Suluhisho La Kiislamu Kwa Changamoto Ya Wamachinga

بسم الله الرحمن الرحيم

Katika Risala ya Wiki No. 116 https://www.facebook.com/400663900784023/photos/a.403329010517512/1081381256045614/ tuliona sababu za kuibuka wamachinga katika miji hususan katika jiji kuu la wa kibiashara la Dar es Salaam, sasa tuangalie namna Uislamu unavyoweza kutatua changamoto ya wamachinga kwa namna bora na yenye kukinaisha
Hapana shaka serikali nayo tayari imeweka wazi mpango wake wa jinsi ya kukabiliana na changamoto ya ongezeko la wafanyabiashara hao, nalo ni kutenga eneo maalum kwa ajili yao.
Suluhisho hilo kimsingi ni butu lisiloweza kutatua ipasavyo tatizo hilo. Serikali ilitangaza mpango wake huo kuwa itajenga soko kubwa la wafanyabiashara hao eneo la Jangwani. Aidha, serikali imesema imetenga kiasi cha TSh32 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa soko la Kariakoo lililoungua kwa moto Julai mwaka huu (Mwananchi 04/11/2021)
Kimbilio la serikali kutenga maeneo kwa ajili ya wamachinga haligusi tatizo katika msingi wake, kwani kinachofaa ni mseto wa wafanyabiashara wakubwa kwa wadogowadogo. Kutofanikiwa matumizi ya mradi mkubwa wa Jengo la Wamachinga ‘Machinga Complex’ eneo la Karume jijini Dar es Salaam ni dhihirisho la wazi la kufeli kwa mkakati huu licha ya jengo hilo kuwa karibu na soko kuu la Kariakoo, lakini ajabu bado waandamizi wanakariri suluhisho hilo siku hadi siku.
Usimamizi wa jambo hili ni wa serikali lakini kulingana na sera za kibepari hili haliwezekani kwani katika mfumo huo wa kibepari kinachoangaliwa ni mtaji wa mtu na si hali za watu. Hivyo, serikali kuingilia kati masoko ili kutetea hali za watu fulani ni muhali kufanyika kwa sababu kufanya hivyo huhisabiwa kama ni kudhulumu maslahi ya watu wengine kwa maana ya wenye mitaji.
Katika Uislamu tatizo la wamachinga ni dogo sana kwani Uislamu katika kutatua matatizo huyaangazia kama matatizo ya kibinadamu na si kama matatizo ya kiuchumi au ya kibiashara.
Awali, serikali ya Kiislamu ya kiulimwengu (Khilafah) ingefuta kodi na tozo zote katika mfumo wa biashara kwani hali za watu ndio muhimu na ndio lengo kuu la serikali kusimamia maisha ya watu. Kwa kufanya hivyo mitaji ingeongezeka na maisha ya wafanyabiashara yangekuwa bora na hivyo wangemudu kulipa pango la nyumba za biashara/ fremu na kufanya biashara katika mfumo rasmi ambao wanatambulika na kuweza kusaidiwa.
Pili, katika kuikabili qadhia hii ni muhimu kuimarisha mseto wa wafanyabiashara ndani ya soko kwa njia mbalimbali ikiwemo kutanua miji bila ya choyo, kumakinisha nidhamu za soko, kufuta fikra za kiushindani na tamaa kupita mipaka, na kutotoa fursa kwa matajiri pekee bali kuwahakikishia nafasi na fursa kwa wafanyabiashara wadogo kwa namna yeyote ile hata kama ni kwa kuwanunulia majengo katikati ya miji na mitaa yenye soko. Kulifikia hilo kunahitajika sera zenye utu na ubinadamu ili fursa ya kutafuta maisha iwe wazi kwa kila mtu.
Tatu, Khilafah ingetoa fursa ya watu kupewa mitaji, kukopeshwa au kukopeshana kwa uadilifu bila ya masharti ya riba na ukandamizaji. Suala hili lingekuza biashara na kuongeza mzunguko wa fedha, lakini katika ubepari ni dhulma za riba na kumuongezea umasikini juu ya umaskini mnyonge anayejaribu kujinasua.
Nne, Uislamu ungehakikisha ulazima wa kila mtu kukidhi mahitajio yake ya msingi hata kwa kupewa kutoka hazina ya serikali (baitul mal) jambo ambalo huleta utulivu wa nafsi na akili kiasi cha kumzuwia mtu kushika njia haramu na batili katika utafutaji na kuhakikisha mustakabali wa uhai wake.
Mwisho, kupitia mafundisho ya Uislamu, kutakuwa na ufafanuzi wa kina wa fikra ya furaha ya mwanadamu katika uchamungu na si kupupia kukithirisha starehe za kiwiliwili, jambo linaloleta madhara makubwa kwa mtu binafsi na jamii kwa ujumla.
Serikali ya Kiislamu ya kiulimwengu (Khilafah) kwa miaka yote ya uwepo wake kabla ya kuangushwa rasmi mwaka 1924 ndani ya karne 13 na zaidi mfululizo, ilionesha mfumo wa uadilifu wa kiuchumi na kuwa kigezo cha kuigwa dunia nzima
Mfano mzuri katika utabikishaji wa nidhamu ya uadilifu ya kiuchumi katika Khilafa Uthmania ni uwepo wa aina kuu mbili ya wafanyabiashara: wanaotembea mitaani na wale ambao wamejikita katika miji ambapo walijengea vituo maalum vya biashara, masoko na maghala ikifahamika kama (Badistani) katika miji ya Busra na Edirne ndani ya Uturuki, ambapo yalizungushwa maduka na kuwekewa barabara pande zote nne ili kurahisisha wafanyabiashara wadogo wadogo na wakubwa kuwa na vituo maalum ambavyo watashughulika na biashara zao pasina kuleta usumbufu na mgongano wa kimaslahi na kimaeneo baina yao, serikali au wafanyabiashara wenzao. Jambo hilo lilipelekea kukuwa kwa miji na dola ya Kiislamu na athari yake inaendelea hadi leo nchini Uturuki hata baada ya kuangushwa dola hiyo.
Hapana shaka Khilafah itakaposimama tena kwa kuanzia katika nchi kubwa za Waislamu itayafanya haya na zaidi ya haya kwa uwezo wa Allah Taala na kueneza nuru yake ulimwengu mzima mashariki na magharibi.
Abdinasir Said
Risala ya Wiki No. 118
28 Rabi’ al-thani 1443 Hijri / 03 Disemba 2021 Miladi

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu!