Siku ya Kumbukumbu ya Moi (Moi Day)

ama ilivyo ada na desturi katika serikali za kidemokrasia baadhi ya viongozi hujiwekea siku maalumu kwa ajili ya kukumbukwa, na siku hiyo kufanywa kuwa tukio maarufu katika taifa husika. Nchini Kenya ifikapo tarehe 10 Oktoba, huwa ni siku ya kumkumbuka Raisi mstaafu Daniel Arap Moi. Rais wa pili wa Jamuhuri ya Kenya.

Sherehe hii iliayosisiwa na mstaafu huyo, kando ya kupoteza gharama kubwa, wakati na nguvu ambazo lau zingetumiwa vyema, zingeleta ufanisi katika taifa, lakini huvurugwa kwa ajili ya kumtukuza kiongozi kwa kile kinachoitwa ati mchango na maendeleo aliofanya.

Sherehe hizi ni ujanja wa kufunika maovu na ukatili uliotokea chini ya utawala wake, kwa kugubikwa na kusahaulishwa raia. Mfano mzuri, ni mauaji ya kikatili ya Wagalla (Wagalla Massacre) ndani ya mwezi wa Februari 1984.
Mauaji hayo yalitendwa chini ya utawala wa Daniel Arap Moi kupitia jeshi la Kenya (KDF) chini ya usimamizi wa Joseph Nkaisery katika uwanja wa ndege wa Wajir almaarufu kama Wagalla Airstrip.

Katika mauaji hayo ya dhulma Waislamu takriban 10,000 wa jamii ya Wasomali waliuwawa, serikali ya Kenya ndani ya mwaka 2000 baada ya miaka 16 kwa mara ya kwanza ilikiri kuwa rais wake aliuwa watu 57.

Taarifa hiyo ya serikali kukiri kuwauwa kinyama raia wake, hasa wanaume waliokusanywa katika uwanja huo wa ndege kwa siku tano, na kunyimwa mahitaji yote msingi ya kibinadamu kuanzia kula hadi kunywa na hatimae kuuwawa kinyama kwa kisingizio cha kupambana na majambazi ilikuwa na utata mkubwa kwenye idadi.

Kwani licha ya madai hayo ya serikali kwamba idadi ni 57, aliyekuwa Mbunge wa Upinzani William Samoei Ruto kwa wakati ule ambaye sasa ni Makamo wa Raisi alitaja idadi kuwa ni watu 380. Huku wakazi walioshuhudia mauaji hayo wakihesabu ndugu,jamaa,marafiki na wahisani wao walitoa idadi ya watu 10,000 kuuwawa.

Huu ni mfano mmoja mmoja katika mingi namna viongozi wa kidemokrasia wanavyotumia nguvu za mamlaka yao vibaya katika kudhalilisha, kudhulumu, kutesa na kuuwa raia wao. Kisha huasisi siku maalumu ati wakumbukwe. Hapana shaka tutawakumbuka kwa uovu na dhulma zao.

Hali hiyo ni tofauti kabisa na Uislamu ambapo uongozi ni dhima kubwa na amana ambayo Siku ya Kiyama kiongozi atahesabiwa kwa namna alivyowahudumia raia wake. Kwa hili liliwapelekea viongozi wake kutekeleza majukumu yao kwa khofu ya kusimama mbele ya Allah SW, kuhesabiwa na kuadhibiwa lau hawatosimamia mambo kwa haki na uadilifu.

Allah SWT anasema katika Quran:

إِلاَّ تَفْعَلُوهُ تَكُنْ فِتْنَةٌ فِي الأَرْضِ وَفَسَادٌ كَبِيرٌ (الأنفال: 73
Msipofanya hivi, itakuwepo fitna katika ardhi na ufisadi mkubwa (TMQ 8:73)

Hussein Muhammad
Malindi – Kenya

Maoni hayajaruhusiwa.