Trump ni Tofauti na Waliomtangulia Katika Sera Zao?

Ummah wa kiislam umekalifishwa juu ya jukumu la kuueneza ujumbe wa kiislam kwa walimwengu. Waislam tunawajibika kuufahamu ulimwengu katika hali zake zote, matatizo yake, misukumo na mashindikizo katika dola zake. Tunatakikana tuwe wenye kufuatilia shughuli na mipango ya kisiasa katika ulimwengu, ikiwemo kudadisi mikakati ya kisiasa ya serikali katika mbinu zake, na namna ya mjengeko wa mahusiano baina ya nchi na nchi. Kwa ujumla imekuwa ni lazima kwetu kuwa na utambuzi wa kihakika katika kufahamu misimamo ya siasa za kimataifa ili tuweze kufafanua mbinu za utekelezaji katika kuisimamisha Dola yetu – Khilafah, na kueneza ujumbe katika ulimwengu.

Siasa za nchi ziliosimama leo katika ulimwengu hugawanyika baina ya zile zenye mfumo na zisizo na mfumo. Dola zenye mfumo kama ilivyo Marekani huwa ni yenye fikra iliyo thabiti na isiobadilika, nayo ni kueneza mfumo wake katika ulimwengu. Twariqa au njia yake nayo huwa si yenye kubadilika, lakini mbinu zake za kufikia lengo hubadilika kulingana na mazingira yanayozunguka maudhui husika. Marekani ni nchi kiongozi katika ushawishi wa siasa za kimataifa na dola kiongozi iliobeba, kueneza, na kuhifadhi mfumo wake wa kibepari/urasilimali unaotawalishwa leo kote ulimwenguni.

Kutokana na malengo na sera za taifa la Marekani, nguvu katika nchi hiyo zimetawanywa katika Taasisi mbali mbali ambazo zinakuwa ni vizuizi kwa kila fikra ya Raisi yeyote wa dola yao. Hivyo Raisi huwa na ukomo na vizuizi vingi vya kumzuwia kupeleka sera zake binafsi. Siasa yao ni kuangalia maslahi kama ilivyo nidhamu yao ya demokrasia kuwa ni nidhamu ya kimaslahi. Fikra ya “Amerika kwanza” kama inavyotangazwa na kupigiwa debe sana na Trump inakwenda sambamba na sera yao ya kigeni. Hii ni siasa ya Amerika kwa kipindi chote na si sera au slogan tu ya Trump kama yeye. Siasa zake za kigeni zimetawaliwa na matajiri na wenye makampuni ya ukiritimba (wenye umiliki wa kipekee katika aina fulani za biashara), yaani siasa za ukoloni asili. Wakiuangalia ulimwengu uliosalia kuwa ni kama mashamba yao tu.

Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya hivi karibuni ya jinsi taifa la Marekani linavyoendesha siasa zake za kimataifa na umahiri wake katika mipango na mikakati yake chini ya fikra yake isioyumba wala kubadilika kutokana na kubadilika kwa Raisi wa dola yao:

  1. Siasa ya Marekani juu ya Urusi na China

Kabla  ya Obama hajaondoka kwenye madaraka ya urais, aliyachafua mahusiano baina ya nchi yake na Urusi, kwa kutumia kisingizio cha udukuzi wa Urusi kuathiri uchaguzi wa Marekani. Obama alitangaza tarehe 15/12/2016 kwamba Marekani italipiza kisasi dhidi ya udukuzi wa Urusi kuathiri uchaguzi wa Marekani. Pia ameishambulia nchi hiyo kwa dhihaka.  Akasema: Wao ni wadogo na madhaifu, uchumi wao hauzalishi kitu kinachohitajika na wengine, mapato yake hayatokani na chochote isipokuwa mafuta, gesi na silaha, na wala haiendelei… (Russia Today, 17/12/2016). Vitisho na vikwazo kadhaa vikatangazwa, pamoja  na kuhusishwa pia suala la Crimea – eneo lililochukuliwa na Urusi, na mapambano yanayoendelea Ukraine. Marekani katika kipindi hicho hicho ikatangaza kurejea kwa mpango wa kukuza silaha za angani dhidi ya kuendelea kwa Urusi kukuza silaha zake za nyuklia. Na kabla, yaani tarehe 2/12/2016 – ilishapitishwa na Baraza la Wawakilishi kuiongezea bajeti ya ulinzi kufikia dola bilioni 3.4 katika mwaka 2017 ili ‘kuizuwia Urusi’ (Dar el-Ikhbar, 24/12/2016), (Dot Misr, 20/12/2016); ikiwa kinacholengwa ni (kuongeza) hali tete na Urusi. Lakini Moscow kwa upande wake ilitowa majibu yasiotarajiwa na yaliyoonyesha udhaifu (Russia Today, 30/12/2016).

