Poleni kwa Ajali ya Mv. Nyerere Na Hizi Nasaha Zetu

Tunatoa mkono wa pole kwa wahanga wote wa ajali ya kivuko cha Mv.Nyerere iliyotokea  Alkhamisi 20 Septemba katika mkoa wa Mwanza. Tunawataka wawe na subra katika kipindi hiki kigumu.

Baada ya kuwafariji kwa msiba huu mkubwa na kuwataka wahanga wawe na subra kwa kuwa ndani yake kuna Qadhaa yenye maamuzi ya Muumba. Pia tuna wajibu sasa kutupia macho kwa makini matendo ya mwanaadamu katika tukio la ajali hii.

Tunasema sio sahihi kusema ati tuendelee na subra wala tusigusie udhaifu na mapungufu ya mwanadamu katika tukio hili ! Au kusema msiba usihusishwe na siasa.

Lazima iwe wazi kwamba katika matukio kama haya ya ajali, huwa kuna vitendo vya mwanaadamu katika mzunguuko wake, ambavyo ni milki ya mwanaadamu mwenyewe. Vitendo hivyo vina muongozo maalum namna ya kuvitenda au kuacha kutenda.

Hivyo, mwanaadamu hupaswa kuwajibishwa akizembea kwa vitendo hivyo katika dunia hii, na Siku ya Kiama ataulizwa kwa matendo hayo. Tunachosema hapa si kuhoji Qadhaa, tunachohoji ni vitendo vya mwanaadamu katika mzunguuko wake ndani ya ajali hii kama mwanaadamu.

Katika ajali kama hizi kama zilizotangulia awali za Mv. Bukoba, Mv Fathi, Mv. Spice nk. kunadhihirika wazi matendo ya uzembe katika uchakavu wa meli, usimamizi mbovu, udhaifu katika udhibiti wa upakiaji, kukosekana muundo mbinu thabiti katika uokozi nk. Kwa ufupi, kuna hali ya kutowajibika, dharau, kutowajali raia nk.

Suala la uchakavu wa mitambo ya kivuko hiki ni kitu kilichopigiwa kelele. Amma suala la uokoaji ndio kumedhihirika aibu isiyo na mithali kwa namna mbili: Kwanza meli hii ya Mv.Nyerere imezama maeneo ya karibu na nchi kavu. Lakini aibu kubwa zaidi ni ile inayofanana na ya ajali ya Mv. Spice Islander iliyotokea maeneo ya Nungwi, Zanzibar mwezi kama huu Septemba 2011, ambapo Idara ya uokozi wakati ajali ikitokea ilikuwa imelala fofofo, ilhali watu binafsi katika vijiji vya karibu kwa moyo wa hali ya juu ya muhanga walifanya jitihada kuokoa kwa vifaa duni. Hatimae uokozi rasmi wa serikali ulianza asubuhi. Baada ya vizee, wanawake, watoto na abiria jumla kuangamia usiku kucha.
Ndivyo hivyo ya zoezi la uokozi wa  wa Mv. Nyerere, ulipoingia usiku ilibidi usitishwe hadi kuche asubuhi. Aibu kiwango gani hii!

Huo ndio mfumo batil wa kidemokrasia, mkali katika kukusanya kodi, lakini dhaifu na una dharau katika kunusuru na kuokoa maisha ya hao walipa kodi.

Kinachodhihirika ni kuvuruga fedha nyingi za Ummah katika chaguzi, ambazo ni maangamizi kwa mtu wa chini, wakati mwengine kuwekeza katika miradi ambayo haigusi wanyonge walio wengi, na kinachobakia mwisho ni kuwagawia wanyonge hao takwimu za fedha (GDP) kwamba uchumi umekuwa, ilhali hawana walicho nacho zaidi ya tabu, mashaka na dhiki.

Nusura ya mwanadamu ni kupata mfumo mbadala kando na ubepari/demokrasia.

#UislamuNiHadharaMbadala

Maoni hayajaruhusiwa.