Bajeti ya Kuwanyonga Zaidi Raia

Habari:

Vyombo vya habari vya Tanzania na vya nje vimeripoti juu ya bajeti ya Taifa ambayo vipaumbele vyake ni miundombinu, kudhibiti ukwepaji wa kodi na uchumi wa viwanda. Waziri wa Fedha Dr. Phillip Mpango katika uwasilishaji wa bajeti hiyo alitangaza mpango wa  serikali wa kuongeza mapato, kuziba mianya ya upotevu wa rasilimali za nchi, kudhibiti matumizi na kusimamia sheria ya manunuzi katika idara za serikali.

Maoni:

Bajeti za kibepari zinazopitishwa katika mabunge ya kidemokrasia hazina maana yoyote kwa raia kwa kuwa zimesimama katika kanuni zilizoshindwa kufikia matarajio ya raia.

Kwa kuwepa kodi ya asilimia 40 katika petroli itasababisha kupanda bei huduma mbalimbali na bidhaa hususan gharama za usafirishaji.

Zaidi, kuanzishwa kwa mfumo mpya wa serikali wa kukusanya kodi wa kielektroniki (government e-payment gateway system) maana yake kutapelekea ongezeko zaidi la kodi ambalo litadhoofisha na kuzinyonga  shughuli za  kiuchumi na kuongeza na kuwatwisha mzigo zaidi walaji.

Kwa upande mwingine wakati bajeti ikiwakaba wanyonge, inawabeba wanaoitwa wawekezaji, kwa kuwapunguzia kodi kutoka asilimia 30 mpaka 10 kikiwa ni kivutio kwao. Ni wazi kama mchana kweupe  kwamba hatua za serikali za nchi zinazoendelea ni kwa ajili ya kuwatumikia mabwana wa kikoloni badala ya kuwalenga watu wao. Kwani kwa ukweli uwekezaji wa nje kwa udhati wake ni ukoloni mamboleo.

Bila kutaja fedheha ya wazi ya tangazo la  Waziri wa Fedha Dr. Phillip Mpango alipotamka kuwa serikali itapata asilimia moja ya ada ya kusafisha madini.

Kwa hakika nidhamu ya kiuchumi ya kibepari iliyozimishwa juu ya Tanzania na kwingineko katika nchi zinazoendelea huwatumikia na kuwanufaisha wakoloni, wanasiasa vibaraka, wapambe wao na familia zao, na kamwe haipo kuwatumikia ustawi wa raia.

Nidhamu pekee ya kiuchumi ya uadilifu ni ya Kiislamu ambayo ilitekelezwa chini ya serikali ya Khilafah. Kupitia nidhamu hiyo ulimwengu utaneemeka tena na kuokoka na ukandamizaji na madhila ya uchumi wa kibepari ambao hutegemea 90% ya mapato yake kutokana na kodi za kidhulma.  Uislamu unaharamisha ukusanyaji kodi mpaka kuwe na dharura kubwa, nazo hutozwa wenye uwezo tu.

Mtume Muhammad (saw) amesema:

لَا يَدْخُلُ الْجَنَّةَ صَاحِبُ مَكْس

“Hatoingia peponi Mkusanya kodi “

(Ahmad).

Badala yake Khilafah ina vyanzo vyake maalumu vya kupata mapato vilivyo mbali na kuwapora raia masikini na kuzinyonga shughuli za kiuchumi.

23 Ramadhan 1438 AH/ Jumamosi 18/06/2017

 

Imeandikwa na Ramadhan Said Njera

Mjumbe wa Afisi ya Habari –   Hizb ut- Tahrir Tanzania

Kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari Hizb ut-Tahrir

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!