Kwa Nini, Uchamungu Haufikiwi

0

Wakati tukiwa ndani ya mwezi wa Shawwal, mwezi unaofuatia baada ya Ramadhani ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha kwa kila mwenye tembe ya imani juu ya kudorora kwa uchaMungu wa Waislamu na walimwengu kwa ujumla. Kabla ya yote ieleweke wazi kuwa dhana ya uchaMungu imeharibiwa na kupotolewa kiufahamu (maana sahihi) katika mabongo ya Waislamu. Hayo ni matokeo ya kampenikabambe ya kuharibu fahamu mbalimbali za Kiislamu ili Uislamu uonekane kana kwamba ni dini ya kiroho na si mfumo kamili wa maisha kuwaoongoza wanadamu katika kila kipengee cha maisha yao.Kwa ufupi uchaMungu ni kutenda au kuacha kutenda kwa kufungamanisha na matakwa ya Allah Taala. Yaani kutenda au kuacha kutenda baada ya kujua hukmu Aliyoihukumia Allah (S.W.T) juu ya kitendo husika.

Kwa udhati uchaMungu kwa upana wake ni kufuata yale yote Alioyaamrisha Allah (S.W.T) na kujiepusha na yale yote Aliyoyakataza kwa kutaka radhi zake. Na Allah Hakuacha kufafanua kila kigusacho maisha ya mwanadamu. Iwe ni mas’ala ya kiibada, kisiasa (utawala), kiuchumi ama kijamii. Kama kauli Yake SWT pale Aliposema:

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِكُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً وَبُشْرَى لِلْمُسْلِمِينَ (النحل:

“Na Tumekuteremshia juu yako kitabu chenye kubainisha kila kitu, na  mwongozo, na rehema, na bishara njema kwa wanaojisalimisha” (TMQ 16:89).

Kwa bahati mbaya na kwa masikitiko makubwa kutokana na fikra ya kutenganisha baina ya dini na maisha (secularism) Uislamu umefanywa unahusiana na utekelezaji wa masuala ya ibadat tu (Ibada binafsi baina ya mja na Mola wake ) pamoja na akhlaq (tabia za Kiislamu). UchaMungu ni dhihirisho la mwitikio (response) wa mwanadamu kwa hisia ya kimaumbile/ ghariza ya kuabudu na kujinyenyekeza kwa Muumba baada ya mwanadamu kutambua uwepo wa Muumba na kukiri mwanadamu huyo udhaifu na mapungufu yake. Kukiri kunakotokana na akili.

Kwanini uchaMungu haufikiwi?

UchaMungu hutengemaa au kudorora kwa sababu za kinje (external factors). Sababu za kinje ni kama vile fikra (ufahamu) na mazingira anamoogelea na anamoishi mwanadamu. Tukisema ni sababu za kinje, ni kwa maana fikra na muundo wa mazingira yake. Mambo haya mwanadamu hazalishi kutoka mwilini mwake. Bali huvibeba na kuvipata (hisi) kutoka nje ya mwili wake. Kinyume na vitu kama njaa au kiu, viashiria vya ghariza ya kubakia, ambavyo mwili wa mwanadamu kimaumbile huvizalisha.

Leo baadhi ya Waislamu wamegubikwa na wimbi kubwa la fikra za kimakosa. Wameacha fikra sahihi juu ya lengo la maisha kwamba mwanadamu yupo duniani kutafuta radhi za Allah (S.W.T) kwa kuishi kwa mujibu wa maamrisho na makatazo ya Allah. Badala yake wamebeba fikra ya kuwa mwanadamu yupo duniani kutafuta manufaa ya kushibisha kiwiliwili chake kwa kukipa sehemu kubwa ya starehe (uhuru). Kadhalika katika fikra juu ya kipimo cha vitendo vya mwanadamu. Yaani kipimo gani hutumia mwanadamu kabla ya kutenda au kutokutenda kitendo. Wakapima vitendo vyao kwa kipimo cha maslahi (manufaa ya kushikika). Badala ya halali na haramu. Kwa fikra kama hizi zilizobebwa na baadhi ya Waislamu leo ni ndoto uchaMungu kufikiwa. Watu huacha kuyaendea maisha kwa lengo la kutafuta radhi za Allah (S.W.T).

Aidha, baadhi ya Waislamu leo hawatizami thawabu wala dhambi, kwa kuwa hayo hayaonekani thamani ya kushikika. Wanapuuza swala, swaumu, tabia njema, zaka ,swadaka, kulingania Uislamu nk. Kwa kuwa tu mambo hayo manufaa yake si yenye kushikika katikamikono yao. Wakawa huru kutenda madhambi kuanzia ulevi, uwongo, wizi,ujambazi,utapeli,tabia mbovu , zinaa, kusengenya nk

Hayo ni kwa upande wa ushawishi wa kifikra. Ama mazingira yanayotuzunguuka leo pia si ya kiuchaMungu. Tumezunguukwa na kila aina ya uchafu na haramu. Pombe,madanguro, kumbi za miziki za kumuasi Allah (S.W.T), wanawake kwenda utupu, mchanganyiko holela baina ya wanawake na wanaume nk.  Si uwepo wa hayo tu bali yanatangazwa na kunadiwa kupitia sauti za shetani kama miziki,filamu, tamthilia, vitabu, vyombo vya habari, mtandao nk.

Kwa hivyo, mazingira yanawaita watu katika kumuasi Allah(SWT). Na kamwe  hayawahamasishi wanadamu katika kumuogopa na kuchunga mipaka ya Allah (S.W.T) maishani mwao kwa kufuata maamrisho na kuacha makatazo.

Msingi wa hili (watu kutokuwa wachaMungu) ni kutokana na fikra zao na maisha yao kusimamiwa na imani ya kikafiri ya kisekula, kutenganisha baina ya dini na maisha. Imani iliyozaa mfumo mbovu wa kibepari unaoleta maisha ya dhiki kwa wanadamu ulimwenguni kote.  Nidhamu yake ya kidemokrasia inampa mwanadamu uhuru wa kufuata matamanio ya nafsi yake badala ya kumuhamasisha kufuata njia ya uchaMungu. Allah Taala Anasema:

أَفَرَأَيْتَ مَنْ اتَّخَذَ إِلَهَهُ هَوَاهُ وَأَضَلَّهُ اللَّهُ عَلَى عِلْمٍ وَخَتَمَ عَلَى سَمْعِهِ وَقَلْبِهِ

“Je! Umemuona yule aliyefanya matamanio ya nafsi yake kuwa ndiye mungu wake, na Mwenyezi Mungu akamuacha apotee pamoja na kuwa ana elimu, na akapiga muhuri juu ya masikio yake na moyo wake…….”(TMQ 45:23).

Imeandikwa na Abdinasir

Mwanachama wa Hizb ut Tahrir Tanzania

Leave A Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.