Mapinduzi bila ya Mfumo ni Nyumba bila ya Msingi wala Paa

Tayari Zanzibar kuna maandalizi na shamrashamra nyingi za kuelekea kilele cha maadhimisho ya Mapinduzi ya mwaka 1964  yaliotokea Zanzibar.

Katika nchi changa huiyangalia dhana ya ‘mapinduzi’ kwa mtazamo finyu, potofu na kughilibu wananchi. Mapinduzi katika nchi hizo huoneshwa kana kwamba yanalingana na matukio makubwa ya mapinduzi yaliyowahi kutokea duniani kama vile Mapinduzi ya Ufaransa, Marekani, Urusi nk. Ilhali katika nchi changa wanachoshindwa kuelewa au kujisahaulisha makusudi ni kuwa, mapinduzi kama hayo tuliyoyataja na mengineyo mfano wake yalikuwa ni mapinduzi ya kimfumo, ya kujitegemea wenyewe, yaliyoleta mabadiliko ya kimsingi na sio mapinduzi kwa jina, nembo, kaulimbiu tu bila ya ajenda yoyote pana.

Tunapozungumzia suala la mapinduzi ya kimfumo ni kule mapinduzi hayo kuwa juu ya fikra msingi inayoongoza muelekeo mzima, na kuzaliwa kutokana na fikra hiyo masuluhisho mbalimbali kutatua matatizo ya dola husika. Hapo utaona kwamba Mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789, na ya Marekani mwaka 1765 yalibeba mfumo wa kibepari uliobeba nidhamu ya kisiasa ya kidemokrasia chini ya fikra ya kutenganisha dini na maisha/ usekula kuwa ndio imani yao msingi/akida iliyoibuka baada ya migongano baina ya makasisi na wanafikra wao.

Amma Mapinduzi ya Usovieti (Bolshevik Revolution 1917) yalibeba fikra ya kukana uungu, kwa mtazamo wao kwamba kila kitu hupatikana kutokana na mabadiliko ya mada, na hakuna kitu zaidi ya mada, yaani hakuna Mungu Muumba.  Hapana shaka mifumo hiyo yote miwili ni batil. Lakini kwa kuwa ni mifumo kwa udhati iliweza kuyafanya madola yao kuwa na malengo na ajenda pana katika kuyaendea waliyokusudia japo kwa muda, halafu mifumo hiyo itaanguka. Na hilo ni jambo lenye kutarajiwa kwa kuwa si mifumo ya haki. Lakini ukweli unabakia kuwa madola yaliyobeba mifumo hiyo yalikuwa au yana malengo ya mbali kinyume na nchi changa zisizokuwa na mfumo zaidi ya kudandiadandia na kuwa watumwa wa madola makubwa yaliobeba mifumo.

Mtume SAAW nae alileta mapinduzi makubwa ya kimfumo, kwa kusimamisha mfumo wa Kiislamu, kuutawalisha, kuwakomboa waarabu na wasiokuwa waarabu kutoka hali duni kwenda katika hali bora na kisha kueneza nuru ya Uislamu mashariki na magharibi ya ulimwengu. Tofauti kubwa ya mapinduzi ya Kiislamu na mapinduzi mengine kama ya kikomunisti na kibepari ni katika upande fikra iliojengewa juu yake (aqida), njia ya mapinduzi hayo na malengo yake ya mbali, ambayo kwa Uislamu ni kupata radhi za Muumba,  na katika dunia hii kutabikisha/kutawalisha nidhamu itakayotatua matatizo yote ya mwanadamu iwe kiuchumi, siasa, elimu, mahkama nk. Bila ya kusahau suluhisho msingi la kiibada ambalo mwanadamu huhitajia kuwa na fungamano la unyenyekevu wa kiibada na Muumba wake. Mtazamo huu wa Uislamu unaowafikiana na maumbile ya mwanadamu uko kinyume kabisa na mfumo wa ukomunisti ambao umetupilia mbali suala la kiroho kwa kudai kuwa hakuna Mungu Muumba,  na pia uko kinyume na ubepari uliofanya suala la uwepo Mungu, Muumba ni suala jepesi jepesi na kuyafunga mamlaka ya Mungu katika majumba ya ibada tu.

