Monday, 12 February 2018 00:00

Ndoa Haitenganishwi na Dola

Written by 
Rate this item
(1 Vote)

Fikra batil ya ilmania/usekula ya kutenganisha baina ya dini na siasa ambayo ndio itikadi msingi ya mfumo wa kibepari imeathiri sana hata kwa baadhi ya Waislamu, kiasi cha baadhi kudhani kuwa Uislamu hauna nidhamu toshelezi ya kisiasa na usimamizi kwa maisha ya mwanadamu.  Jambo hilo si sawa. Uislamu una nidhamu kamili ya kisiasa kuyasimamia na kuyachunga mambo ya Umma, na kamwe haugawi baina ya dini na siasa.

 Leo tunashuhudia juhudi kubwa za Waislamu katika kunusuru, kutoa maelekezo na ushauri nasaha juu ya masuala ya ndoa. Iwe katika taasisi, mitandao ya jamii, mihadhara nk. Hata hivyo, mara nyingi jitihada hizo ambazo husaidia, hukosa kuiwasilisha taasisi ya ndoa kuwa inahitaji usimamizi wa moja kwa moja wa dola na utawala wa Kiislamu.  Japo ni kweli ndoa ni suala la kibinafsi na inaweza kufungwa pakiwa na Khilafa au la, lakini upeo wa kufanikiwa kwake kunahitaji usimamizi kamili wa dola ya Kiislamu ya Khilafah. Ni vipi utaitenga ndoa kando na utawala, ilhali dola ndio msimamizi wa kisheria katika kila nyanja kuanzia uchumi, siasa na masuala yote ya kijamii ikiwemo ndani yake suala la ndoa.

 Mtume SAAW alikuwa mtawala, akishikilia cheo cha kiongozi mkuu wa dola, amiri jeshi pia alikuwa akitatua migogoro mbali mbali kwa kutoa hukmu kwa kulazimisha kwa nguvu kiutekelezaji, ikiwemo migogoro ya ndoa. Na wakati mwengine akiteuwa maqadhi kwa ajili ya kubeba majukumu ya utoaji hukmu. Waislamu wa zama hizo walimfahamu Mtume SAAW kwa mtazamo sahihi kuwa ni Nabii na mtawala, ndio maana katika migogoro yao yote walikuwa wakimkabili awatatulie, na wakinyenyekea upeo wa kunyenyekea kwa hukmu alizokuwa akizitoa.

 Mtume SAAW kamwe hakuitenga ndoa kuwa ni kitu kando na usimamizi wa dola. Bali akiwa mtawala aliitatua migogoro ya ndoa kwa utatuzi wa hukmu thabiti ili kuilinda taasisi hiyo ambayo kufanikiwa kwake kikweli hulazimu kuwe na dola kuisimamia na kuilinda.

Kuna mifano mingi inayodhihirisha namna Mtume SAAW alivyotatua migogoro mbalimbali ya ndoa:

Awali, itakumbukwa Mtume SAAW alipotoa hukmu ya ‘dhihar’ (kitendo cha mume kumwita mkewe mama yake), pale mume wa bi Khawlah bint Tha`labah alipotoa kauli hiyo ya kimakosa. Bibi huyo alipeleka mashtaka yake kwa Mtume SAAW kwa kusema:

 “Mume wangu ametumia utajiri wangu, amestarehe na ujana wangu, na amelichosha tumbo langu kwa kumzalia watoto wengi, sasa nimekuwa mzee siwezi kuzaa ananinasabisha kama mama yake.”  (Ibn Jarir, Musnad Ahmad Abu Daud, Ibn Abi Hatim).

Hatimae, Mtume SAAW akatoa hukmu ya ‘dhihar’ kwa kumuadhibu mume wa mama huyo kwa kitendo chake hicho kiovu kama ilivyonukuliwa kwa urefu mwanzoni mwa Surat Mujadalah.

Pili, Mtume SAAW alitatua mizozo kadhaa ya wanawake waliozeshwa kwa nguvu (forced marriage) ukiwemo mzozo wa ndoa ya bi Khansaa bint Khudhaam A l-ansaria alipomueleza  Mtume SAAW kwamba babayake alimuozesha (akiwa bikra) bila ya idhini yake, na bibi huyo ni mwenye kuchukia jambo hilo.  Mtume (SAAW) akavunja ndoa hiyo mara moja.

(Fathul Bari- Sharah Al Bukhari 9/194, Ibn Majah Kitabun Nikah 1/602)

Tatu, Mtume SAAW aliivunja  ndoa ya Abu Rukanah. Wakati mkewe aliposhtaki kwa Mtume SAAW kwamba hamtoshelezi kinyumba.  Kama ilivyonukuliwa katika Sunan ya Abu Daud, kwa mapokezi ya Ibn Abass:

 “Ya kwamba Abu Rukanah alimuowa mwanamke wa kabila la Muzinah. Kisha mwanamke huyo akaja kushtaki kwa Mtume SAAW kwa kusema: 

“Hanitoshelezi hata kwa ukubwa wa unywele huu  (huku mwanamke huyo akiashiria unywele uliokuwa mkononi mwake) Kwa hivyo, nitenganishe baina yangu na yeye.” Mtume SAAW  akavunja ndoa ile.

Nne, Mtume SAAW alitoa hukmu ya ‘al-khul’ katika mzozo wa ndoa ya Habibah bint Sahl, mke wa Thabit ibin Qaays ibn Shammas. Wakati binti huyo aliposema kwa Mtume SAAW:

“Ewe Mjumbe wa Allah sitaki hata kumuona (mume huyu) na lau sio khofu yangu kwa Mwenyezi Mungu ningemtemea mate usoni pake.”

Mtume SAAW akamuuliza Habibah: “Jee utamrejeshea shamba lake alilotoa kukupa mahari? Habibah akajibu ndio, na alipomrejeshea,  Mtume SAAW akawatenganisha. (Al-Bukhari: kitabu cha Al-jami' al-sahih, mada: khul')

 Tano, pia Mtume SAAW alipitisha hukmu ya ‘hadd’ kwa mwanamke mjane aliyezini kwa kupigwa mawe mpaka kufa. Kisa maarufu cha mwanamke wa kabila Ghamid (Muslim 4206). Kupitishwa hukumu ya ‘hadd’ kwa mzinifu aliyeowa au kuolewa ni katika kulinda ndoa ili zibakie katika mazingira ya uaminifu, kuepusha uchafu ndani ya jamii na kuhifadhi nasabu sahihi kwa kizazi.

Hiii ni mifano michache ya namna Mtume SAAW alivyoikabili mizozo na husuma ndani ya ndoa kwa nafasi yake akiwa mtawala wa Waislamu. Na hivi ndivyo pia walivyoikabili mizozo kama hiyo makhalifa baada yake. Kamwe hawakutenganisha ndoa na dola. Kama ambavyo hawakutenganisha mambo mengine ya kiuchumi, kisiasa na suala la utawala. Na hivi pia ndivyo itakavyokuwa mara Khilafah Rashidah kwa manahaj ya Utume itaporudi karibuni kwa idhini ya Allah Taala InshaAllah.

 

Afisi ya Habari -   Hizb ut- Tahrir Tanzania

 25 Jumada al-awwal 1439 Hijri   | 11/02/2018 Miladi

                           http://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Read 1450 times
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…