Sheikh Suleiman Amran Kilemile Ametutoka

إنا لله وإنا إليه راجعون

Kwa huzuni na masikitiko makubwa tumepokea taarifa za kufariki dunia Mwanachuoni mkubwa wa Tanzania na Afrika Mashariki, Sheikh Suleiman Amran Kilemile.
Umauti ulimfikia Sheikh usiku wa leo katika Hospitali ya Sinza, Dar es Salaam baada ya kuzidiwa na maradhi ya kisukari na baada ya kuwa mgonjwa kwa muda.

Maiti imepelekwa Masjid Thaqafa – Tandika kwa ajili ya maandalizi ya maziko.

Kifo cha Sheikh Kilemile ambae ni miongoni mwa Masheikh wakubwa na wenye elimu kubwa ni pigo na pengo jengine kubwa mno katika uwanja wa elimu ya Kiislamu na daawa sio tu Tanzania , bali Afrika Mashariki na ulimwengu mzima wa Kiislamu, kwa kuwa alikuwa bahri katika kila fani miongoni mwa fani za Kiislamu.

Marehemu amewahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Ulamaa – Bakwata, Mwenyekiti wa Hay-atu Ulamaa, ameandika na kutafsiri vitabu kadhaa na kutoa mamia kama sio maelfu ya wanafunzi wengi mahiri.

Marehemu atakumbukwa kuwa mmoja wa masheikh wachache waliokuwa wakitoa darsa za kiharakati muda mrefu katika Msikiti wa Chihota – Tandika ndani ya miaka ya themanini.

Aidha, marehemu amekuwa na mahusiano mema na walinganizi wa Uislamu ikiwemo kuwa karibu sana na vijana wa Hizb ut Tahrir Tanzania katika mchakato wa kuyarejesha upya maisha ya Kiislamu kupitia kurejesha utawala wa Kiislamu (Khilafah) itakayoaanzia katika nchi kubwa za Waislamu kwa njia ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w) isiyohusisha vitendo vya nguvu wala mabavu.

Hizb ut Tahrir Tanzania inatoa mkono wa taazia kwa Hay-atu Ulamaa, Bakwata, Umma wa Kiislamu amma, Waislamu wa Tanzania khaswa, familia, masheikh, maustadh, walimu kwa msiba huu mkubwa wa kuondokea na muhimili muhimu katika Uislamu.

Tunamuomba Allah Taala Amsamehe marehemu, Amrehemu na kumuingiza katika Jannat Firdaus. Aidha, Tunamuomba Allah Taala awalipe malipo makubwa wafiwa na kuwamakinisha kwa subra na istiqama katika kipindi hiki kizito cha Msiba

اللهم اغفر له وارحمه واسكنه في الجنة
Amiin

Sheikh Mussa Kileo
Mwenyekiti Kamati ya Mawasiliano Hizb ut Tahrir Tanzania

13 Ramadhan 1441 Hijri – 06 Mei 2020 Miladi

Maoni hayajaruhusiwa.