Tafakuri Nyongeza Katika kifo cha Ruge Mutahaba

Nimeita makala yangu hii ‘tafakuri nyongeza kwa kifo cha Ruge’ kwa sababu tangu kujiri kifo cha Ruge Mutahaba aliyekua Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Fm. tumeshuhudia maoni na makala kadhaa za Waislamu na wasiokuwa Waislamu zilizosheheni tafakuri mbalimbali zikigusia nukta moja au nyengine kufuatia kifo hicho.

Kwa kuwa dhamira yangu ni kuandika tafakuri kwa muelekeo wa Uislamu, nimegundua katika tafakuri kadhaa zilizotangulia kwa muelekeo kama huo zimeangazia na kujikita zaidi na zaidi katika sura mbili kubwa:

Ziko tafakuri zenye kuhadharisha na kukumbusha kwamba maisha haya ya dunia ni mafupi, si lolote si chochote, yanakwenda mbio, na safari ya kudumu ni akhera. Hivyo, hatuna budi tujiandae vyema kukabili maisha hayo ya kudumu. Hizi ni nasaha adhimu, na kimsingi ndio mizania ya maisha ya Muislamu inavyopaswa kuwa.

Tafakuri nyengine zimejihusisha katika kueleza juu ya ‘hukmu ya kisheria’ juu ya Waislamu kuomboleza kifo cha asiyekuwa Muislamu, na ufafanuzi juu ya nafasi ya aliyefariki dunia ilhali sio Muislamu. Ufafanuzi wa tafakuri katika sura hii ya hukmu sharii nikiri kuwa uko sahihi na hauna tembe ya shaka juu ya uharamu wa kuomboleza kifo hicho, na kwenda motoni aliyefariki ilhali hakubeba imani ya Kiislamu, na kimsingi mfu huyo anazingirwa na laana juu ya laana:

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَمَاتُوا وَهُمْ كُفَّارٌ أُوْلَئِكَ عَلَيْهِمْ لَعْنَةُ اللَّهِ وَالْمَلاَئِكَةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ (البقرة: 161
“Hakika wale waliokufuru na wakafa hali ni makafiri, hao iko juu yao laana ya Mwenyezi Mungu, na ya Malaika na ya watu wote” (TMQ 2: 161)

Nikiri kuwa sura zote mbili za tafakuri ni zenye tija, muhimu, na ni dalili ya uhai wa Umma wetu kwa kiasi fulani, kwa kuwa waandishi wameweza kutoa sura ya Uislamu juu ya qadhia zinazojiri, ikiwemo kutoa indhari, kuonya na kukumbusha Waislamu juu ya kushikamana ipasavyo na hukmu za kisheria.

Tafakuri yangu katika makala hii kama nilivyodokeza awali ni ya nyongeza, hapana shaka pia wapo kwa kiasi fulani walioigusia tafakuri kama hii lakini najaribu kuileta kwa ufafanuzi zaidi. Ni tafakuri ambayo lau tafakuri nilizozitaja zitaunganishwa nayo zitaleta sura pana zaidi yenye tija kubwa zaidi kwa Uislamu wetu.

Tukiwa Waislamu kuna haja pia katika qadhia kama hizi za kufariki dunia wasiokuwa Waislamu tujitathmini juu ya jukumu letu adhimu la kufikisha ulinganizi wa Uislamu kwao, ni kwa kiasi gani tumefanya juhudi kuwafikishia mfumo wetu na nuru ya Uislamu kwa namna ya ufafanuzi.

Sisemi kwamba lazima wasilimu, Hashalillah! lakini walau tujiangalie na tujitathmini tuliifikisha amana na Rehma ya Uislamu kwao kwa namna inavyopaswa kufikishwa.
Kifo cha Ruge kinaakisi vifo vya wengi wasiokuwa Waislamu mfano wake, wakiwemo maarufu na wasiokuwa maarufu, ambapo Waislamu huwa tunamalizia tu kuonesha kwamba wamekula khasara kwa kufa ndani ya ukafiri, jambo ambalo ni sahihi, lakini pia tulipaswa tufungamanishe vifo hivyo kwa kujitathmini upande wetu ni kwa kiasi gani tumebeba jukumu letu la kuwafikishia ulinganizi wa Uislamu kwa ufafanuzi . Hii ni dhima kubwa kwetu.

