Jee Mmeshuhudia Kwa Uwazi Uwongo Wa Demokrasia Zanzibar?

Siku chache zilizopita Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imeitangaza tarehe 20 Machi 20016 kuwa ndio siku ya kurejea tena uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika awali Oktoba 28 2015. Katika uchaguzi huo wa awali Chama cha CUF kilitoa takwimu kuwa mgombea wake wa uraisi alishinda nafasi hiyo.

Tahamaki na ghafla ! Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi alitangaza kuubatilisha uchaguzi huo. Licha ya kutangazwa na waangalizi wa ndani na kimataifa kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki. Huu ni uchaguzi wa nne tangu kuletwa tena mfumo wa vyama vingi mwaka 1995. Chaguzi zote zilizotangulia zimekuwa zikikabiliwa na fujo na vurugu hususan katika ngazi ya uraisi ambapo chama cha CUF takriban mara zote hutangaza kushinda nafasi hiyo, lakini hatimae mgombea wa chama tawala cha CCM hutangazwa kuwa mshindi.

Kufuatia qadhia hii Hizb ut-Tahrir Afrika Mashariki inaendelea kuwakumbusha Waislamu wa Zanzibar na watu jumla yale yale ambayo tumekuwa tukiyasema mara nyingi bila ya kutafuna maneno:

  1. Mfumo wa vyama vingi vya siasa umeletwa na wamagharibi kwa ajili ya maslahi yao na sio kwa maslahi ya raia wa nchi zetu. Kama wanavyodhani wengi kiasi cha kuchanganyikiwa kwa kujigubika matumaini makubwa ya kiuwongo, kupoteza muda mwingi, kutoa jasho jingi na hadi kupoteza maisha yao, wakitaraji ati kutapatikana mabadiliko. Bali mfumo huo umeletwa kuwa mbinu ya kuwabadilishia raia sura tu ya utawala baada ya kuwaona wamechoshwa na wana hali ya kutoridhishwa kutokana na ukandamizaji mkubwa wa chama kimoja. Aidha, mfumo huo uliletwa kutokana na kubadilika hali ya siasa za kimataifa kufuatia kuanguka dola la kisovieti/ USSR kimataifa, na Marekani kubakia kuwa kinara pekee katika uwanja wa kimataifa.
  1. Chaguzi za kidemokrasia licha ya kuwa ni haramu katika Uislamu. Lakini pia chaguzi hizo hazina athari yoyote, wala maamuzi yoyote ya kuweka au kuondosha kiongozi. Bali chaguzi hizo huhamasishwa kuwashughulisha raia, kuwalaghai, kuwadanganya, kuzuwa husuma/ugomvi baina yao na kuwaweka watu mbali katika kufikiria suluhisho la kweli la matatizo yao. Huku madola makubwa kwa kupitia ukoloni mamboleo wakiendelea kunyonya na kupora rasilmali za Umma kwa usahali, na raia wakijidanganya kwa kuona kuwa ndio wanaofanya maamuzi makubwa ya kisiasa katika nchi zao.
  1. Vyama vyote vya kidemokrasia Afrika Mashariki ni wakala tu wa madola makubwa. Vyengine hupewa jukumu la kiutawala ili kulinda maslahi ya madola makubwa, na vyengine ni kwa ajili ya kudanganya raia ili waone kuna mchakato endelevu wa kidemokrasia. Chama cha CCM kinajua kwa dhati kuwa hakuna demokrasia yoyote ! Licha ya kujifanya wamekubali mfumo wa vyama vingi. Huku vyama vya upinzani kikiwemo cha CUF na vyenginevo wakijuwa wazi kwamba kuufikia utawala ni mpaka yatakapotaka mataifa makubwa. Hata kama vyama hivyo vitapata kura kiasi gani. Kwa msingi huo, vyama tawala na vinavyoitwa vya upinzani vipo kuwahadaa raia, kuwalaghai, kuwadanganya na kuwafanya kuwa ni viumbe duni vilivyoumbwa kuburuzwa kwa ajili ya kufikia maslahi yao tu.
  1. Mataifa ya Kimagharibi hayapo kusimamia demokrasia. Kwa kuwa asili hakujawahi kutokea kitu kinachoitwa demokrasia katika udhati wake. Aidha, wala mataifa hayo hayapo kusimamia haki, kwa kuwa yapo kusimamia maslahi yao. Hivyo, wao daima humuweka mtawala mtiifu kwao waliyemkinai kulinda maslahi yao. Amma awe kapata kura nyingi, kidogo au hakupata kamwe !
  1. Demokrasia na udikteta ni pande mbili za sarafu moja. Kwa kuwa katika hali zote mbili Katiba na sheria jumla hutungwa na husimamiwa na wanadamu ambao hutawaliwa na kipimo cha maslahi na sio kipimo cha halali na haramu au kumuogopa Muumba. Hivyo, kuvunja katiba yao wenyewe au kupinda sheria zao ni jambo la kawaida kama kuna maslahi, kama ilivyodhihirika katika uchaguzi uliobatilishwa karibuni Zanzibar. Licha ya ukweli wa mambo kuwa katiba na sheria hizo ni duni zinazotokamana na akili finyu ya mwanadamu.
  1. Tunawakumbusha Waislamu wa Zanzibar na kuwanasihi kwa ikhlasi kubwa kwamba mataifa ya magharibi yanakuandalieni mazingira ya kumwagwa damu zenu kama ilivyomwagwa kikatili kwa dhulma mwaka 1964 na 2001, na hatimae waathirika wakubwa ni raia wa kawaida. Na mwishowe CUF na CCM huketi meza moja raha mustarehe kugawana ngawira, kana kwamba hakuna kilichopotea cha thamani katika maisha yenu. Kwa kuwa vyama vyote viwili hivi ni vyama vya bwana mmoja, nae ni Marekani.
  2. Kwa kukhitimisha, Hizb ut Tahrir Afrika Mashariki haitochoka kuwaiteni tena na tena enyi Waislamu : Amkeni kutoka katika usingizi mzito wa kupigania mfumo haramu wa kidemokrasia ambao umewaletea nyinyi na dunia nzima mateso, madhila na mashaka makubwa yasioelezeka. Tunawauliza, jee haujafika tu muda wa kuungana na Hizb ut Tahrir katika kulingania mfumo wa Kiislamu. Mfumo pekee wa haki na uadilifu kwa ajili ya kutabikisha/kutekeleza yale yanayomridhisha Mola wetu kwa kupitia Dola ya Khilafah kwa manhaj ya Utume? Au mnataka dalili gani tena ya uharamu na kutofaa mfumo batil wa kidemokrasia? Hebu hudhurisheni nyoyo zenu, zingatieni na mtafakari, mnajuwa kuwa awali mlikuwa chini ya Usultani, baadae mkawa na vyama vingi baada ya uhuru wa bendera mwaka 1963, kisha mkawa na chama kimoja baada ya Mapinduzi 1964, hatimae sasa mmerejea tena kwa mara ya pili kwenye vyama vingi. Basi hamjaona tu kuwa safari yenu sasa imeshafika ukingoni? Jee mnataka kumfanya Allah Taala, Muumba wenu kuwa ndio chaguo lenu la mwisho, baada ya kushindwa juu ya kushindwa? Basi amkeni na zindukeni. Patilizeni fursa hii kabla haijaondoka !

Masoud Msellem

Naibu Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari

Hizb-ut Tahrir Afrika Mashariki

Kumb : 06/1437 AH          

17 Rabii’ II 1437 AH 

27/01/2016 CE

Tel +255 778 870609

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!