Kuangamizwa Fira’uni ni Bishara ya Kurejea Khilafah

Mwezi wa Muharram ndani yake imo siku ya Ashura. Siku ambayo Fira’un na jeshi lake waligharikishwa na kunusuriwa Mtume Mussa AS. na wana wa Israil.

Amesimulia Ibn Abbas RA. kuwa Mtume SAAW alifika Madina akawakuta Mayahudi wanafunga siku ya Ashura. Akasema :

Nini hii?. Wakasema : Hii ni siku ambayo Allah (Taala) aliwaokoa Wana wa Israil kutoka kwa adui wao. Na Mussa (AS) alifunga siku hii kushukuru.

Basi Mtume (SAAW) akasema:

“Sisi tuko karibu zaidi (tuna haki zaidi) kwa Mussa kuliko nyinyi.”Hivyo alifunga siku hiyo, na kuwataka watu wafunge.

(Ibn Majjah).

Allah Taala anatueleza juu ya kuangamizwa huko kwa Fir-aun kwa kusema:

وَاتْرُكِ الْبَحْرَ رَهْوًا إِنَّهُمْ جُندٌ مُغْرَقُونَ
“Na iache bahari ( kuwa katika hali ya kuachana), hakika hilo ni jeshi lenye kuangamizwa.

(TMQ 44:24).
Hivi ndivyo ilivyokuwa hatima ya Fir’aun, na Allah Taala akawaokoa Waumini juu ya unyonge wao na kuwafanya wao kuwa ndio watawala na viongozi :

وَنُرِيدُ أَنْ نَمُنَّ عَلَى الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا فِي الأَرْضِ وَنَجْعَلَهُمْ أَئِمَّةً وَنَجْعَلَهُمُ الْوَارِثِينَ

“Na tunataka kuwafanyia ihsani wale waliokandamizwa katika nchi ili tuwafanye wao viongozi na tuwafanye wao kuwa warithi.”

(TMQ 28:5)

Leo tunashuhudia ukandamizaji wa Waislamu mashariki na magharibi Kuanzia kutoka kwa vibaraka katika nchi za Waislamu na madola makubwa kama Marekani, Uingereza, Urusi nk. Ukandamizaji ambao umeambatana na kila aina ya dhulma ikiwemo mauwaji, utesaji, udhalilishaji, uporaji wa ardhi na rasilmali za Waislamu, utekaji nyara walinganizi, nk. Yote hayo hutendwa na watawala hao katika hali ya kutapatapa kuzuia kurudi tena dola ya kweli itakayowaunganisha Waislamu wote ya Khilafah Rashidah. Wakijisahaulisha watawala hao funzo muhimu kutoka kisa cha Ashuraa cha kuangamizwa dhalimu na jeshi lake na kunusuriwa Waumini.

Enyi Ummah uliotukuka,
Baada ya dhiki faraja. Na kwa kadiri usiku utakavyokuwa mrefu alfajiri hujiri, Basi tuendeleze kazi ya kulingania haki na kupambana na batil katika ardhi. Kwa juhudi zetu, kwa nusra ya Mola wetu hatimae batil na madhalimu wataondoka, na haki itadhihiri kwa kurudi tena dola ya Kiislamu ya kilimwengu ya Khilafah Rashidah InshaAllah.

(وَقُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقًا ).
“Haki imeshadhihiri na batil itajitenga . Hakika batil daima ni yenye kujitenga.

#UislamuNiHadharaMbadala

Maoni hayajaruhusiwa.