Kuangazia Fikra Hatari ya ‘Dini Mseto’

Mtume SAAW na Makhalifa baada yake waliubeba Uislamu kiukamilifu ukiwa ni haki kutoka kwa Mola wao bila ya kuichanganya haki na batil, kinyume na inavyopigiwa debe leo kwa kampeni batil ya dini mseto.

Harakati hizi za dini mseto ili kuleta ukuruba baina ya dini zilianza rasmi 1932 pale Ufaransa ilipotuma wawakilishi wake Chuo cha Azhar ili kuasisi ukuruba baina ya Uislamu, Ukristo na Uyahudi.

Malengo ya dini mseto ni kutaka kuzuiya sheria za dini kutawala duniani. Hili ni kuangamiza Uislamu, kwa kuwa ndio dini pekee yenye nyanja ya utawala, na badala yake kutawalisha sheria za kibepari na kidemokrasia zinazotokamana na akili finyu ya wanadamu kupitia mabunge. Yawe mabunge ya Marekani, Ulaya au nchi vibaraka ambayo baadhi yamesharuhusu ushoga, ulevi, utoaji mimba, kodi za kuuwa maskini nk. Aidha, malengo hayo yanalenga sheria zitokanazo na dini zisiruhusiwe kumuongoza mwanadamu madamu tu dini zingine hazina sheria za siasa na kiutawala.

Hapa Uislamu ndio unabakia kuwa mlengwa mkuu. Harakati za dini mseto zinalenga kulaani na kuzuiya fikra ya dini yoyote kuwa na sheria na utawala, kwa hoja dhaifu kuwa dini zitaleta fujo na maafa duniani. Ilhali maafa, mauaji, mateso na vita visivyokwisha duniani leo na vilivyotangulia vimesababishwa na ubepari na demokrasia yake na wala sio dini. Hata vita vinavyojidhihirisha kuwa vya kidini, mara nyingi, madola ya kibepari ndio waasisi wa vikundi vingi kwa malengo maalumu, na pale wanapoona wavimalize vikundi hivyo, huviangamiza. Basi kwanini wasingelaani mfumo huu wa kibepari wenye maafa, badala yake wanapambana na kitu ambacho wanakhofu tu ikiwa kitapatikana kitaleta maafa? Mbona wanajitia upofu katika jambo lililowazi?

Vipi kuhusu Jihadi?

Ni kweli Uislamu unaruhusu jihadi, kama inavyoruhusu mifumo mengine katika kutanua na kulinda mifumo yao. Ajabu ni kuwa makafiri hususan mabepari kwa propaganda zao wanaipotosha kwa makusudi. Ndani ya jihadi hawapigwi raia, viongozi wa dini, wanawake, wazee wala watoto. Bali jihadi hupiganwa baada ya kushindikana diplomasia dhidi ya watawala madhalimu na wanajeshi wanaowatetea watawala hao. Na Jihadi ya aina hiyo husimamiwa na serikali ya Kiislamu ya Khilafah tu, na sio vikundi vya chochoroni.

Vipi kutawala dini moja pekee?
Hilo ni sawa, na Uislamu ndio utakaotawala peke yake, kwa kuwa ndio wenye mfumo wa kutawala. Amma dini zilizosalia hazina kabisa sheria na kanuni za kiutawala kama siasa, uchumi, nidhamu ya kijamii, nidhamu ya kuadhibu wahalifu, sera za nje nk.

Ikiwa leo wafuasi wa dini zisizokuwa Uislamu wapo chini ya utawala wa mapagani wasiomtambua Mungu (demokrasia), vipi waone tabu kuwa chini ya dini yenye kutawala kwa sheria za Mungu? Madola ya kibepari yamejaza kasumba ya khofu na chuki kwa wafuasi wa dini zingine ili waogope Uislamu, ati siku ukitawala tu basi ‘watakatwa vichwa. Propaganda hiyo huhusisha kuyafadhili makundi maovu yanayoharibu haiba ya Uislamu kwa kuwadhuru watu, wakiwemo Waislamu ili kutisha na kuonesha kuwa Uislamu ni dini ya chinjachinja. Huku ikifichwa historia inayong’ara kwa karne 13, dini mbali mbali zilipokuwa chini ya utawala wa Kiislamu, bila ya kukandamizwa wafuasi wa dini hizo. Mtume (SAAW) anasema:

