Tofauti baina ya kuwa Shingo ya Ardhi ni ya Mtu binafsi na kuwa Shingo ya Ardhi ni ya Serikali.

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Assalamu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

Samahani, katika kitabu cha nidhamu ya kiuchumi katika uislamu cha mwanachuoni mkubwa Taqiyudin Al-Nabahany (Rehema za Allah ziwe juu yake), kazungumza kuhusu ardhi ya kharaj na ardhi ya ushr…

Swali langu, nini tofauti baina ya kuwa shingo ya ardhi na manufaa yake ni ya mtu binafsi na kuwa shingo ya ardhi ni ya serikali na lakini manufaa yake ni ya mtu binafsi?

Jawabu:

Waalaykum Salam Warahmatullah Wabarakatuh,

Ardhi kwa mujibu wa hukmu za kisheria ni aina mbili:  ardhi ya ushr na ardhi ya kharaj, na aina zote hizi mbili ni sawa kubadilishana kwa kuuza, kununua, hiba, na hurithiwa kutoka kwa mmiliki wake, kwasababu (hiyo ardhi) ni umiliki wa kweli kwa mmiliki wake, kwa hiyo hufanyiwa kazi juu yake hukmu zote za umiliki. Na hakuna tofauti kati yao (hizo ardhi) isipokuwa katika mambo mawili tu. La kwanza linahusiana na kitu hasa (‘ain)  anachomiliki, la pili linahusiana na lililowajibu juu ya ile ardhi.

1-Ama linalohusiana na kitu hasa (‘ain) anachomiliki, hakika ya mmiliki wa ardhi ya ushr anamiliki shingo ya ardhi na manufaa yake, na mmiliki wa ardhi ya kharaj humiliki manufaa yake tu na hamiliki shingo yake. Na hupatikana juu ya hili kuwa hukmu ya kisheria ambayo katika sharti za kusihi kwake umiliki wa kitu chenyewe hasa (‘ain)  ni kuwa mmiliki wa ardhi ya kharaj hawezi kukifanya isipokuwa mmiliki wa ardhi ya ushr. Mfano wakf, sharti ya kusihi kwake ni umiliki hasa wa kitu chenyewe kinachowekwa wakf,  kwa hivyo mmiliki wa ardhi ya ushr atakapotaka kuweka wakf ardhi yake  ambayo anaimiliki anaweza kufanya hivyo wakati wowote ule atakapo, kwasababu yeye ndie anaemiliki kitu chenyewe hasa (‘ain), yaani shingo yake. Lakini mmiliki wa ardhi ya kharaj atakapotaka kuweka wakf ardhi yake ambayo anaimiliki, huyu hawezi kufanya hivyo, kwasababu mwenye kuweka wakf  hushurutishwa awe mmiliki wa kitu chenyewe hasa ambacho anakiweka wakf. Na mmiliki wa ardhi ya kharaj hamiliki ile ardhi yenyewe hasa (‘ainul-ardh) yaani shingo yake, bali hakika yeye anamiliki manufaa yake, kwasababu shingo yake ni umiliki wa hazina (baitul-maal )

2-Ama linalohusiana na lililowajibu juu ya ardhi, hakika ardhi ya ushr juu yake (hulipwa) ushr, na ardhi ya kharaj juu yake (hulipwa) kharaj. Na tofauti kati ya ushr na kharaj ni kama ifuatavyo:

Ushr ni juu ya kinachozalishwa na ardhi, ambapo ni serikali huchukua fungu la kumi (ushr ) ya kinachozalishwa kivitendo kutoka kwa mkulima wa ardhi ikiwa ile ardhi inanyeshelezewa maji kikawaida na mvua, na (serikali) huchukuwa nusu ya fungu la kumi (nisful-ushr)  katika kinachozalishwa kivitendo ikiwa ile ardhi inanyeshelezewa kwa umwagiliaji au njia nyengine. Muslim amepokea kutoka kwa Jabir amesema: Kasema Mtume (SAAW):

«فِيمَا سَقَتْ الْأَنْهَارُ وَالْغَيْمُ الْعُشُورُ وَفِيمَا سُقِيَ بِالسَّانِيَةِ نِصْفُ الْعُشْرِ»

“Kwa kinachonyweshelezewa na mito na mawingu (mvua) hutolewa fungu la kumi, na kinachonyweshelezewa kwa umwagiliaji hutolewa nusu ya fungu la kumi”.

Na ushr hii huzingatiwa kuwa ndio zaka, na huwekwa katika hazina (baitul-maal), na haitumiwi isipokuwa kwa ajili ya mbeya/aina katika zile mbeya nane zilizotajwa katika Aya:

﴿إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِنَ اللَّهِ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ﴾

Hakika zaka ni kwa mafakiri, masikini, wenye kuzifanyia kazi, wenye kuzoweshwa nyoyo zao, watumwa, wenye madeni, katika njia ya Allah, na aliyekatikiwa na safari, ni faradhi hiyo kutoka kwa Allah na Allah ni mjuzi mwenye hekima”.

Na haichukuliwi (ushr)  isipokuwa katika mbeya nne. Ametoa Hakim, Baihaqy na Tabarani kutoka kwa Hadithi ya Abi Musa na Muadh wakati Mtume (SAAW) alipowatuma Yemen kuwafundisha watu jambo la dini yao, akasema:

«لَا تَأْخُذَا الصَّدَقَةَ إِلَّا مِنْ هَذِهِ الْأَرْبَعَةِ: الشَّعِيرِ، وَالْحِنْطَةِ، وَالزَّبِيبِ، وَالتَّمْرِ»

“Musichukuwe zaka isipokuwa katika hivi vinne: ngano (sha’iir /barley), hintwa ( pia ni aina ya ngano/wheat), zabibu na tende”

-Ama kharaj ni juu ya ardhi, ambapo serikali huchukuwa kiwango maalumu kutoka kwa mwenye ile ardhi, serikali hukikadiria na hukiwekea kiwango maalum kulingana na kinachozalishwa na ardhi kwa makadirio ya kikawaida na sio kinachozalishwa  kivitendo hasa (al-fi’iliy),  na hukadiriwa ile ardhi kwa kiasi inavyohimili ili asidhulumiwe yule mwenye ardhi wala hazina. Na kharaj hutolewa na mwenye ardhi kila mwaka… (Umar bin Al-Khatab alimpeleka Uthman bin Haniif huko Sawad (Iraq) na akamuamrisha aipime, akaweka diham na kafiiz kwa kila jariib  iliyoamirishwa au yenye maji na itafanywa mfano huo huo. (Ameitoa Abu Yusuf katika kitabu cha Al-kharaj  kutoka kwa Amr bin Maimuun na Haritha bin Mudhrib). Na kharaj  huwekwa katika hazina ila si katika mlango wa zaka, na hutumiwa kwa njia zote inazoziona serikali kama zinavyotumiwa mali nyengine.

Nataraji maelezo haya yametosha.

Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu Rashtah

8 Jamadul Akhirah 1440H

13 February 2019CE

Maoni hayajaruhusiwa.