Khutba kwa Makhatibu wasiojua khutba

0

Khutba sio kutoa darsa juu ya mimbari, sio kutoa mawaidha, sio darasa la kufundisha fiq’hi, sio ulingo wa mijadala ya kimadh’hab, sio ulingo wa mbwembwe za elimu na taaluma, sio jukwaaa la kughani sauti nzuri na mahadhi ya sauti, sio mimbari ya kuzungumza misimamo ya kimakundi au kifirqah, na mwisho kabisa khutba sio kiriri cha simulizi za historia/taariikh.

Leo waislamu wamechoshwa na khutba za makhatibu wetu na kuishia kupiga  usingizi  kwa sababu makhatibu  hawatoi khutba bali wanatoa darsa juu ya mimbari na wengine huenda mbali zaidi kwa kufanya ni jukwaa la malumbano. Labda tujiulize kwa nini makhatibu wetu hawawezi kutoa khutba dakika 15, kama ilivyotaka sheria kuwa khutba isizidi urefu wa swala ya ijumaa

JE KHUTBA NI NINI?

Khutba ni kutangaza msimamo juu ya tukio jipya kwa Umma wa Kiislamu na kwa wasio kuwa Waislamu. Ima kuunga mkono jambo, kupinga jambo au kuanzisha agenda/kampeni maalumu na kuizindua rasmi juu ya mimbari. Sharti jambo lenyewe lisiwe ni jambo la kifiq’hi au kimadh’hab kwani fiq’hi ni somo linalohitaji mtu kusomeshwa na sio kuambiwa ndani ya dakika 15. Msikiti wa Ijumaa wanahudhuria Waislamu wa madh’hab tofauti tofauti na lau khutba ikiwa ni juu ya Swala au Talaka au Ndoa; je utazungumza kwa mujibu wa madh’hab ipi? Bali wapo makhatibu leo wanapanda juu ya mimbari siku ya Ijumaa na ‘mada ya Usul-ul Fiq’hi au Mustalahu l-hadith’ somo ambalo khatibu mwenyewe halijui.

Leo khatibu yupo juu ya mimbari ananukuu aya au hadithi na kutaja namba za kurasa na mstari wa ngapi katika kitabu, hii sio khutba bali haya ni mashindano ya watoto darasani kuwakomaza uwezo wa kuhifadhi. Khatibu anazungumza mada dakika 50 hatimaye anatangaza mada yaendelea wiki ijayo hiyo sio khutba bali  ni darsa za wanafunzi  katika maandalizi ya mitihani.9!

Khutba ni kutangaza msimamo wa Kiislamu juu ya hatua gani Waislamu wa chukue juu ya kadhia husika katika jamii.  Mfano kumezuka kipindupindu eneo la Zanzibar –Tanzania; khutba za Ijumaa zilitakiwa kuangazia suala hili kwa mfano tukizingatia nukta/sura ifuatayo:

  1. Uwezo na maamuzi ya Allah(qadhaa)
  2. Uwezo na majukumu ya binadamu(uzembe na ufanisi)
  3. Hukmu ya Muislamu  anayekufa kwa kipindupindu
  4. Uozo na Uzembe kwa watawala na nini walitakiwa kufanya kabla na baada ya kipindu pindu kutokea,
  5. Kutoa pole walio fikwa na msiba na tahadhari juu ya ugonjwa huo.

Lakini la kushangaza na kusikitisha utamuona khatibu anapanda juu ya mimbar na mada ya ‘Fadhila za Maulamaa’ na ilhali pembeni  ya Msikiti anaohutubia kuna zikwa ndugu watatu wa familia moja kwa sababu ya kufa kwa ugonjwa wa kipindupindu.

Asili ya mimbari za Ijumaa ni jukwaa/ulingo wa kisiasa na misimamo na sio jukwaa/ulingo wa fiq’hi na darsa za kimadh’hab. Na ikiwa makhatib wetu hawajui siasa za Kiislamu na pia siasa za kikafiri ili wazikosoe, kwa kutumia kipimo cha siasa za Kiislamu basi tutaendelea kusisinzia sana kwenye khutba.

Aidha, ikiwa makhatib wetu ikiwa hawajui tofauti ya uchumi wa Kiislamu na uchumi wa kibepari tutasinzia sana. Ikiwa makhatibu wetu hawajui dunia inaongozwa na mfumo aina gani tusubiri khutba za nguzo 17 za swala, milango ya pepo na majina na aina zake. Lau makhatibu wetu hawajui tofauti ya hadhara na madaniya (mambo yepi tunaruhusiwa kuchukuwa toka kwa makafiri na yepi haturuhusuwi) tusubiri khutba za  namna ya kuchagua mke bora au mume bora. Mwisho kabisa, ikiwa makhatib wetu hawajui vipi kuurudisha Uislamu utawale dunia leo tusubirini khutba za namna ya kufanya jimai baina ya mke na mume.

Khatibu anayepanda na karatasi (gazeti) kama anayetaka kusoma mapato na matumizi ya ulimwengu ya mwaka mzima kama hotuba ya Bungeni, hiyo sio khutba bali ni mawasilisho ya mapato na matumizi. Khatibu anayepanda mimbari na zigo la vitabu ili kutoa ushahidi huyu si khatibu bali yupo kwenye mdahalo. Nikimalizia natamka kwa unyenyekevu “Ewe khatibu rudisha hadhi na heshma ya mimbari ya Al Habib Mustafa Muhammad Ibn Abdullah SAAW”

Ramadhani Moshi Othman (Abu Fat’hi)

Leave A Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.