ألا مَنْ ظَلَمَ مُعَاهِداً أَوِ انْتَقَصَهُ أَوْ كَلَّفَهُ فَوْقَ طَاقَتِهِ أَوْ أَخَذَ مِنْهُ شَيْئاً بِغَيْرِ طِيبِ نَفْسِهِ فَأَنَا خَصْمُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ» رواه أبو داود.
“Sikilizeni! Yeyote atakayemdhulumu muahid (raia asiyekuwa Muislamu aliye chini ya dola ya Kiislamu)au kumdhalilisha au kumpa kazi nzito asiyoiweza au akachukua chochote kutoka kwake pasina ridhaa yake mimi nitakuwa mgomvi (wa mtu huyo) Siku ya Qiyama”
(Abu Daud)

Jee Uislamu unaruhusu kushirikiana na dini nyengine?

Uislamu haukubali kabisa kushirikiana na dini zingine katika mambo ya kiimani na kidini isipokuwa unaruhusu Waislamu kushirikiana na wasiokuwa waislamu katika miamala binafsi ya kijamii na kiuchumi kama ujirani, biashara, kusaidiana nk. Lakini sio kuungana kidini na kiimani na watu wa dini zingine kama tunavyoona leo masheikh wakiingia kanisani na maaskofu kuingia misikitini.

Sisi tunaamini huo ni ukafiri, na msimamo huu wa kutoshirikiana kiimani pia upo hata kwa dini zingine. Kamwe hutosikia makanisa yakipiga marufuku kula nguruwe ili kuungana na Waislamu, japo tunaona wakristo na Waislamu wakisaidiana kwenyo matatizo yao. Basi vipi Muislamu anayeamini Mungu Mmoja, hakuzaa wala kuzaliwa kuungana na mtu anayeamini Mungu alizaa au alizaliwa, alikufa bali alicharazwa viboko kamwe? Hawawezi watu kuungana isipokuwa pale mmoja atakapoacha dini yake na kufuata ya mwingine.

Ufadhili wa kampeni ya dini mseto.
Madola ya kibepari ndio waasisi na wafadhili wa kampeni hii. Wameanzisha vyama, jumuiya na mashirika mbalimbali na wamewanunua baadhi ya viongozi wa dini kutoka dini zote kulingania dini mseto. Wakitoa hoja za uwongo kuwa watu wote waungane na washirikiane pamoja pasina kuangalia dini zao, kumbe ni kwa ujanja wa kuwaweka chini ya utawala wa ukandamizaji wa kidemokrasia, wakidai dini ziishie ndani ya majumba ya ibada tu, kwa kisingizio kuwa dini moja ikitaka kutawala dini zingine kutazuka maafa na vita vya kidini ambavyo ni vibaya zaidi.

Kauli mbiu zake za kuhadaa.

Kauli mbiu kama amani, upendo, umoja, mshikamano, kusaidiana, utaifa, ubinadamu nk. hutumika kuwavutia watu na kuonesha anayepinga fikra hii ya dini mseto ni mtu asiyependa mambo hayo. Ifahamike kuwa kabla ya kuzuka kwa demokrasia na ubepari Waislamu na wakristo au watu wa dini zingine zote walikuwa wakiishi pamoja na hapakuwa na vita baina yao lakini baada ya kuzuka ubepari vita vimezuka kila pembe. Ajabu! leo hii wao ndio wanataka kuwafundisha amani watu waliokuwa kwenye amani kwa makarne?

Majukumu ya harakati za Dini Mseto

Harakati hizi zinapinga kwa nguvu zake zote watu kuwaza kutawaliwa na sheria za Mungu. Kimsingi harakati hizi ni ajenda ya madola makubwa, vibaraka wa wanasiasa wake, na kamwe huwezi kuzisikia harakati za dini mseto hata kwa bahati mbaya kukosoa maovu ya wanasiasa na uovu wa mfumo wa kibepari na madola yake ya kikoloni.

