Kumbukumbu Ya Marehemu Sadiq Issa Dafa Mwanamume Asiyesahaulika Kwetu

بسم الله الرحمن الرحيم

Ukingoni mwa mwezi wa Ramadhani mwaka 1434 Hijri / 2013 miladi tulipata msiba wa kufariki ndugu yetu, kipenzi chetu na mwanaharakati imara marehemu Sadiq Issa Dafa kufuatia ajali ya gari iliyotokea huko Mbeya wakiwa safarini kuelekea Malawi.

Mnamo tarehe 9/08/2013 ijumaa / Shawwal 2, 1434
Al-Jum’ah tulipokea taarifa za msiba huo, na ilipofika tarehe 11/08/2013 tukamzika ndugu yetu huyo katika makaburi ya Chang’ombe jijini Dar-es-Salaam baada ya maiti yake kuwasili.

Kwa hakika tumefikiwa na wakati mgumu baada ya kuondokewa na kipenzi chetu na mwanachama mwenzetu wa Hizb-ut-Tahrir ambae kenda kukutana na Allah Taala. Tunamuomba Allah Taala Amkutanishe na wenye kutenda matendo mema katika Pepo yake iliyojaa neema.

Kwa msiba huu tunapata msukumo wa kumuelezea ndugu yetu marehemu kwamba kweli alikuwa mwanamume kweli kweli.
Kwanini tuseme hayo?
Kwa hakika mwanaume si kuwa tu kuvaa shati na suruali, kuwa na sauti nzito, ndevu nyingi , kifua kipana nk. Bali hizi ni sifa tu miongoni mwa sifa zinazoonyesha kuwa huyu anayezungumziwa ana jinsia ya kiume lakini si lazima awe manamume. Basi tufahamu si kila mwenye jinsia ya kiume ni mwanaume. Bali mwanamume ni sifa ya kipekee ambayo hata mwenye jinsia ya kike anaweza kuwa nayo. Hakika mwanamume huwa na sifa ya kujitolea muhanga katika qadhia ngumu, hujipinda katika kuyaendea yale waliyokata tamaa nayo wengine mpaka kufikia lengo lake. Hakika hizi ni miongoni mwa sifa za mwanamume.
Allah (SW) anasema:


مِنْ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّهَ عَلَيْهِ فَمِنْهُمْ مَنْ قَضَى نَحْبَهُ وَمِنْهُمْ مَنْ يَنْتَظِرُ وَمَا بَدَّلُوا تَبْدِيلاً (الأحزاب: 23
“Katika Waumini kuna wanaume wamesadikisha yale waliyomuahidi Mwenyezi Mungu juu yake, wapo miongoni mwao wamemaliza muda wao kuishi na wapo miongoni mwao wanasubiria muda wao na hawajabadilika hata kidogo” (TMQ Ah-zab: 23)


Sababu ya kuteremka ayah ni ni yale yaliomkuta sahaba Anas bin Nadhir ra. katika vita vya Uhud. kwani alipigana kwa ujasiri wa hali ya juu na kuuwa wengi katika mushrikina, na mwisho na yeye pia akauwawa. Anasimulia Anas bin Maalik “…Tukampata na majeraha themanini na kadhaa aliyopigwa nayo kwa panga au kudungwa mikuki au kudungwa na mishale na tulimpata ameshauwawa na washirikina walikuwa wamemharibu vibaya na hakuna kati yetu aliye mtambua isipokuwa dada yake kwa kidole chake” na anasema Anas tulikuwa tunaona ayah ii iliteremka kwa ajili yake.


Hakika tunapowazungumzia wanaume wa Umma huu hatuwezi kumsahau marehemu Sadiq Issa Dafa. Kwa kuwa ni miongoni mwa Waislamu wachache waliojitolea muhanga nafsi pamoja na mali zao kwa ajili ya dini hii tukufu.
Mwaka 1997 marehemu Dafa aliwahi kujiunga na Umoja wa Vijana wa Kiislamu katika Msikiti Temeke Tungi na alibeba majukumu yote aliyopewa na uongozi wa msikiti huo kwa Ikhlasi. Alitusimulia mmoja katika viongozi wa Umoja huo ambaye pia alikuwa kama mlezi wa Dafa kwa kipindi chote alipokuwa akitumikia Umoja huo.
Mwanzoni mwa miaka ya 2000, marehemu Dafa alikutana na mashababu wa Hizb-ut-Tahrir na kufahamishwa Qadhia ya Umma huu, Qadhia ya kufa na kupona, Qadhia ya kurejesha tena maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Dola moja ya Kiislam ya Khilafah. Dola kuu ya Kiulimwengu. Dafa hakusitasita wala kufanya khiyana alijiunga na Hizb-ut-Tahrir katika kipindi hicho na kubakia kuwa muaminifu na mtenda kazi katika harakati hiyo mpaka yanamkuta mauti.


Marehemu Dafa alikuwa ni miongoni mwa mashababu wa mwanzo mwanzo wa Hizb-ut-Tahrir jijini Dar-es-salaam alibeba kwa nguvu zote da’awa ya kuamsha Ummah wa Kiislamu uliozama katika kiza cha ukafiri wa ubepari na nidhamu yake chafu ya kisiasa ya Kidemokrasi. Hizb jijini Dar es Salaam ilifanikiwa kufanya mihadhara kadhaa katika Msikiti wa Temeke Tungi kupitia yeye, na hakusita kukabiliana na mtu yeyote katika kumkumbusha jukumu hili tukufu la kurejesha maisha ya Kiislamu kwa kufanya ulinganizi wa kurejesha tena Dola ya Khilafah.

Aliwakabili watu wa kawaida, wasomi wa sekula, maustadh na hata mashekhe. Marehemu hakujali licha ya baadhi ya maustadh na mashekhe kumbeza kwa kumwambia eti analingania Khilafah hali ya kuwa hana elimu. Kana kwamba kusema haki unapaswa kufikia daraja fulani ya elimu.
Hakika Dafa hakupumbazika na kazi, biashara wala kuuza mbele ya kumkumbuka (kumtaja) Mola wake juu ya jambo lolote lile. Alibeba majukumu yake ya daawa kwa muhanga mkubwa, hata katika hali ngumu.

Aidha, marehemu daima alijifunga na kipimo cha Halali na Haramu katika matendo yake yote, na khasa katika kuindea rizki yake. Alijiepusha kurithi mashamba, viwanja na mali nyengine za baba yake mzazi ambaye aliritadi na kufa katika ukafiri. Na Daffa akabakia katika umasikini wake kwa kumridhisha Mola wake. Na hata alipokuwa anafanya kazi ya boda boda alijiepusha kumpakia abiria yoyote wa kike isipokuwa mkewe na maharimu zake tu. Hali ya kuwa wateja wengi wa boda boda katika jiji la Dar-es-salaam ni wanawake. Hii ni ishara tosha ya kukhofia kukaribia yatakayomkera Mwenyezi Mungu SW.

Kwa hakika mwanamume huyu hatuwezi kumueleza katika kurasa hizi chache, letu kubwa ni kuinua mikono yetu Tukimuomba Allah Taala Amkubalie matendo yake mema na Amsamehe makosa yake na Amkutanisha na waja wema waliotangulia katika Pepo yake ya daraja ya juu. Ameen.

INNAA LILAHI WA INNA ILAYHI RAAJIUUN

Mkiongwe Mbwana

Maoni hayajaruhusiwa.