kurudi nyuma, kwa kuwa muhanga wa kweli lazima ufungamane na thamani ya kiroho na maisha yajayo ya akhera. Kwa vile katika maisha haya mafupi ya dunia unaweza kupoteza kila kitu bila ya kupata malengo unayokusudia.

Demokrasia ni nidhamu muflis na imeivurumisha mbali thamani ya kiroho yenye kuweza kudhamini kikweli dhana ya muhanga. Allah SW anatukumbusha juu ya muhanga wa waumini waliomuamini Nabii Mussa As. ambapo mwanzo walikuwa makafiri na wachawi wa Fir aun, baada ya kumuamini Nabii Mussa As., Firaun aliwatisha kwa mateso na kuwauwa, lakini walisimama na msimamo thabiti wa muhanga wakifungamanisha muhanga wao na  maisha yajayo ya  kudumu ya akhera:

قَالَ آمَنْتُمْ لَهُ قَبْلَ أَنْ آذَنَ لَكُمْ إِنَّهُ لَكَبِيرُكُمْ الَّذِي عَلَّمَكُمْ السِّحْرَ فَلَسَوْفَ تَعْلَمُونَ لَأُقَطِّعَنَّ أَيْدِيَكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ مِنْ خِلاَفٍ وَلَأُصَلِّبَنَّكُمْ أَجْمَعِينَ (الشعراء: 49).

قَالُوا لاَ ضَيْرَ إِنَّا إِلَى رَبِّنَا مُنْقَلِبُونَ (الشعراء: 50).

“(Fir-aun) akasema: Jee mmemuamini Mussa kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye ndie mkubwa wenu aliyekufunzeni uchawi. Na hivi punde mtajua! Nitakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakupachikeni juu misalabani nyote.”

“Wakasema haidhuru, (potelea mbali) kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu” (26: 49-50)

Kwa ndugu zetu Waislamu wanaotetea kimakosa nidhamu ya kidemokrasia wajionee zaidi uovu wake kwa matukio kama haya yasiokwisha, licha ya kuwa msingi na sheria zake ni ubatil wa wazi. Basi haujafika muda kwao kuufanyia kazi ya kuurejesha mfumo wetu wa haki wa Uislamu?  Na kwa wasiokuwa Waislamu umefika muda kwao kutafiti mfumo wa Kiislamu, kisha kujitenga na ubepari mfumo  muovu, dhaifu na tete ambao wafuasi huona kana kwamba wameshikilia kitu imara kumbe ni udanganyifu.

مَثَلُ الَّذِينَ اتَّخَذُوا مِنْ دُونِ اللَّهِ أَوْلِيَاءَ كَمَثَلِ الْعَنكَبُوتِ اتَّخَذَتْ بَيْتًا وَإِنَّ أَوْهَنَ الْبُيُوتِ لَبَيْتُ الْعَنْكَبُوتِ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ (العنكبوت41  : .

 “Mfano wa waliowafanya walinzi (wasimamizi wa mambo yao ) badala ya Mwenyezi Mungu ni mfano wa buibui anavyojifanyia nyumba.  Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote  ni nyumba ya buibui laiti wangelijua “ (29: 41)

 

 

Afisi ya Habari -   Hizb ut- Tahrir Tanzania

25 Rabi' al-thani 1439 Hijri -   12/01/ 2018 Miladi

 

                           http://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Read 370 times
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…