Aidha, harakati hizi zinahubiri iwe mwiko kujadili dini ipi ya haki na ya kweli, bali wanachokitaka wao ni kila mtu abakie kwenye dini yake kwa sharti tu akubali kutawaliwa na demokrasia na asipingane nayo na utawala wake.

Huu ni msimamo wa kidemokrasia waliobebeshwa wanaharakati wa dini mseto wa kuzuiya kujadili dini ipi ya haki. Na kamwe huo sio msimamo wa Uislamu, ukristo au uyahudi kwani wafuasi wa dini hizi kila mmoja anaamini dini yake ndio ya kweli na haki, jambo ambalo kimaumbile linafungua mijadala ya kila mtu kutetea dini yake. Na mara zote Uislamu huibuka mshindi, muhimu tu isiwe fujo, mapigano na lugha chafu.

Matumizi ya neno ‘kafiri na ‘amani’
Katika kilio kikubwa katika harakati za dini mseto ni kupambana dhidi ya matumizi ya neno ‘kafiri’. Katika kampeni hii wanajaribu kuonesha kuwa ni kosa la jinai kumwita asiyekuwa Muislamu ‘kafiri’ na badala yake wamekuwa na ujasiri mkubwa wa kuutengenezea Uislamu matamshi mengine kwa mtu wa aina hiyo, eti aitwe ‘asiyekuwa Muislamu, mtu wa dini nyingine au imani ya upande wa pili.

Kwa mujibu wa Uislamu neno ‘kafiri’ limetumika kwa maana ya kila ambaye si Muislamu, awe anapiga vita Uislamu au haupigi vita. Na halina maana ya tusi kama wanavyojaribu kuonesha watu. Haya ni katika majaribio ya kutaka kubadilisha Uislamu kama walivyofanikiwa kubadilisha baadhi ya mambo ndani ya Biblia. Kama alivyowahi kutamka Obama kuwa, Biblia ilifanyiwa marekebisho, anatamani Quran pia ifanyiwe hivyo. Jambo ambalo katu halitowezakana. Hivyo, fikra za kupinga kutumika neno kafiri ni kuikosoa Quran ambayo imetumia neno hilo mara mia kadhaa. Basi atakayekubali fikra na misimamo ya dini mseto na kuona dini ya Uislamu ipo sawa na dini zingine baada ya kufahamishwa atakuwa ni kafiri. Allah atuepushe na ukafiri huo.

Aidha, tamko amani ambalo ni maarufu na hudandiwa sana ndani ya kampeni hii, nalo kwa mujibu wa Uislamu ni ile hali ya watu kuwa chini ya sheria za Muumba na sio kuwa chini ya mfumo katili wa kibepari unaoangamiza viumbe na kuruhusu kila aina ya uchafu, kuwatukuza wanasaisa na kuwadhalilisha raia na viongozi wa dini.

Enyi Waislamu:

Mabepari wameshindwa kumletea mwanadamu amani ya kweli ndio maana wakamtafutia amani ya kufikirika kupitia dini mseto. Kwa bahati mbaya baadhi ya madalali wa kampeni hii pia wamo Waislamu ili iwe rahisi kuwarubuni watu wa kawaida. Tunawazindua juu ya hatari, fitna na balaa la dini mseto. Tunawadharisha juu ya amani ya kufikirika, huku wafadhili wa kampeni hiyo wakiendelea kuwarundika Waislamu magerezani kwa dhulma, kuwatesa na kumwaga damu zao kila mahala. Basi simamaeni imara kuifedhehi fikra hii ya hatari na ya kikafiri. Tunawalingania Waislamu kuja katika uwajibu wa kurejesha tena dola ya Khilafah itakayodhamini kuulinda Uislamu na kila adui wa kivitendo au kifikra.

Imeandikwa na Ust. Ramadhan Moshi (imehaririwa)

Risala ya Wiki No. 58

26 Muharram 1441 hijri 25/09/2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.