Hapana shaka Ruge amekufa kafiri, lakini katika miamala yake maishani alizunguukwa na Waislamu wengi kila upande. Alikuwa na maswahiba wa ndani Waislamu, wafanyakazi wenzake Waislamu, marafiki, wanasiasa Waislamu, wanajamii nk. Aidha, si ajabu hata katika familia yake kuwepo Waislamu. Kwa mujibu wa Gazeti la Mwananchi la tarehe 1 Machi, kaburi la Ruge lilichimbwa katika eneo lenye makaburi mengine ya tisa ya familia wakiwemo mabibi na mababu zake wakiwemo marehemu Jafary Rwabyo (babu mdogo), Fatuma Mbeikya (dada wa babu) ambao kwa mujibu wa majina hayo wanaonekana kuwa walikuwa Waislamu.

https://www.mwananchi.co.tz/…/1597296-5004438-11…/index.html

Suala linalojitokeza katika upande wa jukumu letu, jee Ruge aliwahi kupatiwa ufafanuzi wa kina juu ya Uislamu. Awe yeye au kila asiyekuwa Muislamu tunaeamiliana nae katika maisha yetu ya kila siku.

Waislamu kwa wakati huu kuna haja sana ya kujitafakari zaidi kuhusu jukumu letu la ulinganizi kwa sababu mbili kubwa: Kwanza, haiba ya Uislamu leo imechafuliwa vya kutosha kuanzia kimataifa na kuigwa kitaifa kufuatia kampeni thaqili ya kiuadui dhidi ya Uislamu inayoendeshwa na madola ya kimagharibi ikiongozwa na Marekani.

Pili, dhana nzima ya ufuasi wa dini imedharauliwa na kudogoshwa mno katika mfumo wa kibepari chini ya fikra ya kisekula ambayo ndiyo inayofinyanga sera yao ya kielimu. Katika hali kama hiyo wasomi na wasiokuwa wasomi katika wasiokuwa Waislamu wanahitaji ufafanuzi wa kina, tena kwa hoja za kiakili ili waone nuru ya Uislamu kwa usafi wake na masuluhisho yake katika kila kipengee cha maisha ya wanadamu.

Kwa bahati mbaya Waislamu katika hili suala la ulinganizi kunadhihirika madhaifu matatu makubwa:
A. Baadhi ya Waislamu kukosa hali ya kujiamini na Uislamu wao hadi kushindwa kufanya ulinganizi.
B. Baadhi kukosa kuufahamu na kuutetea Uislamu wao kimfumo, na badala yake hulingania kwa namna ambayo haiathiri wala haigusi nafsi ya anayelinganiwa.
C. Baadhi ya Waislamu kukosa na kuacha kabisa kulingania kwa kudhani kwamba kufanya ulinganizi kwa asiyekuwa Muislamu, kutapelekea kuharibu mahusiano yao yaliyopo.

Ni muhimu sana Waislamu katika qadhia kama hizi tuonyane, tukumbushane hukmu za kisheria lakini pia muhimu zaidi tujitathmini juu ya wadhifa na jukumu letu kubwa tulilopewa na Muumba wetu la kuifikisha nuru ya Uislamu kwa wengine ili kukamilisha nafasi yetu ya kuwa mashahidi kwa wanaadamu.

وَكَذَلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطًا لِتَكُونُوا شُهَدَاءَ عَلَى النَّاسِ وَيَكُونَ الرَّسُولُ عَلَيْكُمْ شَهِيدًا
“Na ni kama hivyo tumekufanyeni Umma wa kati na kati ( bora), ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe shahidi juu yenu…..” (TMQ 2: 143)

06/03/2019

Masoud Msellem

Maoni hayajaruhusiwa.