Demokrasia ni Mfumo Kigeugeu

0

Aliyekuwa Katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Dr. Wilbrod Slaa karibuni ameapishwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Sweden.

Dr. Slaa mgombea aliyewahi kuwa mgombea nafasi ya urais kupitia Chadema, na  kwa miaka mingi kuwa mwiba mkali kwa serikali ya CCM alijiondoa katika chama chake mwaka 2015 kwa madai ya kutoridhishwa na chama hicho kumpokea Edward Lowassa aliyetokea CCM.

Dr. Slaa hakuishia hapo na badala yake alifanya kazi ya kufa na kupona kujaribu kudhoofisha upinzani katika kipindi cha uchaguzi mkuu kipindi ambacho ni muhimu mno kwa vyama kuliko wakati wowote ule. Pengine kwa kibarua hicho ndio leo amepewa zawadi ya ubalozi.

Akizungumzia uteuzi huo, Dr Slaa alimshukuru Rais kwa kumuona, kumuamini na kumpa jukumu kubwa huku akiahidi kwa raisi kuwa hatomuangusha. Mbali na Dr. Slaa wapo madiwani wengi ambao wamesaliti juhudi za wafuasi wao bila ya kujali muhanga wao wa hali na mali walioutoa katika kipindi cha uchaguzi mkuu kuwapigania na kuwachagua. Qadhia ya aliyewahi kuwa mbunge wa Kinondoni kwa chama cha CUF pia ni mfano hai pia, ambaye haikuwa rahisi kupata nafasi ile bila ya muhanga wa wafuasi wake na upinzani kwa jumla. Aidha, tumeshuhudia mivutano na husuma za wazi kiasi cha wengine kuacha chama cha CCM hususan siku za uchaguzi pale walipoona  maslahi yao yapo hatarini.

Hiyo ndio tabia ya kigeugeu ya wanasiasa wa kidemokrasia kama ulivyo mfumo wenyewe wa ugeugeu, na bila shaka tutaendelea kuyashuhudia mengi makubwa zaidi.

Hili ni jambo la kimaumbile kutokea na kutarajiwa kwa mfumo wa kibepari\kidemokrasia usiotokana na Muumba. Mfumo unaotokana na fikra duni za binadamu ukiwa na lengo moja tu la kuongeza maslahi ya maisha mafupi ya kidunia kwa gharama yoyote na bila kujali chochote si utu, ahadi, maadili wala fadhila.

Tunashuhudia katika upande wa kimataifa namna mataifa makubwa yanavyopora rasilimali za mataifa machanga, bila ya kujali wala kubali. Kwa upande wa kitaifa wanasiasa wenye hatamu za uongozi daima huwadhili raia wao huku wao, familia zao na wapambe wao wakinufaika kwa gharama ya wanyonge.

Demokrasia ni mfumo uliombali na usiojali raia. Thamani ya raia ni katika kipindi cha uchaguzi ambacho raia hutumika kama ngazi ya mgombea kufikia utawala ili kudhamini maslahi yao. Tahamaki baada ya uchaguzi mambo huwa kinyume kabisa!.

Amma kwa hakika ni makosa makubwa mbele ya Muumba, kwa mwanadamu kutoa juhudi na muhanga wake kwa mfumo wowote batili ukiwemo wa kidemokrasia, na badala yake muhanga na juhudi havina budi kuelekezwa kwa mfumo wa Muumba yaani Uislamu.

Pindi Uislam unapotabikishwa kikamilifu na serikali yake ya Khilafah, wanadamu huishi maisha yaliyojaa neema duniani, na Akhera watapata  radhi za Allah Taala ambalo ndio jambo kubwa zaidi.

وَلَوْ أَنَّ أَهْلَ الْقُرَى آمَنُوا وَاتَّقَوْا لَفَتَحْنَا عَلَيْهِمْ بَرَكَاتٍ مِنْ السَّمَاءِ وَالأَرْضِ َ (الأعراف: 96

Na lau kama watu wa miji wangaliamini na kumcha Mwenyezi Mungu, kwa yakini   tungaliwafungulia baraka za mbingu na ardhi”

(TMQ 7:96).

 

Afisi ya Habari –   Hizb ut- Tahrir Tanzania

 13 Jumada al-thani 1439 Hijri   | 01-03-2018 Miladi 

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Leave A Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.