Kusafiri kwa Wanawake.

Hadithi ya Mtume SAAW aliyoitoa Muslim kupitia kwa Abu Huraira inasema:

“Si halali kwa mwanammke mwenye kumuamini Allah na Siku ya Mwisho akasafiri safari ya siku nzima isipokuwa lazima awe na maharimu wake”

Ufafanuzi wa hadithi hii ni kama ufuatao:

1. Ni ‘haramu’ kwa mwanammke kusafiri peke yake bila ya Maharim wake kwa muda uliotajwa. Yaani siku kamili (masaa 24) usiku na mchana.

2. Hadithi hii inaeleza juu ya ‘muda’ na wala sio umbali wa ‘masafa’. Lau kama atasafiri mwanammke kwa ndege bila ya Maharim kwa masafa ya kilomita 1000, akenda na kurudi bila ya kukamalika muda huo (siku moja) basi jambo hilo linajuzu. Ama lau atasafiri kwa miguu kilomita 20 na ikamchukuwa safari hiyo zaidi ya siku moja (usiku na mchana). Basi itakuwa ‘haramu’ kwake kusafiri bila ya Maharim.

3. Hadithi nyengine zilizopokelewa katika suala la kupunguza swala na ruhusa ya kula mchana katika mwezi wa Ramadhani zinagusia masafa ya ‘umbali’ ambao ni wa ‘Bureda’ 4, ambazo zinakadiriwa kuwa ni kiasi cha kilomita 89, katika hilo ‘masafa’ ndiyo yanayozingatiwa. Basi yoyote atakaesafiri masafa haya kwa ndege, meli au kwa miguu itajuzu kwake kupunguza swala, vyovyote muda utakavyokuwa.

4. Mazingatio katika safari bila ya Maharim kwa mwanammke ni muda wa usiku na mchana vyovyote yatakavyokuwa ‘masafa’. Ikiwa mwanammke hatokaa katika safari yake muda huu na akasafiri na kurejea kabla ya muda huu kukamilika itajuzu kwake kusafiri bila ya maharim. Amma katika kupunguza swala na ruhusa ya kula mchana ndani ya Ramadhani kinachozingatiwa ni ‘masafa’ vyovyote muda utakavyokuwa ama mrefu au mfupi.

5. Amma suala la usalama wa mwanammke binafsi hilo ni suala jengine kando. Ikiwa hatoamini juu ya usalama wake isipokuwa awe na maharim wake, basi katika hali yoyote itakayokuwa asisafiri hata kama nusu siku. Kwa kuwa hilo ni suala jengine.

6. Maharim awe ni mwanamume na awe katika maharim wa mwanamke msafiri. Amma wanawake kwa wanawake wenzao walio waaminifu kuna baadhi ya mafuqaha/wanavyuoni wamejuzisha kwamba wanaweza kusafiri nao. Lakini sisi tunashikilia msimamo/tunatabanni kwamba asisafiri mwanamke bila ya maharim wake ila kwa muda ulioruhusiwa.

7. Mwenye kusafiri kwa ajili ya Semina fupi kama muda wa miezi mitatu, hukmu yake itakuwa ni sawa na hukmu ya msafiri ikiwa hakusudii kufanya makaazi katika mji anaokwenda kwenye semina. Bali awe kaenda kwa semina tu na kurudi katika mji wake wa asili. Basi katika hali hii hukmu yake inakuwa ya msafiri. Ama kama atakusudia kufanya makaazi huko kwenye mji inakofanyika semina, basi katika hali hii hukmu ya msafiri itaondoka

Imefasiriwa kutoka mtandao wa: www.. hizb-ut-tahrir. Info/arabic

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!