Tatizo ni Zaidi ya Wanafunzi

Taarifa zimezagaa kuhusu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kuwachapa viboko wanafunzi 14 wa Shule ya Sekondari Kiwanja, Chunya, mkoani Mbeya waliokamatwa na simu shuleni hapo, na kudaiwa kuwa chanzo cha kuchomwa moto mabweni ya shule hiyo mnamo Oktoba Mosi 2019.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule hiyo, kitendo cha kuchomwa moto mabweni hayo yanayokaliwa na wanafunzi 150 ni kama kulipiza kisasi kufuatia msako wa simu kwa wanafunzi uliofanywa shuleni hapo tarehe 30 Septemba na kufanikiwa kukamata simu 26, na siku ya pili, Oktoba mosi mabweni yakapigwa moto.

https://www.mwananchi.co.tz/…/1597296-5296980-7q…/index.html

Ni ukweli usiopingika kwamba vitendo vya kuchoma moto mabweni ni vitendo viovu kwa kuwa huathiri, mali, uhai na masomo yenyewe katika shule husika, na yoyote anayetenda unyama huo hustahiki kuchukuliwa hatua na kulaaniwa kwa nguvu zote.

Hata hivyo, matukio kama haya na mfano wake yanapaswa kutuongoza katika mwelekeo wa kuangalia kiini na msingi wa mambo na sio matawi yake. Tukumbuke moja katika dalili kubwa ya kuanguka Umma kifikra ni kushughulika zaidi na mambo madogo madogo (trivial) na kuacha mambo makubwa na ya msingi. (vital issue)

Ni jambo la wazi kwamba hata mujibu wa sheria ambazo viongozi huapa kuzitekeleza na kuzilinda sio makosa kwa barobaro kumiliki simu, na ndio maana hata askari akimuona kijana ana simu hachukuwi hatua yoyote, kwa kuwa hajavunja sheria yoyote. Tatizo linakuja simu hizo zinatumika katika mazingira gani na kwa matumizi gani. Hakuna asiyewafiki kuwa mazingira ya shule, matumizi ya simu yatamshughulisha mwanafunzi na kuwashughulisha wengine.

Na dawa ya hilo sio kupiga marufuku simu, kuwapora au kuwachapa viboko kwa kuwa wana simu, bali ni kuwa na sera nzuri ya kudhibiti simu hizo kwa kushikiliwa kwa muda, kwa kipindi chote cha masomo mpaka muda wa kutoka shule, kisha wanafunzi wanaporudi nyumbani jioni au wanapokuwa nje ya mazingira ya darasani kama kumaliza masomo kukabidhiwa simu zao, kwa kuwa asili umiliki wa simu hizo sio makosa, pengine wanahitaji kuwasiliana na familia zao.

Amma uwepo wa suala la kuporomoka maadili kutokana na matumizi mabaya ya simu hilo lipo, na kwa udhati suala zima la kuporomoka maadili ni suala pana sana, sio kwa wanafunzi tu, bali hurejelea zaidi kwa utawala ambao ndio una dhamana kubwa kuliko yoyote kuyalinda na kuyahifadhi maadili hayo. Ni jambo la kichekesho cha karne, wakati upande mmoja kunadhibitiwa wanafunzi wasitumie simu kinyume na maadili, ilhali upande wa pili nidhamu/ utawala ndio kinara cha kuchochea na kuvunja maadili hayo.

Wakati wanafunzi wanazuiliwa simu kwa kuwa zinakoroga maadili mema, kumeruhusiwa mambo yasiyo na idadi ambayo ni ya kuchochea na kuvunja maadili, kuanzia miziki kwa jina la wasanii, kutembea nusu uchi kwa wanawake, filamu chafu nk. Hivi kweli suala la wanafunzi kumiliki simu mashuleni ni jambo kubwa na ovu kuliko wanafunzi wa kike (wanawari) kuvishwa sare nusu uchi, huku ‘wakigaragara’ muda wote pamoja na mabarobaro na walimu wa kiume, kasha ati hunadiwa kila siku kuwa idadi ya mimba za wanafunzi inaongezeka.

Ni vipi mtoto atakuwa na ghera/ hamu ya kulinda maadili mema ilhali nidhamu/ utawala haidhamini maadili hayo? Na ni jambo la kutarajiwa kuporomoka maadili kwa kuwa kwa bahati mbaya tawala za nchi changa ikiwemo Tanzania zinaburuzwa na mfumo muovu wa kimagharibi wa kibepari usio na tembe ya maadili, tahamaki tawala hizo zimeweka pembeni dini za watu wao na hata tamaduni asili za watu wao, na yanayojiri kwa wanafunzi ni natija tu/ matokeo ya hali hiyo.

Watu makini hulikabili tatizo katika msingi wake, na si kugusagusa katika mitagaa/ matawi yake. Na kwa kuwa msingi ni mfumo muovu wa kibepari, hutarajiwa na matunda yake kuwa maovu.

وَالْبَلَدُ الطَّيِّبُ يَخْرُجُ نَبَاتُهُ بِإِذْنِ رَبِّهِ وَالَّذِي خَبُثَ لاَ يَخْرُجُ إِلاَّ نَكِدًا كَذَلِكَ نُصَرِّفُ الآياتِ لِقَوْمٍ يَشْكُرُونَ (الأعراف: 58).

“Na mji mwema (ardhi njema) hutoa matunda (mema) kwa idhini ya Mola wake, na ardhi mbaya haitoi ila mimea isiyo na faida. Na hivyo ndivyo tunavyopambanua aya zetu kwa watu wanaoshukuru” ( TMQ 7: 58)

04 Oktoba 2019

Masoud Msellem

Maoni hayajaruhusiwa.