Friday, 13 April 2018 00:00

Waislam na Wanadamu kwa Jumla Ikumbukeni Siku Hii

Taarifa kwa Vyomba vya Habari

Mwishoni mwa mwezi huu mtukufu wa Rajab, dola za kibepari za kikoloni baada ya njama za hali ya juu na mikakati ya muda mrefu zilifanikiwa kuingusha dola ya mwisho ya Kiislamu ya Khilafah Uthmania ambayo makao makuu yake yalikuwa Uturuki.  Tukio lililofikia kilele mwishoni mwa mwezi wa Rajab 1342AH/ Machi 1924 Miladi.
 
Kwa kuwa Uislamu umeletwa kuwa rehma kwa walimwengu wote, kimaumbile dola yake ya Khilafah pia ni nuru na ukombozi kwa Waislamu na walimwengu kwa jumla. Hivyo, kuangushwa kwa dola hiyo kumeacha athari kubwa isiyo na mfano, mashaka na maumivu kila mahala.  Kwa maneno mengine, kuangushwa kwa Khilafah kumepelekea Waislamu na wanadamu kwa jumla kusibiwa na wimbi kubwa la dhiki, majonzi, maangamizi nk.   
 
Kwa kuangushwa Khilafah Waislamu wamepata hasara kubwa ya kukosa kutawaliwa kwa mujibu wa dini yao ya Uislamu. Hili likawaweka mbali na majukumu nyeti na ya faradhi katika Uislamu na pia kuwatenga na unyenyekevu timilifu mbele ya Muumba wao.  
 
Pia, Waislamu wamekosa kuishi chini ya kivuli kimoja thabiti (Dola ya Khilafah)kinachowaunganisha wote pamoja kama Ummah mmoja bila ya kuzingatia rangi, umbali wa kijografia au mipaka / mistari iliyochorwa na wakoloni. (mipaka ya kitaifa)  
 
Na zaidi, Waislamu wamekosa kuishi kwa amani, utulivu na furaha, na badala yake wanaishi maisha ya khofu, mateso, mauwaji, kuporwa ardhi zao, unyanyasaji usio na mfano, wanaishi bila ya mtetezi wala msimamizi wa kweli.  Kubwa zaidi, kuoneshwa Waislamu na Uislamu kupitia madola ya kimagharibi hususan Marekani kama maadui wa ubinadamu katika ulimwengu.
 
Kwa wasiokuwa Waislamu, kwa kuangushwa Khilafah kumewanyima fursa adhimu ya kukosa kutawaliwa na Uislamu. Pamoja na ukweli kwamba hawangelazimishwa kuwa Waislamu. Lakini kutokana na utekelezaji wa utawala wa Kiislamu na hukmu zake wangeweza kushuhudia nguvu ya Uislamu kifikra na kivitendo katika kusimamia insafu, haki na uadilifu. Kutokana na hilo pia wangepata fursa ya kulinganisha baina ya nidhamu ya utawala ya Kiislamu inayowafikiana na uhalisia na maumbile ya wanadamu dhidi ya nidhamu ya kidikteta ya kileo yaani demokrasia, inayoshikilia itikadi ya usekula inayozitenga dini kando na kutegemea nidhamu na sheria zinazotungwa na mwanadamu.  
 
Pia, wamekosa kuishi chini ya dola inayowazingatia na kuamiliana na raia wake wote kwa msingi mmoja tu wa uraia na sio dini, asili wala kabila. Kama inavyoshuhudia tareekh/historia namna dola
ya Khilafah ilivyofikia kilele cha mafanikio katika kuwafinyanga pamoja watu kutoka jamii mbalimbali wakawa Ummah mmoja bila ya ubaguzi.  
 
Zaidi ya hayo,  wasiokuwa Waislamu wamekosa fursa ya kulindwa, kuhifadhiwa na kutoingiliwa dini zao, kinyume na hali ya leo chini ya nidhamu ya kidemokrasia/ubepari ambapo dini hubenwa na kuburuzwa kwa mujibu matamanio na matakwa ya kidemokrasia, kiasi cha kudiriki kutenzwa nguvu dini hizo  kuhalalisha maovu, machafu na  mambo ya fedheha kama suala la  ushoga.
 
Kwa kumalizia, kwa Waislamu lazima waendelee na jukumu la kufanya kazi ya daawa/ ulinganizi ili kuirejesha tena dola ya Khilafah Rashidah, wakilenga kuasisi dola hiyo kutoka katika nchi kubwa za Waislamu, kwa kupitia njia ya Mtume SAAW ya mvutano wa kifikra na kisiasa ambayo kamwe haihusishi utumiaji nguvu, silaha wala mabavu.
 
Na kwa wasiokuwa Waislamu, wakati umefika kwao kuusoma Uislamu kwa undani na kuutafiti kama mfumo mbadala wenye tija, wa ukweli na wenye uadilifu, inawapasa wafanye hilo hususan kutokana na hali ya duniani leo, ambapo kushtadi kwa mfumo wa kibepari na nidhamu yake ya kisiasa ya kidemokrasia vimeleta nakama, maangamizi makubwa na mashaka yasio na mfano kwa ubinadamu.
 
Masoud Msellem
 
Mwakilishi Kwa Vyombo vya Habari 

Hizb ut Tahrir Tanzania

Read 775 times

Media

Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…