Msimamo huu wa Urusi ulitokana na khofu kubwa iliyokuwa nayo juu ya malengo na matokeo ya mzozo huu na Washington, lakini pia juu ya tamaa yake ya kurejesha mahusiano ya unafuu chini ya uongozi mpya wa Trump. Na kwa kutokana na Urusi ilivyo dhaifu kimtazamo wa kisiasa, ilidhani kuwa rais ajae wakati huo, Trump, atakua tafauti na Obama aliyemtangulia katika kuitazama Urusi, wakiwa wameghafilika kwamba asasi kubwa za uongozi nchini Marekani zote humuongoza rais yeyote  yule na kutoka chama chochte kile ili kuendelea katika kutekeleza siasa ya nje ya nchi yake. Na kwamba tofauti baina ya Obama na Trump ikitokezea hukusudiwa kutekeleza siasa ya Marekani iliyopangwa.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa kisiasa haionyeshi kuwa suala la udukuzi wa Urusi juu ya uchaguzi wa Marekani ndilo lililosababisha shinikizo dhidi ya Urusi kutokana na hasira ya kushindwa mgombea wa Democrat, Hillary Clinton. Kwani ingekuwa hiyo ni sababu, Obama angeliharakisha suala la mbinyo na vikwazo kabla ya Tume ya Uchaguzi (Electoral College) kuthibitisha kuchaguliwa kwa Trump kuwa Rais tarehe 19/12/2016. Wala mbinyo huo hautokani na maendeleo ya Urusi ya silaha za nyuklia na makombora kwani Urusi haina juhudi za kushindana na Marekani kimataifa, bali inaihitaji Marekani kuikubali dori ya Urusi katika siasa za kimataifa, mahitaji ambayo Marekani inayakataa yote kijumla. Hata Urusi inavyoitumikia Marekani Syria haijatosha kwa Marekani kuitambua Urusi kuwa ni dola kubwa na kuishirikisha katika kadhia nyengine za kimataifa.

Sababu za mbinyo dhidi ya Urusi

Marekani imekuwa na wasiwasi mkubwa juu ya kuinuka kwa China na kuweza kujenga uchumi mkubwa unaoweza kutishia uchumi wa Marekani ulio wa aina ya kipekee duniani. Na zaidi ya hayo ni matumizi ya kijeshi ya China yanayoshika kasi ambayo yanapita matumizi ya nchi kama Urusi, Uingereza na Ufaransa kwa pamoja; na pia programu zake nyingi za siri za kijeshi. Kwa hiyo suala la China  limekua ni jambo lenye kuwashughulisha zaidi wanasiasa wa Marekani. Alisema waziri wa ulinzi Ashton Carter “China kutengeneza ardhi kwa kufukia bahari katika bahari ya China ya kusini (South China sea) kumenyanyua uwezekano wa kuongeza nguvu za kijeshi na hatari kubwa kutokana na makadirio mabaya…”(Al-Quds Al-Arabi, 08/11/2015).

