Polisi Tanzania wazuiya Kongamano la Hizb ut Tahrir la Kukaribisha Ramadhani

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Jeshi la Polisi kwa kiburi limepiga marufuku Kongamano la Hizb ut Tahrir la Kukaribisha Ramadhani lililokuwa lifanyike siku ya Jumamosi 20 Mei 2017 katika Hoteli ya Mayfair, Dar es Salaam. Polisi walitoa waraka wa vitisho kwa hoteli mnamo tarehe 19 Mei 2017 yakiwa yamebakia masaa machache kufanyika kongamano hilo. Kisingizio cha Polisi katika upigaji marufuku kongamano hilo ni madai yao kwamba kongamano hilo lilikuwa ni kikao cha siri chenye viashiria vya kutokuwa na malengo mazuri kwa jamii.

Sisi Hizb ut Tahrir Tanzania tunauliza, jee kikao cha siri hufanywa ndani ya ukumbi wa hoteli ulioalikwa watu zaidi ya 450? Au kikao cha siri kitaalikwa watu mbalimbali wakiwemo masheikh, maimamu, wasomi, wanasiasa, wanahabari, wanasheria, wanaharakati, wanamichezo nk? Tunauliza zaidi, jee kikao cha siri hutangazwa ndani ya tovuti na mitandao mbalimbali ya jamii waziwazi? Na kwanini taarifa za barua ya kupiga marufuku ikatolewa siku moja kabla ya mkutano na kutuarifu sisi masaa machache kabla ya kufanyika kongamano hilo?

Qadhia hii inafedhehi ziada juu ya dhulma, maonevu na mabavu ya mfumo wa kidemokrasia kama inavyodhihirika kwa serikali zake duniani kote, ambapo hudai kushikamana na kinachoitwa uhuru wa kuabudu na uhuru wa maoni ilhali kiuhalisia matamshi hayo ni kauli mbiu za udanganyifu.

Kwa unyenyekevu mkubwa, tunawaomba radhi waalikwa wote kwa mashaka yoyote yaliyowasibu kufuatia kuzuiwa kongamano hili adhimu lililokuwa na lengo la kugusia masuala nyeti likiwemo la kufeli kwa mfumo wa kibepari kilimwengu. Aidha, kwa unyenyekevu tunawazinduwa kuwa qadhia hii ni moja ya dhihirisho la waziwazi la kutoweza kumsimamia binadamu, kutofaa na kukosa nishati kwa mfumo wa kibepari na nidhamu/system yake ya kisiasa  ya kidemokrasia, kwa kuwa vinamnyima mwanadamu kila kitu ikiwemo hata fursa ya kufanya mjadala wa masuala nyeti.

Wakati umewadia kwa kila mwanafikra makini kutafiti mfumo mbadala ambao bila ya shaka ni Uislamu na nidhamu yake ya kiutawala ya Khilafah

 

Masoud Msellem

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari

Hizb ut Tahrir Tanzania

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!