Aidha, mapinduzi ya Mtume SAAW yalikuwa ya kimsingi katika kutekeleza Uislamu katika sheria zake zote, si kama  mapinduzi ya Iran yaliyopachika baadhi ya vionjo vya Kiislamu kisha sehemu kubwa kushikilia fikra za kimagharibi ikiwemo kutambua sheria za kimataifa,  kutetea ubaguzi kwa jina la ‘utaifa’ na kushirikiana na madola maadui kuwadhuru Waislamu.

Katika hali kama hiyo utaona mapinduzi ya kimfumo katika nchi kubwa licha ya kuja na majibu na malengo mapana, yamekosa kumlenga mwanadamu kwa upana wa maumbile yake. Kimsingi, huwa ni mapinduzi yaliozaliwa kuja kufa tu.

Amma yanaoitwa mapinduzi katika nchi changa kamwe huwa sio mapinduzi, kwa maana ya kupatikana mabadiliko ya kimfumo kama tulivyotaja sifa za kimfumo. Bali huwa amma ni matukio ya mauaji, dhulma na uonevu kufuatia kuchanganyikiwa raia, au ni mbinu ya kumakinisha zaidi athari za madola makubwa ya kibepari kwa kuwagonganisha vichwa raia kwa kundi moja dhidi ya wengine kwa maslahi ya wakoloni.  Na hii ndio hali halisi ya yaliojiri ndani ya Zanzibar ndani ya mwaka 1964.

Ndani ya miaka ya khamsini na sitini dola ya Uingereza ilikabiliwa na changamoto kadhaa na ilihitaji kujizatiti haiba yake zaidi. Na hili ni kufuatia kampeni kali dhidi ya ukoloni mkongwe ilioendeshwa na Umoja wa Kisovieti na Marekani, madola mapya katika uwanja wa siasa za kimataifa. Uingereza ilibidi ibadilishe mbinu kwa kujifanya kutoa uhuru wa bendera na kuweka vibaraka watakaolinda maslahi yake kwa sura nyengine.

Kwa muktadha wa Zanzibar, Uingereza ilihisi kuwa dhana ya usultani haikubaliki tena, na kwa bahati mbaya vyama vilivyofanikiwa baada ya uchaguzi wa kunyakua uhuru wa bendera wa mwaka 1963, japo kwamba havikuwa vyama vya Kiislamu, lakini Uingereza haikukinai kwamba vitaweza kulinda vyema maslahi yake.

Kwa hivyo, Uingereza haikuwa na namna ila kusaidia na kutengeza mazingira ya vurugu na machafuko kwa sura ya mapinduzi ili kumakinisha chama ilichokikinai zaidi, nacho ni Afro-Shirazi. Pia kwa kupitia chama hicho Uingereza ingeweza kwa usahali kukakabidhi mamlaka ya Zanzibar kwa haraka kwa mtu ambaye Uingereza inamuamini zaidi ndani ya Tanganyika (Nyerere). Aidha, mkakati wa mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa ni jaribio la Uingereza la kujiepusha kuporwa ushawishi  na ubwana wake na dola la Marekani ambalo lilikuwa na shauku kubwa kuzichukuwa ngome zake hususan baada ya Marekani kuuchukuwa uongozi wa kilimwengu mara baada ya Vita vya Pili.

Ulimwengu umeshuhudia mfumo batil wa kikomunisti namna ulivyowatia watu dhiki na mashaka kisha ukaanguka kwa muanguko wa aibu na fedheh, kisha ukapotea kabisa juu ya mgongo wa ardhi. Pia tunaona leo dhiki, tabu, mashaka, dhulma, uonevu na ukandamizaji wa mfumo wa kibepari ambao nao uko katika chumba cha mahututi ukisubiri kutangazwa kifo chake. Hapana shaka yoyote Umma wa Kiislamu na wanadamu kwa jumla wanahitaji mapinduzi ya kimfumo  yatakayorejesha kusimama kwa mfumo wa haki, uadilifu na unaokubaliana na maumbile ya wanadamu, nao ni mfumo wa Uislamu ambao leo hauna dola ya kuutawalisha. Basi ni wakati muwafaka kwa Waislamu kufanya kazi kuurejesha nafasi mfumo huo. Amma kwa wasiokuwa Waislamu ni muda kwao kutafiti mfumo wa Kiislamu hasa ukizingatia kuwa mfumo uliobakia wa kibepari uko ukingoni.

 

11/01/2018

 AFISI YA HABARI

HIZB UT-TAHRIR TANZANIA

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!