Hatari hiyo na mipango dhidi ya China iliashiriwa zamani. Katika tarehe 04/02/1972 Nixon alipofanya mkutano na mshauri wake wa mambo ya usalama wa taifa wa wakati huo, Kissinger, ili kujadili ziara ya “Nixon” ijayo kuelekea China. Kissinger akasema kumwambia rais Nixon katika mkutano huo kwamba “Wachina ni hatari kama Warusi, na kihistoria ni hatari zaidi kuliko Warusi” Akamwambia zaidi Rais Nixon kwamba baada ya miaka 20 “Rais wa Marekani ajae akiwa mwenye hekima kama nyinyi, atategemea Urusi katika siasa yake dhidi ya Wachina”

Marekani imeona ukaribu wa Urusi kwa China hivyo inataka kuutenganisha ukaribu huu kama hatua iliyo muhimu ili kuiweka mbali China na kuidhoofisha, kama ilivyofanya hapo nyuma wakati wa vita baridi, ila sasa ni kwa njia tofauti.

Kwa haya, inawezekana kufahamu vikwazo vya karibuni vya Marekani dhidi ya Urusi, pia shinikizo la Marekani dhidi ya Urusi wakati wa Obama. Na shinikizo hili ndilo walilonalo wanachama wengi wa Republican ndani ya Congress, na pia chama cha Democrat. Shinikizo hili ndio ikawa siasa mpya dhidi ya Urusi kwa lengo la kuivuta iungane pamoja na Marekani dhidi ya China. Ya kuwa uongozi wa Obama umevunja mahusiano ya Marekani na Urusi na kuyafikisha kuwa duni; lakini Urusi ina fursa ya dhahabu kwa kuja rais Trump ili kuboresha mahusiano yake na Washington! Yaani taasisi thabiti za utawala nchini Marekani kwa makusudi zilitumia muda uliobakia wa uongozi wa Obama kuharakisha hali ya mvutano na Urusi ili Urusi isiwe na njia ya uokovu na matarajio isipokuwa kwa maelewano na uongozi ujao wa Trump, uongozi ambao unaamini maelewano ya kimaslahi (deal). Kwamba kuboresha mahusiano na Urusi hakupatikani ila baada ya maelewano ya kimaslahi makubwa yenye faida pamoja nayo kuhusu China, na ili kufikia jambo hili ni kwa kutumia ujanja wa rais ajae Trump wa kumheshimu rais Putin. Na wawili hao yawezekana kuwa na itifaki kama marafiki dhidi ya China.

Kwa hivyo, vikwazo vya Obama na mvutano huu wa makusudi ni kwa lengo la kuiweka Urusi kipembeni na kuiburuza kwa Trump “rafiki yake” na njia kuwa safi kwa makubaliano ya kimaslahi ya Trump na Urusi ili kuitenga na China, bali ni kufanya uadui dhidi ya China! Hii ndio sababu yenye nguvu ya mvutano huo uliokusudiwa na Obama mwishoni mwa utawala wake ili kumuandalia njia Trump kulifikia lengo la kisiasa la Marekani lililotajwa ambalo limewekwa na asasi za Marekani kwa ajili ya zama mpya kama inavyooneshwa na viashiria. Hivyo siasa ya Marekani huamuliwa na asasi na kutekelezwa na marais, na haijalishi chama chochote kiwacho cha rais.

  1. Kujitoa kwa Trump kutoka mkataba wa nyuklia na Iran

Baada ya Obama kuidhinisha mkataba wa nyuklia na Iran na kuusifu kuwa ni ushindi, na baadae Trump kujitoa na akazingatia hilo kuwa ni ushindi, kunaweza kuzingatiwa kuwa sera za marais hao  kwa taifa la Marekani ni tofauti.

Kwa hakika mkataba huo wa nyuklia haukuwa ni ushindi wala maslahi kwa Iran, bali ni fedheha na aibu kwa Iran. Lakini kilichojitokeza ni kwa maslahi na mahitaji ya Marekani. Msingi wa asasi za Marekani ni maslahi. Pindi kunapokuwepo na hali yenye kuhitaji mkataba, basi asasi huruhusu, na Rais nae huruhusu, na mkataba hufungwa. Ikiwa maslahi yao yanahitaji kuuvunja mkataba basi huruhusu na Rais hutoa ruhusa kuvunjwa.

