Sunday, 18 March 2018 00:00

Sheria ya Ugaidi, Chombo cha Kuhalalishia Kuuwa, Kutesea,Kubagua na Kukandamizia Waislam

Kesi ya ndugu zetu ilitajwa mnamo tarehe 12 Machi 2018 na itatajwa tena tarehe 26 Machi 2018 InshaaAllah.

 Waislamu na waaadilifu katika watu jumla jioneeni wenyewe dhulma ya wazi ya sheria dhidi ya Uislamu na Waislamu inayoitwa  ya 'ugaidi'. Sheria hii ni ya kibaguzi iliyotungwa  kukandamiza jamii moja tu ya Waislamu.

 Ndugu zetu hao watatu Ustadh Ramadhan Moshi, Waziri Suleiman na Omar Salum wametiwa nguvuni tangu mwezi Novemba 2017 na bado mpaka leo kesi hii inatajwa tu, bila ya maelezo yoyote. Na kimsingi dhulma kama hii sio wao tu bali wapo Waislamu wengi wakiwemo ndugu zetu wa Uamsho na maelfu ya Waislamu wanaosota mahabusu kwa kisingizio cha ugaidi na kutokamilika ushahidi. Mfano hai ni ndugu zetu Waislamu walioko mahabusu za Arusha na Mwanza.

 Hii ni dalili bayana kuwa hakuna ushahidi wowote dhidi ya watuhumiwa hao, bali kinachotendwa  ni uonevu tu,  kutokana na chuki na dhulma dhidi ya Uislamu na Waislamu zilizomwagwa katika mataifa machanga ikiwemo Tanzania na madola ya magharibi hususan Marekani zikichanganyika na  chuki binafsi za baadhi ya wanasiasa na watendaji

Kwa masikitiko makubwa taasisi za utetezi wa haki za binadamu ziko kimya kufuatia qadhia hizi.  Kimsingi taasisi hizo zinapaswa kuondokana na kuangalia qadhia za dhulma kwa macho ya makengeza. Kama wanavyoyaangazia matukio fulani fulani ya dhulma na ukandamizaji, vivo hivyo wanapaswa waangazie dhulma na mateso kwa Waislamu kwa uadilifu na insafu kama kweli wanalenga kutetea wanadamu.

 Tuendeleeni kuwaombea dua ndugu zetu hao Ustadh Ramadhan Moshi, Waziri Suleiman, Omar Salum na Waislamu waliodhulumia mashariki na magharibi ya Ulimwengu ambao bado wapo katika mikono ya dhulma na uonevu.

 Tunamuomba Allah Taala kwa nguvu zake awakomboe Waislamu wote kutoka katika uonevu na dhulma – Amiin

 "WAACHIWE HURU SIO MAGAIDI"

16 Machi 2018

     

Read 822 times
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…