Marekani iliiona Iran kuwa ni nchi muhimu kuitumia katika kuendeleza utawala wa Bashar- kibaraka wa Marekani, hadi itakapompata kibaraka mbadala. Amerika ilihofia mwamko wa ummah wa Syria uliokuwa na wito wa Uislam na kutaka kutawaliwa na Uislam. Ilihofia kuanguka kwa utawala na hivyo kupelekea kuondoka kwa ushawishi wake katika eneo, kwani  katika kipindi hasa cha mwaka 2015 ushindi wa wanamapinduzi ulikuwa dhahiri. Hivyo Iran ilihitajika na Amerika kuingilia kati kwa ajili ya kuhifadhi utawala wa Syria na hivyo kuiondolea vikwazo ili iweze kuucheza mchezo wa Amerika kama ilivyowapangia. Si hivyo tu, bali Amerika imeishirikisha pia Urusi baada ya Obama kukutana na Putin tarehe 30/9/2015 kwa ajili ya lengo hilo hilo. Lakini baada ya Urusi kujifanya inayatawala mambo ya Syria yenyewe mbali na Amerika, ndipo Amerika ikaandaa mashambulizi ya anga kwenye silaha za maangamizi ndani ya Syria kwa kuiadabisha Urusi.

Baada ya utawala wa Bashar kupata nguvu mwishoni mwa kipindi cha Obama, umuhimu wa Iran ndani ya Syria haukuwepo tena kwa Amerika, kwani jukumu la moja kwa moja juu ya Syria  amekabidhiwa Uturuki na Saudi Arabia. Ndipo hatimae Rais Trump akatangaza Marekani kujitoa kwenye mkataba tarehe 08/05/2018.

Jambo jengine ambalo ni kwa maslahi ya Marekani kuuvunja mkataba ni: Kugeuza hisia za umma na watawala katika nchi za waislam kutoka kushughulishwa na uadui na unyama wa Israili dhidi ya waislam wa ki-Palestina, pamoja na uamuzi wa Marekani wa kuhamishia ubalozi wake Al-Qudus – ardhi tukufu ya Israa na Mi’raj; na kuhamishia hisia zao kwa Iran. Hivyo Trump akaitangaza Iran kuwa ni adui na kuiwacha Israili.

Kuna sababu nyengine iliyoisukuma Amerika kuvunja mkataba, nayo ni kuiadabisha Ulaya, hasa katika masuala ya biashara, kwani Ulaya ilifaidika sana na mkataba wa nyuklia na Iran. Iliweza kufunguwa mikataba ya biashara na Iran kutokana na  kuregezwa mahusiano ya biashara na Amerika.

Hitimisho

Marekani ni kama makafiri wengine waliotangulia, hawatimizi ahadi na mikataba, bali huivunja kila wakati na wala hawana hofu na Allah (swt). Wao wako mbali na maadili ya kiislam ya kuheshimu mikataba iliyofungwa, kwani Allah (swt) anasema:

(يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَوْفُوا بِالْعُقُودِ)

“Enyi mlioamini! Tekelezeni ahadi” (Al-Maida:1)

Ni jambo la wazi kwa makafiri; kwao wao ni, kueneza ufisadi katika ardhi, kuwakandamiza watu na  kila kitu. Hivyo hitajio la kuwa na Dola ya Khilafah  itakayotekeleza mikataba na kuheshimu makubaliano, kueneza uadilifu, amani na usalama ni jambo ambalo umuhimu wake unaonekana na kila mwenye chembe ya imani. Kwa  kuisimamisha Khilafah ndipo itapatikana heshima na usawa kwa wanaadamu katika ardhi. Amesema SAAW:

إِنَّمَا الْإِمَامُ جُنَّةٌ يُقَاتَلُ مِنْ وَرَائِهِ وَيُتَّقَى بِهِ

“Hakika imamu ni ngao hupiganwa nyuma yake na hujikinga kwake”     

(Muslim kutoka kwa Abu Hurayra)

 

Na: Ust: Habibu Abdallah Ali

Maoni hayajaruhusiwa.